Thursday, August 22

DK.MABODI AMWAGA NEEMA KIJIJI CHA KIKOBWENI

0


 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar
Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi akizungumza katika Mkutano wa Jimbo wa
Jimbo la Chaani wa  kuelezea Utekelezaji wa Ilani ya CCM.

IMG_3592A

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar
Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi(kulia) akimsikiliza Mkaazi wa Kijiji cha
Kikobweni Ndugu Hassan Nganja(kushoto) aliyetoa maoni yake juu ya
kuwepo na upungufu wa huduma za Maji Safi katika Kijiji hicho.

IMG_3545A

BAADHI ya Wananchi wa Jimbo la Chaani wakisikiliza kwa makini taarifa mbali mbali za Utekelezaji wa Ilani katika Jimbo hilo.

IMG_3578A

MWAKILISHI wa Jimbo la Chaani
Unguja Mhe.Nadir Abdul-Tif Yussuf akizungumza na Wananchi katika Mkutano
wa Jimbo hilo katika uwanja wa Mpira wa Kijiji cha Kikobweni Wilaya ya
Kaskazini ‘A’ Unguja.

…………………….

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dk.Abudlla Juma  Saadalla Mabodi amesema CCM
itachimba Kisima cha Maji Safi na Salama kwa  muda wa Wiki mbili ili
kuondosha changamoto ya ukosefu wa huduma hiyo  kwa Wananchi wa Kijiji
cha Kikobweni Jimbo la Chaani Wilaya ya Kaskazini  ‘A’ Unguja.

Ahadi hiyo ameitoa katika Mkutano
wa Jimbo la Chaani wa kueleza  utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa Chama na
Serikali,ambapo baadhi ya  Wananchi wa kijiji hicho wamedai  kukabiliwa
na upungufu wa huduma za maji safi na kwa sasa wanatumia maji ya kisima
cha zamani cha kuvuta kwa kamba  kisichokidhi mahitaji yao.

Dk.Mabodi alisema kwa hatua ya
awali anatoa kiasi cha shilingi milioni  1.5 kwa ajili ya maandalizi ya
uchimbaji wa kisima hicho ili wananchi wa  kijiji hicho na vijiji jirani
wapate huduma hiyo kwa wakati hasa katika  mwezi Mtukufu wa Ramadhani
unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Alisema wananchi wana haki ya
kueleza changamoto zinazowakabili kwa  viongozi wao waliowapa ridhaa ya
kuwaongoza katika ngazi mbali mbali za kiuongozi katika Chama na
Serikali.

Alisema CCM ni Taasisi ya Kisiasa
inayoahidi na ikatekeleza kwa vitendo na kwa wakati mwafaka na haitoi
ahadi za kuwalaghai wananchi kama vinavyofanya baadhi ya vyama vya
upinzani kuwa wataijenga Zanzibar kwa  Siku 100 iwe kama Nchi ya
Singapore.

Alisema maendeleo hayana itikadi
wala misimamo ya kisiasa kwani inapotekelezwa Ilani ya CCM kwa
kuwafikishia wananchi huduma za maji,Umeme,Bababara na Vituo vya Afya
fursa hizo hazitumiwi na Wanachama wa CCM pekee yao bali wananufaika
wananchi wote.

Alieleza kwamba Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa sasa inatekeleza Ilani ya CCM kwa kujenga
Barabara yenye kiwango cha Lami katika Mkoa wa Kaskazini Unguja ili
kurahisisha huduma za Usafiri kwa wananchi wa Mkoa huo.

Katika maelezo yake Dk.Mabodi
aliwambia wananchi wa Jimbo la Chaani kwamba Serikali ipo katika hatua
za kutekeleza Mradi mkubwa wa Maji Safi na Salama ambapo ukikamilika
utamaliza changamoto ya upungufu wa huduma za maji Mkoani humo.

