Tuesday, August 20

Magufuli asisitiza ukusanyaji kodi EAC – Mtembezi

0


RAIS John Magufuli amezitaka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kukusanya kodi vizuri ili ziweze kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu na kuimarisha huduma za afya kwa wananchi.

Pia, ametoa wito kwa nchi wanachama wa EAC, kusimamia vizuri rasilimali walizonazo. Kwa mujibu taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Rais Magufuli alitoa wito huo jijini Kampala nchini Uganda jana. Alisema hayo wakati akichangia katika mkutano wa wakuu wa nchi wa EAC, unaojadili maendeleo na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya sekta ya miundombinu na afya.

Kabla ya Rais Magufuli kutoa mchango wake, marais walioshiriki mkutano huo, walipokea taarifa ya mkutano wa majadiliano ya kisekta (Round Table) kuhusu mahitaji ya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya sekta ya miundombinu na afya. Ilielezwa kuwa katika miaka 10 ijayo, nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, zitahitaji dola za Marekani bilioni 78 kutekeleza miradi ya miundombinu inayopendekezwa.

Taarifa hiyo ilichangiwa na wadau mbalimbali wakiwemo marais, wawakilishi wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo, ambao walielezea njia mbalimbali za kupata fedha za kutekeleza miradi hiyo, ikiwemo kutumia Mfumo wa Ushirikiano Kati ya Serikali na Sekta binafsi (PPP). Katika mchango wake, Rais Magufuli alisema pamoja na kutumia mfumo wa PPP, ni muhimu kwa serikali za kila nchi, kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya kodi na rasilimali nyingine ili kutekeleza miradi ya miundombinu, afya na sekta nyingine.

Alitahadharisha kuwa japokuwa mfumo wa PPP ni mzuri, ni vyema wataalamu wakachukua tahadhari za kutosha ili kuepusha serikali kuingia katika mikataba isiyokuwa na maslahi kwa nchi zao kutokana na baadhi ya wadau wa sekta binafsi, kutaka kutengeneza faida kubwa kwa kupandisha gharama za miradi. Rais Magufuli alitoa mfano wa miradi mikubwa iliyoanza kutekelezwa nchini Tanzania, ukiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) na ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’ Gorge).

Alieleza kuwa Serikali ya Tanzania, imeamua kuanza kutekeleza miradi hiyo, kwa kutumia fedha zake, baada ya kufanikiwa kusimamia vizuri rasilimali zake na kubana matumizi. “Mimi naamini tukiamua tunaweza, nchi zetu zina rasilimali nyingi za kuweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Mathalani tafiti zinaonesha kuwa kama nchi zetu zitaweza kukusanya vizuri mapato ya kodi, zinaweza kutekeleza nusu ya miradi yake ya maendeleo.

“Lakini ukiachilia mbali mapato ya kodi, tunapoteza fedha nyingi kupitia utoroshaji wa rasilimali zetu, ripoti ya jopo la Umoja wa Afrika lililoongozwa na Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki imeeleza kuwa nchi za Afrika zinapoteza Dola za Marekani bilioni 150 kila mwaka kutokana na utoroshaji wa rasilimali,” alisema Rais Magufuli. Marais waliohudhuria mkutano huo ni Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir. Marais wa Rwanda na Burundi waliwakilishwa. Leo, Rais Magufuli atahudhuria mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

The post Magufuli asisitiza ukusanyaji kodi EAC appeared first on Mtembezi.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.