Saturday, August 17

Mpayukaji apanga kuanzisha kanisa

0


  Image result for photos of kakobe          Baada ya Mamlaka ya Ukusanyaji na Ulaji Kodi (MUUK) kumbana askofu wa kujipachia Zach Ka-tortoise na kukuata anaweka njuluku kwenye ndoo na majaba, Mpayukaji anasukuti namna ya kuanzisha kanisa ili akaukate kwa jina la Yesu na Mungu. Maana hakujua kuwa kuwa kumbe kuna namna ambayo mchovu tena mwenye dhambi anavyoweza kujigeuza msamehe dhambi na akaishia kuwa bilionea wa kutupwa.
Isitoshe, baada ya kushuhudia matapeli wengi tena wasiopiga buku kama mimi wameanzisha NGO hizi aka Makanisa ya kuhubiri neno la Bwana na kuwatoa njuluku wachovu wajinga.  Kwanini nami nisianzishe kitu cha kunitoa hasa usawa huu ambapo vyuma vimekaza kwa kupigwa makufuli? Kwanini nisianzishe iwapo wakuda, washamba na matapeli wa kawaida wamejipachika vyeo vitakatifu huku wakifanya uchafu wao kwa jina la Bwana? Kwanini nisianzishe kitu hii lau nami nile dezo na kuukata kama wao? Nani huyu asiyependa kuukata akatakata?
Japo ni dhambi kumtumia Bwana kutengeneza ukwasi, kama kaya imelala usingizi wa pono kuendelea kusamehe walaji na wachumia tumbo kama hawa, kwanini nami nisiukate kabla mrija huu rahisi haujastukiwa na kukatwa. Nataka nichanganye njuluku hadi siku moja nijidai kuwa nina njuluku kuliko hili lisirikali ambalo halikuwa linajua siri kali za ulaji wa wenye magwanda wa kujipachika.  Kosa langu ni nini iwapo nitachanganya njuluku na kununua hadi mapipa kama yule jamaa aliyejipachika ukuu aitwaye Jose Gwajimmy? What’s wrong mimi kuwachuna kondoo wa Bwana badala ya kuwachunga wakaishia kuliwa na mifisi watu?
Ili kuwapata wapenda mkato katika kutatua matatizo yao, nitajiita Mtakatifu Mpayukaji. Maana nikijipachika cheo cha Mchungaji au Askofu hata Nabii, vimeishachafuliwa sana.  Ili kuzidi kuwachanganya nitaita dhehebu langu The Life of Important Father for Everybody (LIFE) Tabenacle of Miracles au Uhai na Maskani ya Miujiza kwa Kiingereza.  Nitaanzisha runinga yangu ya kutangaza vitu vyangu huku nikichombeza na magazeti kama matatu hivi ya kuhakikisha kila mliwaji anapata habari zangu. Nitachapisha vitambaa vilvyoandikwa Miracles is my Work au Miujiza ndiyo Kazi Yangu ili kuzidi kuwachanganya hawa wachunwaji ambao wachunaji na maaskopo wengi wa kujipachika wameishawachuna na kuwapachika mkenge.
Kuzidi kuzichanganya njuluku, nitaanzisha kampuni ya uuzaji magari ambayo itasimamiwa na vitegemezi vyangu huku mama nikiamuru ajengewe hekalu kwa vile atakuwa akinitunza vizuri niwalize vizuri. Kupitia deal hili lazima nihakikishe nachanganya njuluku vilivyo na wazee wa kodi hawanipati.
Ili kuwanasa zaidi wapenda kuukata bila kutumia akili wala kusota, nitapiga suti kali na kujitona na bling bling za bei mbaya na kuwaambia kuwa haya yote ni matokeo ya miujiza wasijue miujiza yenyewe ni kuwachuna wao mimi kama mchunaji aka mchungaji wao.
Kuhakikisha njuluku yangu haiguswi na wasaka kodi, nitahakikisha nachimba mahandaki na kuweka njuluku huku. Acha hawa wanaoweka kwenye ndoo na vijaba. Mie lazima nichimbe mahandaki na kuhakikisha yanajaa minoti.
Ili kuwamaliza zaidi, lazima nimuarike rahis na nkewe waje kusali kwangu. Wakishafika napiga picha nao na kuzitundika kila mahali kwenye ofisi zangu ili kuhakikisha wakija vinyamkera wadogo wadogo nawatisha kuwa mimi na munene iko dugu moja katika biasara ya Mungu. Watakaozubaa nawavisha mkenge kuwa mimi ndiye nilifanya miujiza munene akaukwaa unene.
Kitu nyingine cha kulia orodo ni kuhakikisha nawatangazia wote ambao wana bi wakubwa zao wachanga na warembo wasiopata watoto waje kwangu niwape watoto wa miujiza. Hapa lazima ukisoma soma taratibu bi Mkubwa wangu asikusikie akastukia na kuharibi miujiza ninayopanga kuwafanyia hawa vidosho ili wapate watoto. Ukishawafanyia miujiza, hata wakichemsha hawawezi kuwaambiwa warume zao ili kitu uliwafanya nyuma ya pazia la miujiza.
Jukumu jingine ambalo nitalitangaza chapchap ni kuwafanyia miujiza wale walioghushi vyeti vya kitaaluma ili waendelee kupendwa na munene kama jamaa yangu Bashit. Hapa najua nitachuna wengi hasa ikizingatiwa kuwa wenene wengi ninao wajua wana elimu za kuunga unga na kughushi ghushi.  Kwa wale waliokwishafukuzwa tokana na kughushi, nitawafanyia miujiza na kuwashauri wafungue kesi ya kushitaki lisirikali ili washinde na kupewa mabilioni ya njuluku. Ila kabla ya kuwaombea, mie naramba changu kwaju ili noma itakapobainika niwe nsharamba na kufanya vitu vyangu.
Mradi mwingine wa miujiza nitakaoanzisha ni kuwafanyia miujiza wale ambao vyuma vimekaza. Nitawafungulia milango ya njuluku hadi wachanganyikiwe wote tuukate. Hapa wale ambao missions zao bandarini na mipakani zimedoda nitahakikisha nawafungulia waendelee kuibia kaya kama ilivyokuwa zama zile za kaya ya shamba la bibi ambapo kila mharifu alijipigia njuluku na kuukata kama hana akili nzuri.

Kwa vile mimi ni bonge la mjanja, lazima niukate haraka kabla sheria hazijabadilishwa kiasi cha kumtaka kila mpigaji ataje alivyopata na kuutumia ukwasi wake. Hapa lazima nichangamke haraka kabla wazo langu halijaibiwa na wasaka tonge. Onyo, mie nafanya kweli na miujiza yangu ni ya kweli. Tofauti na wao, mie nasema wazi kuwa naunda dhehebu ili kuwachuna kondoo wa Bwana mchana kweupe.
Chanzo Tanzania Daima Feb., 28, 2018. Read More

Share.

About Author

Comments are closed.