Friday, August 23

Naibu Spika BLW awataka wazazibar kutoona aibu kutangaza utalii wao

0


Mohamed Khamis

Naibu  Spika wa Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma, jana amesema wakati umefika kwa wananchi wa Zanzibar kutoona aibu na kuisimulia historia ya Zanzibar kwa wageni mbali mbali wanaotembelea visiwani hapa kwa lengo la kukuza utalii.

Aliyasema hayo juzi kisiwani Unguja katika kampeni maalumu ya amka na utalii wa ndani iliofanyika katika ukumbi wa idrissa Abdulwakel kikwajuni.

Kampeni hiyo imeandaliwa na taasisi ya ‘Mwanamke Chakarika’ kwa kushirikiana na Kamisheni ya Utalii Zanzibar, na kufanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil mjini hapa, kwa lengo la kuwahamasisha wazawa kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya utalii vilivyosheheni nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na idadi kuwa ya vijana wa kike na kiume, Mgeni alisema wakati umefika kwa jamii ya Wazanzibari na Watanzania kwa jumla, kufuta dhana kwamba utalii ni kwa ajili ya wageni kutoka nje pekee.

Alichukua fursa ya uzinduzi huo, kuipongeza Serikali na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuanzisha dhana ya ‘utalii kwa wote’, pamoja na Kamisheni kwa hatua inazochukua kuitekeleza kwa vitendo.

Alisema dhana hiyo inatoa fursa kwa kila mwananchi kujitambua kwamba ni sehemu muhimu katika kuendeleza utalii nchini, ambao unaingiza asilimia 27 ya pato la nchi, sambamba na asilimia 80 ya fedha zote za kigeni zinazoingia kutokana na vyanzo mbalimbali.

Alikiri kuwa, kwa kipindi kirefu, shughuli za utalii hapa Zanzibar zimekuwa zikinasibishwa na wageni kutoka nje pekee, hali iliyofanya sekta hiyo kuonekana haijatoa fursa kwa wananchi.

Aidha alishauri, utekelezaji wa dhana ya utalii wa ndani uende sambamba na hamu ya wananchi kujifunza na kuijua historia ya maeneo mbalimbali ili wasaidie kuwaongoza wageni wanaofika nchini kwa shughuli za kitalii pale wanapohitaji taarifa zinazoihusu Zanzibar.

“Yumkini wananchi wengi bado hawazijui rasilimali na vitu vinavyowazunguka, sasa iko haja tufanye kazi kubwa kuhakikisha kila mmoja anafahamu tunu na rasilimali zilizopo nchini,” alisisitiza.

Katika muktadha huo, aliishauri Kamisheni ya Utalii kukaa pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, ili kutengeneza mpango mkakati maalumu, ikiwemo kujumuisha somo la utalii kuanzia ngazi ya msingi ili watoto wakue wakielewa thamani yake, historia yao na namna utalii unavyokuza pato na uchumi.

Mbali na kutembelea maeneo na vivutio vya utalii, Naibu Spika huyo pia alisema utalii una fursa nyingi ambazo wananchi wanaweza kuzitumia kwa kustawisha maisha yao, ikiwemo biashara za bidhaa zinazopendwa na watalii, sanaa, usafiri, huduma za afya, mapambo na nyenginezo.

“Haipendezi kuwa tunatangaza utalii wetu lakini hatuna taarifa sahihi zinazoihusu nchi wala huduma mahsusi. Inasikitisha kuona hoteli zetu zinategemea bidhaa hata za mbogamboga kutoka nje. Hili linatutangaza vibaya, tutumie fursa ya utalii kwa wote kubadilisha hali hiyo,” alisema Mgeni.

Alihitimisha kwa kuwataka vijana kujivunia amani iliyopo nchini, na kuitumia kufanya kazi yoyote halali kwa mujibu wa sheria, wakitambua kuwa wao ni sehemu ya kukuza utalii na kulijenga taifa.

Aidha aliahidi kubeba jukumu la kuwa mlezi wa kampuni ya kwanza ya kutembeza watalii iliyoanzishwa na mwanamke iitwayo Lady Tour Guide’, akisema wakiwa pamoja watakuwa na nafasi pana zaidi ya kujiinua na kushajiisha wanawake wengine kujikita katika sekta ya utalii.

 

Mapema, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud, aliwataka vijana kuchangamkia fursa zinazopatikana katika sekta ya utalii, lakini kwa kufanya mambo yasiyokinzana na sheria za nchi au kukiuka mila na silka za Wazanzibari.

Alisema, siku zote katika jambo lenye manufaa kwa taifa, wananchi wa nchi hiyo ndio wanaopaswa kuwa mstari wa mbele katika kuiendeleza, lakini si vyema watu wenye nia mbaya kupotosha dhana ya utalii kwa wote kwa maneno au kwa vitendo.

“Lazima biashara ya utalii ifanywe kwa mujibu wa sheria za nchi, atakayekiuka hilo hatutamuacha, wala asije akatafuta mwamvuli, tutakula naye sahani moja,” alitanabahisha Mkuu wa Mkoa.

Risala ya ‘Mwanamke Chakarika’ iliyosomwa na Fat-hiya Abdulhamid, ilibainisha changamoto kadhaa za sekta ya utalii, ikiwemo utegemezi wa wageni wa kimataifa unaowaweka nyuma wazawa.

Kwa sababu hiyo alisema, taasisi yao iliwasilisha  wazo la kuanzisha kampeni hiyo maalumu kwa uongozi wa Kamisheni ili kutangaza utalii wa ndani na kufikisha elimu ya utalii ili jamii ivijue na kuvitunza vivutio kwa maslahi yao na taifa kwa jumla.

Alisema kampeni hiyo yenye kaulimbiu ya ‘Tushirikiane katika kukuza utalii wa ndani’, itakuwa endelevu na itatoa fursa za kimatembezi katika vituo tafauti vya Zanzibar, ikianza jana kutoa nafasi 50 za kufanya ziara katika maeneo ya utalii.

Share.

About Author

Leave A Reply