Kupitia Mkutano huo Dk.Mabodi
alielezea kuridhishwa kwake na Utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Jimbo
hilo, licha ya kuwepo kwa changamoto ndogo ndogo zinazotafutiwa ufumbuzi
wa kudumu na viongozi wa jimbo hilo.

Aliwataka Mbunge na Mwakilishi wa
Jimbo hilo watatue changamoto zilizopo katika maeneo mbali mbali ya
jimbo hilo ili Chama kishinde bila vikwazo  katika uchaguzi mkuu ujao.

Alisema CCM inapozungumzia ushindi
wake wa Kihistoria katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020, ni kutokana
na utekelezaji mzuri wa ahadi zilizotolewa kupitia Uchaguzi Mkuu
uliopita.

Pamoja na hayo aliwasihi wananchi
wa Jimbo hilo kuthamini miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwani kuna
baadhi yao wamekuwa wakihujumu miradi hiyo kwa makusudi hali
inayokwamisha baadhi ya fursa za kimaendeleo.

” Nimeshuhudia katika Mkoa huu
inahujumiwa miondombinu ya Maji Safi na Salama kwa kuiba vifaa vya
umeme,kuharibiwa kwa Gari ya wagonjwa na matukio mengine ya kukatisha
tamaa na yote hayo yanatekelezwa na watu wachache wapinga maendeleo.

Kupitia Mkutano huu nawambia
waache Tabia hizo mara moja vinginevyo mtu yeyote atakayebainika
anatekeleza uhalifu huo litakalomkuta litakuwa ni fundisho kwa watu
wengine, kwani haiwezekani mtu kuharibu miundombinu inayotegemewa na
makundi mbali mbali ya wananchi wakiwemo Wenye Mahitaji Maalum.
“,alifafanua Dk.Mabodi.

Aliwaonya baadhi ya Watendaji na
Viongozi wa Ngazi za Majimbo katika Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja,
wanaojihusisha na mipango ya kuwaandaa wagombea wa ngazi mbali mbali za
uongozi kabla ya muda wa kufanya hivyo kufika kwani kufanya hivyo ni
kukiuka Katiba ya CCM ya mwaka 1977 na miongozo yake. 

Pamoja na hayo alisema kwamba CCM
itaendelea kulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa gharama yeyote
na atakayejaribu kubeza atakuwa ni msaliti na adui wa Taifa.

 Akitoa Taarifa ya Utekelezaji wa
Ilani ya CCM Mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe.Nadir Abdul-Tif Yussuf alisema
kwa kipindi cha mwaka 2016-2017 alitekeleza masuala mbali mbali
yakiwemo kuvipatia fedha za mitaji vikundi vya ujasiriamali,alinunua
Gari maalum la Wagonjwa,kuweka Taa za umeme za kuwasha usiku Viwanja
Vitatu,kujenga visima vya Maji Safi na Salama pamoja na kununua mashine
za Kilimo za Power Tiller kwa ajili ya shughuli za Kilimo.

Miradi mingine iliyotekelezwa ni
pamoja na matengenezo ya Ofisi mbali mbali za CCM,ununuzi wa Dawa za
Binadamu katika Vituo vya Afya mbali mbali mbali pamoja na ununuzi wa
Vyarahani 10 kwa ajili ya vikundi vya Jimbo.

Mhe.Nadir alitoa alitoa tahadhari
kwa baadhi ya Watu wanaotengeneza makundi ya kuwagawa na kuwafitinisha
viongozi wa Jimbo hilo uku wakipanga wagombea kinyume na utaratibu na
kuongeza kwamba watu hao hawakitakii mema Chama Cha Mapinduzi.

Wakizungumza kwa wakati tofauti
Wananchi wa Jimbo hilo mara baada ya Mkutano huo,walieleza kwamba
wamenufaika sana na miradi inayotekelezwa na fedha za Mfuko wa Jimbo wa
Mwakilishi.

Share.

About Author

Leave A Reply