Sunday, August 18

Kagame, Museveni wamuunga mkono JPM – Mtembezi

0


DHAMIRA ya Rais John Magufuli ya kuijengea Tanzania miundombinu bora na ya kisasa ya usafiri na usafirishaji, imeonekana kuwagusa viongozi wa mataifa mengine wanachama ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wakiwemo Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda.

Kagame na Museveni waliokutana mwishoni mwa wiki jijini Kampala, Uganda, wameahidi kuimarisha miundombinu na ushirikiano wa kiuchumi ili kujenga uchumi imara katika nchi zao na ukanda nzima wa EAC uliolenga kusaka kwa kasi maendeleo ya viwanda.

Rais Magufuli aliahidi kushirikiana na nchi zote za Afrika Mashariki katika nyanja zote za kiuchumi hasa katika kuboresha miundombinu ili kujenga uchumi wa kisasa.

Makubaliano ya viongozi hao yameonesha dhahiri kuitikia mwito wa Rais Magufuli wa kusisitiza Afrika Mashariki lazima iwe na miundombinu imara ili kuimarisha uchumi.

Rais Magufuli alisema nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinatumia gharama kubwa kusafirisha mizigo kutokana na kuendelea kukumbatia miundombinu ya zamani isiyoendana na wakati. Aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa kipande cha reli ya kisasa ya Standard Gauge kutoka Morogoro hadi Makutopora mkoani Dodoma.

Alisema kutokana na miundombinu isiyo rafiki, usafirishaji wa kontena moja lenye urefu wa futi 20 kwa umbali usiozidi kilomita 1,500 katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unagharimu dola za kimarekani 5,000. Gharama hiyo ni kubwa ukilinganisha na usafirishaji wa kontena la ukubwa huo katika mabara mengine.

Ametolea mfano China ambapo kusafirisha kontena hilo kutoka nchi hiyo mpaka katika nchi za Afrika Mashariki umbali wa zaidi ya kilomita 9,000 pia hugharimu dola za Marekani 5,000.

Rais Magufuli alisema kutokana na ukweli huo ndio maana nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeamua kujenga miundombinu ya kisasa ya usafiri na usafirishaji ili kukidhi haja ya soko linalokua kila siku.

Rais alisema moja ya changamoto kubwa inayozikabili nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla ni kukosekana kwa miundombinu imara hali inayosababisha gharama za usafiri na usafirishaji kuwa juu ukilinganisha na mabara mengine.

Tafiti zinaonesha kuwa kukosekaa kwa miundombinu imara kunahatarisha pato la Afrika kwa asilimia moja mpaka mbili na kuongeza gharama za usafirishaji kwa asilimia 40.

“Hii ni moja ya sababu inayozifanya nchi zetu za Afrika Mashariki zishindwe kushindana na nchi zilizoendelea katika maswala ya biashara, uwekezaji na masuala ya viwanda,” alisema Rais Magufuli.

Kuna njia kuu nne za usafiri duniani yaani usafiri wa anga, usafiri wa maji, usafiri wa barabara na usafiri wa reli. Kwa mujibu wa Rais Magufuli, tafiti zimethibitisha kuwa usafiri wa reli ni bora, salama na wa haraka ukilinganisha na usafiri mwingine.

Rais Magufuli alisema usafiri wa reli una faida kubwa ukilinganisha na usafiri mwingine. Amesema ripoti ya Benki ya Maendeleo ya Afrika kuhusu usafiri wa reli barani Afrika, imesema usafiri wa reli ni muhimu kwa maendeleo bora ya kiuchumi ya bara hilo.

“Na endapo usafiri huu hautaboreshwa au kuimarishwa Afrika haitaweza kutumia rasilimali na utajiri mkubwa iliyonao kujiendeleza. Hii inadhihirisha kuwa usafiri wa reli ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi,” Rais amenukuu sehemu ya ripoti hiyo.

Kagame alimwambia Museveni kuwa nchi yake iko tayari kushirikiana na Uganda pamoja na wenzao wa Afrika Mashariki kuboresha miundombinu ili kuimarisha uchumi wa Kanda nzima. Alisema nchi za Afrika Mashariki haziwezi kushindana na nyingine katika bara la Afrika ikiwa hazitaboresha miundombinu kulingana na wakati uliopo.

The post Kagame, Museveni wamuunga mkono JPM appeared first on Mtembezi.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.