Wednesday, August 21

Bilionea Mtanzania azifunda nchi EAC – Mtembezi

0


NCHI za Afrika Mashariki zimeshauriwa kujenga viwanda vingi ili kukwepa kutengeneza soko kwa ajili ya nchi zingine zenye nguvu duniani. Hayo yamesemwa na mfanyabiashara bilionea wa Tanzania, Ali Mufuruki ambaye pia ni Mkurugenzi mwanzilishi wa Kampuni ya Infotech Investment Group Ltd alipozungumza na gazeti la Habari Leo.

Amesema soko la Afrika Mashariki lina watu zaidi ya milioni 160 likiunganishwa na ushirikiano wa nchi wanachama wa Afrika Mashariki. Lakini soko lililosainiwa jijini Kigali katika Mkutano wa Machi 21 ni kubwa mara nane ya soko la Afrika Mashariki.

Mufuruki amesema, katika miaka 20 iliyopita kuna ongezeko kubwa la biashara kati ya nchi zote sita za Afrika Mashariki kutokana na ushirikiano mzuri na unaochagizwa na kuwa na eneo moja la forodha.

Biashara hiyo pia imeimarika pia kutokana na kupunguzwa kwa vikwazo vya kibiashara katika mipaka vilivyokuwa vikikabili nchi hizi na kufanya kuwa rahisi kwa wananchi wa nchi hizo kufanya biashara au kufanya kazi katika nchi nyingine.

Kulingana na mkataba uliotiwa saini mjini Kigali, utatengeneza soko kubwa karibu mara nane ya soko la Afrika Mashariki.

Ni soko kubwa zaidi la watu zaidi ya bilioni 1.2. Katika soko hilo watu wataweza kuuza bidhaa kutoka nchi moja kwenda nyingine lakini pia kuhama kutoka nchi moja na nyingine kutafuta kazi na kuanzisha makazi au makampuni ya kibiashara.

“Kwa hiyo kupanuka kwa soko katika bara la Afrika kuwa kubwa kiasi hicho kutakuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Mufuruki.

Alisema nchi za EAC zinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa viwanda vyao kabla ya kuingia katika soko huria lililosainiwa mjini Kigali.

Bilionea huyo amesema nchi za EAC zisipojenga viwanda vingi, kuna hatari ya kuwapanulia soko watu wengine kutoka mataifa makubwa kwa kuwa soko litakuwa wazi, lakini watakaonufaika watakuwa ni watu wengine.

“Kuna haja ya nchi za Afrika Mashariki kuhakikisha kuwa zinajenga viwanda vya kutosha ili tukiuziana vitu basi tuwe tunauziana vitu vyetu na sio kuuziana vitu vya wachina au vya Waingereza, Wajerumani au Wamarekani,” aliongeza Mufuruki.

Aidha, alisema ni vizuri kuuziana vitu vilivyotengenezwa Afrika Mashariki kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine, hapo ndipo zinaweza kutengeneza faida.

Mufuruki alisema kinyume na hapo nchi hizo zitakuwa zimewatengenezea watu wengine mazingira mazuri ya biashara na kuwa hatari kwao wenyewe.

Pia katika makubaliano hayo nchi za Afrika Mashariki zina nafasi ya kutengeneza ajira kutokana na kufunguliwa milango ya soko huria katika nchi za Afrika.

Hii pia ni nafasi kwa kampuni za Afrika Mashariki kuwekeza katika mataifa mengine ya Afrika kutokana na soko kubwa litakalopatikana kutokana na makubaliano ya Kigali.

Amezisihi nchi za Afrika Mashariki kutumia nafasi hiyo ya kuwa na soko huria na kuweka mawazo chanya mbele kuwa zinaweza kufanya biashara ya ushindani na nchi zingine kama Nigeria, Afrika Kusini, Misri na nyingine.

The post Bilionea Mtanzania azifunda nchi EAC appeared first on Mtembezi.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.