Friday, April 19

WAZIRI WA AFYA UMMY MWALIMU AKABIDHI MAGARI 10,PIKIPIKI 35 KWA LENGO LA KUBORESHA SEKTA YA AFYA

0


WAZIRI wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amekabidhi magari 10 na pikipiki 35 kwa mikoa mbalimbali nchini huku akisisitiza Serikali ya Awamu ya Tano imejikita kuboresha sekta ya huduma ya afya kwa Watanzania.

Magari na pikipiki amekabidhi leo Januari 14, 2019, Mwalimu amesema tukio hilo la kukabidhi rasmi Magari 10 na Pikipiki 35 kwa uongozi wa mikoa kwa ajili ya kwenda kusimamia na kuhakikisha kwamba wananchi wanapatiwa huduma za Kifua Kikuu na Ukoma ipasavyo ni muhimu . 


“Kama mnavyofahamu bado nchi yetu inakabiliwa na janga la ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) na Ukoma. TB ni hatari kwani inasababisha vifo, na Ukoma husababisha vifo na ulemavu wa kudumu. TB pia inaongoza kusababisha vifo vingi miongoni mwa wananchi wenye VVU,” amefafanua Waziri Mwalimu.


Ameongeza kila mwaka Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa TB wapatao 154,000 ambao kati yao ni 44% (69,818) tu ndio waliogunduliwa. Changamoto kubwa ni jinsi ya kufikishia wananchi wote huduma za kufanya uchunguzi na upimaji pamoja na kuwapatia elimu ya kutosha kuhusu magonjwa hayo.


Ameongeza Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa inafanya jitihada kubwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizo ili kuongeza kasi ya ugunduzi wa ugonjwa wa TB na kwamba mojawapo ya juhudi hizo ni pamoja na ununuzi wa mashine za kupima vinasaba vya Kifua Kikuu kitaalamu Gene-Xpert.


Ambapo zimeongezeka kutoka 64 mwaka 2015 hadi 210 Disemba 2018 na kufanya 85% (158/186) ya Halmashauri zote nchini kuwa na mashine hizi zinazoweza kupima TB kwa haraka na kwa ufanisi zaidi. 

“Mashine hizo hutoa majibu ndani ya saa 2 tofauti na kipimo cha Hadubini ambazho huto majibu baada ya saa 48. Lengo ni hadi kufikia mwisho wa mwaka huu wilaya zote ziwe na mashine hizi. Kipimo hiki cha Gene-Xpert hutolewa bure,” amesema.

Waziri Mwalimu amesema Serikali hiyo imepeleka huduma ya kifua kikuu sugu karibu kwa wananchi, huduma ambayo wakati Serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani ilikuwa inapatikana katika hospitali moja tu ya Kibong’oto lakini kwa sasa inapatikana katika vituo 81 katika mikoa 23. 

“Ni katika kuongeza juhudi hizi, Serikali kupitia Wizara imenunua magari 10 na pikipiki 35 tunazozikabidhi leo kwa lengo la kuhakikisha Waratibu hawa wanawatumikia wananchi kwa kwenda kuhakikisha kama huduma zinawafikia kwa wakati.

” Magari haya 10 yamegharimu kiasi cha Sh.Milioni 611,869,741 na Pikipiki 35, zilizogharimu Sh.milioni 167,042,538. Jumla ni milioni 778. Mikoa inayopatiwa Magari ni Pwani, Songwe, Ilala II, Kilimanjaro, Lindi, Kagera, Tabora, Mtwara, Ruvuma na Rukwa. 

“Pikipiki 35 zinatolewa kwa Halmashauri 35 ambazo ni Nzega Mjini, Urambo, Kasulu, Ujiji Manispaa, Ngara, Kyerwa, Mkalama, Itigi, Msalala, Kishapu, Bariadi, Same, Mbarali, Kyela, Mbulu, Hanang, Chato, Mbozi, Ileje, Kilolo, Chamwino, Amana, Madaba, Wanging’ombe, Ilemela, Mpanda, Kalambo, Nanyumbu, Mtwara, Mbagala, Mburahati, Tanga Jiji, Muheza, Kilombero na Gairo ,” amefafanua.


Pia amesema magari hayo na Pikipiki zinazokabidhiwa kwa uongozi wa mikoa vitasaidia katika usimamizi wa shughuli za Mpango, kuhakiksha wagonjwa wa TB na Ukoma wanapatiwa elimu, wanagunduliwa na kupatiwa matibabu.


Amesema vyombo hivyo vitatumika kwa shughuli zinginezo za mikoa na wilaya zinazolenga kumfikishia huduma bora za afya mwananchi. Ametoa rai yake kwa uongozi wa Mikoa inayopatiwa vyombo hivyo vya usafirishaji vitumike kwa shughuli iliyokusudiwa kuimarisha huduma za Kifua Kikuu na Ukoma.


Amesisitiza vyombo vitumike kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo na wanaamini kwamba Mikoa hiyo itaongeza kwa kasi ugunduzi wa wagonjwa wa Kifua Kikuu na kutokomeza ugonjwa wa Ukoma katika mikoa yenu. 

Ameongeza lengo la Serikali ni kuhakikisha ifikapo 2020 tunawaibua na kuwapatia matibabu asilimia 70 ya watu wanaougua TB kutoka asilimia 48 ya hivi sasa.

Waziri Mwalimu amesema kwa upande wa ugonjwa wa Ukoma ni malengo ya Serikali kutokomeza ugonjwa huo katika Wilaya 20 zilizobakia ambazo ni Liwale, Mkinga, Nkasi, Lindi DC, Ruangwa, Nanyumbu, Shinyanga Manispaa, Kilombero, Mafya, Pangani, Mvomero, Masasi, Chato, Mpanda TC, Nachingwea, Rufiji, Korogwe, Ulanga, Morogoro DC na Kilwa DC.


Ametumia nafasi hiyo shukurani kwa Mfuko wa Dunia (GF – ATM) kwani, fedha hizo ni sehemu ya mfuko huu wa mzunguko wa 2018 – 2020.


Baadhi ya piki piki kati ya 35 na Magari 10 yatakayosambazwa katika mikoa mbalimbali, zilizokabidhiwa leo jijini Dar na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu kwa uongozi wa mikoa kwa ajili ya kwenda kusimamia na kuhakikisha kwamba wananchi wanapatiwa huduma za Kifua Kikuu na Ukoma ipasavyo. 


Mikoa 10 inayopatiwa Magari ni Pwani, Songwe, Ilala II, Kilimanjaro, Lindi, Kagera, Tabora, Mtwara, Ruvuma na Rukwa na Pikipiki 35 zinatolewa kwa Halmashauri 35 ambazo ni Nzega Mjini, Urambo, Kasulu, Ujiji Manispaa, Ngara, Kyerwa, Mkalama, Itigi, Msalala, Kishapu, Bariadi, Same, Mbarali, Kyela, Mbulu, Hanang, Chato, Mbozi, Ileje, Kilolo, Chamwino, Amana, Madaba, Wanging’ombe, Ilemela, Mpanda, Kalambo, Nanyumbu, Mtwara, Mbagala, Mburahati, Tanga Jiji, Muheza, Kilombero na Gairo.


Magari haya 10 yamegharimu kiasi cha Sh.Milioni 611,869,741 na Pikipiki 35, zilizogharimu Sh.milioni 167,042,538

Share.

About Author

Leave A Reply