Sunday, August 18

Nape ataka aliemtolea bastola hadharani akamatwe

0


Na mwandishi wetu Dodoma

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye bado anaendelea kukumbuka tukio lililoibua hisa kwa wengi baada ya kutolewa bastola hadharani jinini Dar es salam.

Nape alisema licha ya kutolewa bastola hadharani mbele ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa na anashangazwa kuwa  aliyefanya kitendo hicho hajakamatwa hadi sasa.

Nape ametoa kauli hiyo leo jioni Alhamisi Aprili 25, 2019 bungeni jijini Dodoma wakati Bunge lilipokakaa kama kamati kupitisha bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani mwaka 2019/2020.

Waziri huyo wa zamani wa Habari, Utamaduni na Michezo amesema mtu huyo yupo na amekuwa akitajwa kwa jina lake na kazi anayoifanya lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

Nape alikumbana na kadhia hiyo Machi 23, 2017 ikiwa ni saa chache kupita tangu Rais John Magufuli alipotangaza kumwondoa kwenye Baraza la Mawaziri akihudumu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Baada ya kuondolewa asubuhi, siku hiyohiyo mchana Nape alipanga kufanya mkutano na waandishi wa habari katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam ambako alikuta zuio la vyombo vya dola na alipolazimisha alijikuta akitolewa bastola mbele ya waandishi wa ndani na nje akitakiwa kurudi ndani ya gari lake na asifanye mkutano huo.

Tangu kutokea kwa tukio hilo, kumekuwapo mijadala hasa ikilenga kujua kwa nini hatua hazichukuliwi kwa mtu huyo licha ya video na picha mbalimbali zinazomwonyesha akitoa bastola na kumnyooshea Nape zipo na zinasambaa mitandaoni.

Amesisitiza, “Nina amini hakutumwa na Serikali, alifanya kwa ujinga wake wa kutotumia busara kutekeleza kazi aliyotumwa. Serikali ni vizuri ikajitenga na matukio haya, busara ndogo ya kumaliza mambo haya ili wanaotumwa kutekeleza majukumu wakatumia busara..,”

Hata hivyo, Nape hakuweza kumaliza kuzungumza jambo hilo baada ya mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu kumueleza kuwa muda wake wa kuchangia umekwisha.

Mbunge huyo wa Mtama alikuwa akichangia hoja za mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa aliyeshika shilingi akitaka Serikali itoe majibu kuhusu matukio ya utekaji na watu kupotea.

Share.

About Author

Leave A Reply