Sunday, August 18

ZLSC yawataka wananchi kisiwani Pemba kutotumia uhuru wa maoni vibaya

0


Mohamed Khamis

Pemba. Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC kimewataka wananchi kisiwani Pemba kutotumia vibaya uhuru wa kutoa maoni ikiwemo ikiwemo kuwatukana na kutoa maneno yasiofaa kwa viongozi.

Kauli hiyo imetokewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Harusi Miraji Mpatani, wakati alipokuwa akijibu maswali ya wananchi wa shehia ya Wingwi njuguni, wilaya ya Micheweni Pemba, kwenye mkutano wa wazi wa wilaya hiyo, juu ya namna jamii wanavyoweza kuutumia uhuru wa maoni, kujikusanya na kujiunga.

Alisema, ingawa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 18 na baadhi ya sheria nyengine, zinaeleza juu ya uhuru wa kutoa maoni, lakini pia katiba hiyo hiyo na sheria zinaelekeza namna ya kutoa maoni hayo.

Alisema haki, uhuru, sheria na katiba hazimpi nafasi mtu au kundi la watu linapotekeleza haki na wajibu wao, kumkera na kumdhalilisha mwengine, bali ni vyema kabla ya kutumia haki hizo kuangalia inavyoelekeza.

Mkurugenzi huyo, alisema katiba ikiwa ndio sheria mama, hutakiwa kufuatwa kama ilivyo, ingawa sio kosa kwenda ndani zaidi, kuona njia ambazo mtoa maoni anaweza kuzitumia bila ya kumuudhi mwengine.

“Ni kweli katiba yetu ya Zanzibar ya mwaka 1984 na ile ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania ya mwaka 1977, zote zimelekeza juu ya uhuru wa maoni, lakini hazijaelekeza matusi na maneno ya kashfa,”alifafanua.

Akizungumzia juu ya vitambulisho vya mzanzibari mkaazi, Mkurugenzi huyo Mtendaji wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ Harusi Miraji Mpatani, alisema vinamuhusu mtu alikekaa Zanzibar kwa miezi 36 mfululizo.

Alisema hata ikifika wakati sheha wa shehia husika, amekataa kumkosesha mtu haki hiyo, lazima awe na sababu za msingi, na muhusika huyo anaweza kuonana na Mkurugenzi wa vitambulisho, kulilalamikia.

“Wewe kijana ambae umekoseshwa kitambulisho na sheha wako, sio ukae na kulalamika pembeni, unatakiwa uonane na wahusika kueleza tatizo hilo, ili hatua nyingine zifuate,”alieleza.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo, alikemea vikali baadhi ya wazazi na walezi, wenye tabia ya kuwaoza waume watoto wao kabla ya kufikia miaka 18 au kumaliaza elimu ya lazima.

Awali, sheha wa shehia Wingwi njuguni wilaya ya Micheweni Ali Hamad Said, alisema kazi inayofanywa ZLSC, inafaa kuthaminiwa kutokana na kuwaamsha wananchi juu ya kujua haki na wajibu wao.

Alisema, imekuwa mashaka kwa baadhi ya wananchi kwa kutoelewa utaratibu wa baadhi ya mambo ya kiserikali, ikiwemo cheti za kuzaliwa na kitambulisho, na kuwalalamikia masheha, bila ya kujua kuwa, kuna sheria inayoongoza.

Baadhi ya wananchi wa shehia wa Wingwi Njguni, waliuomba uongozi wa Kituo hicho, kufanya ziara kama hizo mara kwa mara kwenye shehia, ili wapate uwelewa wa wambo kadhaa ya kisheria.

Kijana Abdull –karim Aboud Rubea ‘kidungo’, alisema bado kelele za wanaharakati juu ya haki sawa baina ya wanawake na waume, anasema bado ni gumu.

“Mbona mimi sielewi nyinyi wanasheria na wanaharakati mnapotutaka sisi wanaume tuwe haki sawa na wanawake, maana Muumba ameshaweka kila jambo lake sawa,”alieleza.

Nae Rashid Hamad Haji wa kijiji cha Mlindo, alisema anashangaa kuona wanafunzi wa kike, baada ya kutoroka skuli na wakitaka kuolewa, huzuiliwa ingawa kwa upande wa wanaume ni tofauti.

Awali kabla ya kuanza kwa mkutano huo, kulitanguliwa na igizo juu ya uminywaji wa uhuru wa kujieleza sehemu za kazi, lililowasilishwa na kikundi cha wasanii cha Thesode kutoka wilaya ya Mkoani Pemba.

Kituo cha huduma za sheria Zanzibar, kwa sasa kimo katika harakati za kufanya mikutano ya wazi ngazi ya wilaya, ili kukutana na wananchi na kuwafahamisha namna ya kutumia uhuru wa kujikusanya, kujiunga, kupata habari na kesho ni zamu ya wilaya ya Chakechake.

 

 

 

Share.

About Author

Leave A Reply