Saturday, August 17

Okwi: Tunaenda hatua kwa hatua – Mtembezi

0


MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Simba, Emmanuel Okwi, amesema kikosi chao kinajizatiti kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbao FC na baadaye wataelekeza nguvu kwa wapinzani wao wa Kombe la Shirikisho Afrika, timu ya Al Masry ya Misri.

Vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, wanaodhaminiwa na Kampuni ya Kubahatisha Matokeo ya Michezo ya SportPesa itawakaribisha Mbao katika mchezo wa ligi hiyo utakaofanyika Jumatatu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti la nipashe jana, Okwi, alisema kuwa kila siku wanajiandaa na kujiimarisha kwa kuzingatia mchezo unaofuata na hiyo ndiyo mbinu sahihi ya kuhakikisha wanapata pointi tatu kila wanaposhuka dimbani.

Okwi alisema kuwa wataikabili Mbao FC bila kujali matokeo ya sare ya mabao 2-2 waliyopata kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza, kwa sababu kila timu inaingia tofauti katika hatua ya lala salama ambayo bingwa na klabu zinazoshuka daraja hujulikana.

“Najua wengi wanaiwaza mechi dhidi ya Al Masry, lakini kumbukeni tunamechi nyingine dhidi ya Mbao kutoka Mwanza, ni mchezo mgumu ambao tunatakiwa kupambana ili tupate pointi tatu na kujiweka katika mazingira bora ya mbio za kuwania ubingwa,” Okwi alisema.

Mshambuliaji huyo aliongeza kuwa bado katika mawazo yake hakufikiria kuwaza kuwania kiatu cha dhahabu lakini anafurahi kuona Simba iko kileleni na yeye ndiye anaongoza kwenye safu ya washambuliaji msimu huu.

“Sikupanga kuwania kiatu cha dhahabu, awali malengo yangu yalikuwa ni kuisaidia timu ili kutwaa ubingwa, lakini sasa niko kwenye nafasi hiyo, hivyo naongeza nguvu kuhakikisha pia napata tuzo hiyo kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu,” aliongeza Okwi.

Naye Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema kuwa wanawaomba mashabiki wa timu hiyo kuendeleza umoja ili waweze kutimiza malengo yao katika mechi zilizobakia za nyumbani na ugenini.

Baada ya mechi hiyo dhidi ya Mbao FC, Simba itaendelea kukaa jijini kuwasubiri Stand United kutoka Shinyanga na Machi 6 mwaka huu itawakaribisha Al Masry katika mchezo wa kwanza wa hatua ya kwanza utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.

The post Okwi: Tunaenda hatua kwa hatua appeared first on Mtembezi.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.