Sunday, August 25

Watu 31 wamefariki Dunia kwa ajali 2017-19 kisiwani Pemba

0


Pemba.Jumla  ya watu 31 wamefariki dunia kwa ajali za barabarani ndani ya Mkoa wa usini Pemba, kuanzia mwaka 2017 hadi Machi mwaka 2019.

Kati ya vifo hivyo, vilivyotokea wilaya ya Chake Chake ilikuwa na watu 25 na wilaya ya Mkoani iliripotiwa watu sita (6) waliofariki.

Akizungumza na gazeti hili kamanda wa Polisi Mkoa wa kusini Pemba, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Hassan Nassir Ali, alisema jumla ya ajali 45 ndio ziliripotiwa katika kipindi hicho, kilichopelekea vifo vya watu 31.

Alisema katika ajali hizo, 34 zilitokea Wilaya ya Chake Chake na 11 Wilaya ya Mkoani, ambapo watu 47 walijeruhiwa wakiwemo wanawake wanne (4) na wanaume 43.

“Katika ajali hizo 45, watu 31 walifariki, kati yao 27 ni wanaume na wa 4 ni wanawake, ambapo Wilaya ya Chake Chake ni 25, kati yao 23 ni wanaume na wanawake wawili na Wilaya ya Mkoani watu sita (6) waliofariki,wanne (4) ni wanaume,”alisema.

Kamanda Nassir, alieleza kuwa, kati ya majeruhi hao, Wilaya ya Chake Chake ni watu 33 wote wakiwa ni wanaume na Wiliya ya Mkoani ni 14, wanaume kumi na wanawake wanne.

Akitaja sababu zinazopelekea kutokea kwa ajali hizo alisema, ni pamoja na mwendo kasi wa madereva, kuendesha chombo bila ya hadhari, kukosekana kwa nafasi ya wapita kwa miguu (road reserve) na miundombinu chakavu ya barabara hususan maeneo ya vijijini.

Kamanda huyo alisema, mikakati waliyojipangia katika kudhibiti ajali hizo, ni kufanya msako wa mara kwa mara kwa kushirikiana na Idara nyengine, zikiwemo Bodi ya Mapato Zanzibar, Mamlaka ya mapato Tanzania, shirika la Bima na wizara Mawasiliano na Usafirishaji pamoja na kuongeza alama za barabarani.

“Mkakati mwengine tuliojiwekea ni kutoa elimu kwa wanachi kuhusu matumizi sahihi ya barabara, wakiwemo madereva na wamiliki wa vyombo vya moto ili kupunguza ajali kwenye Mkoa wetu”, aliongeza.

Aliwataka madereva , wamiliki wa vyombo vya moto na watumiaji wengine wa barabara kuzingatia matumizi sahihi ya barabara kwa kutii sheria bila ya kushurutishwa.

Baadhi ya wananchi wakizungumzia hali hio walisema nikutokana na baadhi ya madereva kuwa wazembe njiani huku wnegine wakiendesha vyombo vya moto bila leseni.

Abdalla Ridhwani alisema jeshi la polisi liwe na utaratibu wa kufanya ukaguzi kila mara katika vyombo vya moto ili kuepusha ajali hizo.

Salma Nassor nae alisema anaamini kuwa mikakati zaidi ikiwemwa bila ya shaka Zanzibar inaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani.

Share.

About Author

Leave A Reply