Thursday, August 22

SERIKALI YAKABIDHI SHILINGI BILIONI 688.615 KWA MKANDARASI ANAYEJENGA MRADI WA UMEME WA MTO RUFIJI, TANESCO WAFURAHISHWA ….WATOA NENO

0


Na Said Mwishehe,Globu ya jamii 

SERIKALI ya Tanzania imekabidhi hundi ya fedha yenye thamani ya Sh. Bilioni 688.615 kwa mkandarasi wa Kampuni ya Arab Contractors kutoka nchini Misri anayejenga mradi wa umeme wa maporomoko ya maji ya Mto Rufiji (RHPP). 

Fedha hizo ni malipo ya awali kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo huku ikielezwa kuwa ni mara ya kwanza kwa Serikali ya Tanzania kutoa fedha nyingi kiasi hicho tena kwa mkupuo kwa ajili ya kulipa malipo ya awali kwa ajili ya mradi huo. 

Wakati Serikali inakabidhi fedha hizo kwa mkandarasi, wa ujenzi huo baadhi ya maofisa wa Wizara ya Fedha na Mipango, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO), Mkurugezi Mtendaji wa TANESCO, Mwakilishi wa Benki Kuu(BoT) pamoja na viongozi wa Wizara ya Nishati walikuwepo kushuhudia tukio hilo. 

Akizungumza baada ya kukabidhi hundi hiyo leo Aprili 24, 2019 jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Doto James amesema Wizara hiyo kwa niaba ya Serikali imekabidhi fedha hizo kwa mkandarasi wa kampuni ya Arab Contractors na fedha nyingine zilizobaki zitaendelea kulipwa hatua kwa hatua kulingana na maendeleo ya ujenzi. 

” Hazina kwa niaba ya Serikali tumekabidhi fedha Sh.bilioni 688.615 kwa mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji ni mradi wa kihistoria kwani ni utekelezaji wa wazo la muasisi wa Taifa hili Mwalim Julius Nyerere aliyelitoa mwaka 1971 na Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kutekeleza kwa kuanza ujenzi. 

“Mradi huu utakapokamilika utakuwa na megawati 2,115 ambazo zitazalishwa na kwa sasa nchi yetu kwa ujumla wake inazo mewagati 1, 602 kutoka vyanzo vyote vilivyopo nchini lakini kwa mradi huu peke yake tutakuwa tumeongeza megawati zaidi ya 2000,”amesema Katibu Mkuu James. 

Amefafanua mradi huo utakamilika baada ya miezi 36 na fedha za mradi zinatolewa na Serikali kwa asilimia 100 Kwa umuhimu wa mradi huu ndio maana Serikali imetoa fedha nyingi kwa mkupuo. “Hakuna mradi mwingine wowote ambao fedha za awali zimetolewa nyingi kiasi hicho tena kwa mara moja.Miradi mingi fedha zake hazikuwahi kuzidi Sh.bilioni 50,”amesema James. 

Amesisitiza mradi huo utakapokamilika utakuwa na manufaa makubwa kwa nchi yetu hasa kwa kuzingatia muelekeo wa Serikali ni kuwa na Tanzania ya viwanda ambapo nishati ya umeme wa uhakika inahitajika zaidi ili kuvutia wawekezaji huku akieleza faida nyingine ya mradi huo ni kwamba utakapokamilika hata bei ya umeme itapungua. 

Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa wakati wa ujenzi wa mradi huo ajira zitaongezeka kati ya 4500 hadi ajira 6000 wakati wote wa ujenzi, hivyo ni fursa kwa wananchi wa Tanzania. Pia eneo la mradi kutakuwa na uhakika wa maji kwa ajili ya umwagiliaji kutokana na maji ya maporomoko hayo. 

“Pia shughuli za utalii katika pori la Selous na faida nyingi ujenzi wa mradi huo ni kwamba hakutakuwa na mafuriko kwani maji yatajengewa kuta imara na hivyo kzuia mafuriko. Faida nyingine mradi utakapokamilika na umeme kusambaa sehemu kubwa ya nchi utasaidia utnzaji wa mazingira,”amesema James. 

Hata hivyo amefafanua kiasi cha fedha ambacho kimetolewa hadi sasa kwa ajili ya mradi huo wa umeme wa maporomoko ya Mto Rufiji ni Sh.trilioni moja kati ya Sh.trilioni sita ambazo zinahitajika kuukamilisha mradi huo. Pia amesema Serikali kupitia hazina imejipanga kufanikisha mradi huo wa kimkakati na wamejiandaa kikamilifu katika kuutekekeza. 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Dk.Hamis Mwinyimvua ameongeza kuwa Aprili 15, mwaka huu Benki ya CRDB na UBA walitoa dhamana ya fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi huo wa Rufiji. “Kutolewa kwa dhamana hizo kuliwezesha kuanza kwa baadhi ya hatua kwa mkandarasi Kwa mujibu wa mkataba asilimia 70 ni fedha zitakuwa za kigeni na asilimia 30 ni fedha za ndani. 

Fedha za kigeni tayari imelipwa kwa asilimia 70 na ndani zitaendelea kulipwa. 
“Mkandarasi kama ambavyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango alivyosema , tunakuhakikishia fedha zipo na hivyo asiwe na wasiwasi.Malipo ya awali kwa ajili ya mradi huu ni muhimu na tayari yamelipwa, hivyo ni matarajio yetu sasa vifaa vyote vinavyotakiwa kwa ajili ya kuanza ujenzi vitakwenda eneo la mradi,”amesema Dk.Mwinyumvua. 

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO Dk. Alexandra Kyazuri amesema Tanesco wamefurahi sana na kwamba umeme uliopo ni megawati 1600 na sasa kupitia mradi huo zitapatikana megawati 2000 

“Tunaishukuru Serikali chini ya Rais Dk.John Magufuli kwa uamuzi wake wa kuamua kuanza kwa mradi huo.Kwa siku ya leo hii TANESCO hatutaki kuwa na maneno mengi zaidi ya kuwa na furaha sana,”amesema Dk.Kyaruzi .

Share.

About Author

Leave A Reply