Saturday, August 17

JICA yatoa msaada wa Miundombinu ya BRT Jijini Dar es Salaam – Mtembezi

0


Serikali ya Tanzania imepokea msaada wa Shilingi bilioni 77.3 kutoka Serikali ya Japan kwa ajili ya kutekeleza awamu ya pili ya mradi wa ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo (New Bagamoyo Road) kuanzia makutano ya Morocco hadi Mwenge Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwenye hafla ya kutiliana saini makubaliano ya msaada huo iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Doto James aliishukuru Japan kwa msaada huo ambao utawezesha upanuzi wa barabara hiyo yenye urefu wa Kilometa  4.3 ili iweze kuwa njia nne na kuacha nafasi kwa ajili ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT).

“Upanuzi wa barabara hii sio tu unapunguza foleni Jijini Dar es Salaam, bali  ni kiunganishi muhimu kwa usafirishaji wa bidhaa kati ya Bandari ya Bagamoyo na mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na hata maeneo mengine ya nchi,” alisema Katibu Mkuu huyo.

Pia Katibu Mkuu huyo alisema kuwa Tanzania inaishukuru Japan kwa misaada mbalimbali inayotoa kwa ajili ya kufadhili miradi mingine mingi hapa nchini ikiwemo miradi ya barabara, umeme, kilimo na kadhalika.

Aidha  aliihakikishia Serikali ya Japan kuwa Tanzania itaendelea kudumisha uhusiano mzuri uliopo kati yao na kuahidi kufuatilia kwa karibu miradi yote ili kuhakikisha inajengwa kwa ubora na kiwango kinachotakiwa.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkuu kutoka Shirika la Kimataifa  la misaada la Japan (JICA), Toshio Nagase alisema kuwa  shirika hilo limekuwa likifadhili miradi mbalimbali ya usafiri Jijini Dar es Salaam ukiwemo mradi wa barabara ya juu ya TAZARA (flyover) ambao utakamilika Oktoba mwaka huu.

The post JICA yatoa msaada wa Miundombinu ya BRT Jijini Dar es Salaam appeared first on Mtembezi.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.