Sunday, August 25

Kijiwe chalaani masupastaa uchwara wanaojiona wako juu ya sheria

0            Baada ya mamlaka kuwaijia juu waharibifu wa maadili yetu, kama Kijiwe tumekaa kuzipongezana kuwaonya hata kuwalaani wale wanaojiona wao ni masupastaa japo ni masupastaa uchwara waliolewa sifa kiasi cha kuanza kujiona wao wako juu ya sheria.
Mgoshi Machungi mwana wa Mashindei analianzisha ‘hivi jamani juzi muimsikia msanii fuani akidai eti wazii amemhujumu kwa kupiga maufuku upuuzi wao unaokiuka maadii ya kaya?’
Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anamkwanyua mic “unaongelea hawa malimbukeni wetu ambao wamelewa sifa zitokanazo na usupastaa uchwara siyo?  Nafurahi kuwa mamlaka zimeanza kula nao sahani moja kuhakikisha wanafuata maadili ya kaya. Maana, chini ya tawala za kilimbukeni zilizopituka, kaya ilikuwa imegeuka dampo la kila aina ya uchafu wa kiutamaduni wa kigeni.”
Mijjinga aliyekuwa anamalizia kikombe chake cha kwanza cha kahawa anaamua kutia guu “ni kweli, kaya yetu iligeuzwa dodoki la kunasa kila uchafu wa kigeni kiasi cha kuanza kuonekana kama ni jamii ya mataahira au wendawazimu wasiojitambua. Hivyo, kama wanakijiwe, nashauri tuwalaani wajalaana hawa huku tukiziimiza mamlaka kuwapa kibano hadi wakome na kukomaa. Haiwezekani tukaendelea kuendekeza njaa huku tukichekwa na kaya za jirani kwa ujuha na upuuzi huu utokanao na ujinga na ulimbukeni.”
Msomi Mkatatamaa anaamua kula mic “japo mada hii inaweza kuonekana si muhimu, tukiangalia tulipo, tulipotoka na tunakokwenda, kuna haja ya kutafakari kwa kina. Juzi nilimsikia Denjamani Makapi akilalamikia ilmu kuwa imeendelea kudorora wakati naye alichangia kuiua. Siku hizi usanii uliojaa ulimbukeni na ukosefu wa maadili umegeuka chanzo kimojawapo cha matokeo ya kifo cha ilmu yetu kama kaya. Vijana siku hizi hawataki kusoma. Badala yake wanatumia muda mwingi kuimba upuuzi ili wapate njuluku na kuukata kirahisi. Zamani haikuwa hivi. Je tutageuka kaya ya wasanii? Nni wataendesha kaya huko tuendako iwapo hatutakuwa na wataalamu wa kutosha tena wanaojitambua? Hii ukiiangalia inatisha sana. Hata hivyo, nashukuru kuwa dingi ameliona hili na kuamua kulishikia bango japo sijui kama wasaidizi wake wataendelea na msimamo huu. Maana wengi wanafanya kazi kwa mazoea na kutafuta kiki ili wasitumbuliwe au kutimliwa.”
Kabla ya kuendelea, Kapende anamchomekea “unaongelea njomba Makapi siyo? Japo anachosema kina mashiko, amekumbuka blanketi asubuhi hasa ikizingatiwa kuwa naye ni sehemu ya tatizo. Waliua ilmu kwa kuendekeza ulaji kiasi cha sasa kuanza kulalamika. Mlikuwa wapi wajalaana nyie ambao mlipeleka vitegemezi vyenu kwenye skuli za binafsi na ughaibuni huku mkiua elimu na mfumo mwetu? “
Kanji naye anaamua kula mic “hii leo iko naongelea ilm. Kesho tasikia nalalamikia afia. Yeye nasomesha toto yake ghaibuni natibiwa Bombey kama naugua. Kwani kama taua ilm au afia takosa nini vakati vanalipiwa vitu yote ugaibuni?”
Kapende aliyekuwa ametoka kuongea na mshirika wake wa bedroom anaamua kula mic “kimsingi, kumekuwa na kuendekezana chini ya usupastaa uchwara. Hamsikia limbukeni mmoja akimlalamikia waziri kuwa amemtilia mtima nyongo kwa kupiga marufuku nyimbo zake za kipashkuna akidai kuwa kufanya hivyo kunafanya vitegemezi vyake vikose riziki kana kwamba lazima riziki itokane na sanaa chafu? Hata hivyo, ana bahati vinginevyo ilibidi afungiwe maisha ili akauze maandazi. Si aliwahi kujiweka kwenye mtandao akijifanya kuongea slang ya kiJoji Bush kuwa ana njuluku kama hana akili nzuri. Basi, kama anazo aendeke akatumie hizo asituletee wendawazimu na ulimbukeni hapa.”
Da Sofia Lion aka Kanungaembe anamkonyeza shoga yake Gau Ngumi Linungaembe na kula mic “mwenzenu hakuna kinachoniudhi kama kuwadhalilisha akina mama kwenye miziki yao ya mitusi. Kwanini wanawavua nguo na kuonyesha laana zao utadhani kuna anayezitaka? Akina mama nasi tumezidi. Tunapewe vijisenti kumi halafu tunauza na kudhalilisha utu wetu na wanawake wote tokana na ujinga, umaskini na ushankupe.”
Mpemba aliyekuwa akisikiliza kwa makini anaamua kuchumpa na kula mic “wallahi japo akina mama mpaswa kulaumiwa, mie nadhani wa kulaumiwa zaidi ni jamii yetu iliyojirahisi na kuwa ya kidaku na kitwahuti bila sababu. Kwanini ntu acheze nziki uchi halafu ategemee kuungwa nkono? Yakhe hii yauma na kuumiza haswa jamii nzima inapogeuzwa dodoki la kubeba kila uchafu na upuuzi eti nayo waita sanaa. Sanaa gani hii zaidi ya laana?”
Mzee Maneno kama kawaida yake anaamua kuingia kivinginevyo. Anaramba mic “wenzenu wanajihadaa kuwa huu ndio usasa wakati ni ushamba na ulimbukeni wa kutupwa. Wengine wanasema huu ndiyo ujana. Kwani nani hakuwa kijana? Mbona hatukufanya upuuzi kama huu? Nashauri uwepo mkakati wa kulazimisha vijana wasome kwanza ndiyo wavamie hiyo sanaa baadaye.”
Msomi anamchomekea “mzee Maneno umetoa pwenti ya msingi. Kama vijana wetu waliogeuzwa watumwa kimaadili kwa kutaka kuukata wakati unawakata wangekuwa na elimu safi na ya kutosha, wala wasingekubali kugeuzwa watumwa wa kimaadili. Wangeweza kuwa na nyenzo ya kupima kila jambo na kufanya mambo ya maana. Kimsingi, sanaa siyo mbaya bali wasanii uchwara wanaozuzuliwa na ulimbukeni wakisukumwa na njaa na ujinga. Finish.”

Kijiwe kikiwa kinanoga si kakapita kanungaembe kakiwa uchi wa mnyama! Gues what. tuliamua kukatia bakora kakawaambie wapuuzi wenzake.
Chanzo: Tanzania Daima Leo Machi 28, 2018.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.