Tuesday, August 20

Tuna kila sababu ya kumuita Mother Fii

0


Tarehe 13 Februari 2018, mwanzilishi wa Sekondari ya Kifungilo Sr. Mary Fidesta Rimisho C.P.S., alitangulia mbele ya haki. Kikawaida kila mtu ana wazazi wa kumzaa, wa kumlea au wakujitolea ambao huwa wanampatia mwongozo. Sr. Fidesta, akiwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kifungilo amesimamia watoto wengi wa kike kwa kuwapatia elimu na mafunzo mengine ya Maisha.

Unapotokea msiba watu wa karibu wanaumia sana, na msiba huu wa Sr. Fidesta hauna tofauti. Wote tulimuita Mother Fii, kwani alikuwa Mama yetu. Wengi wetu tulikutana naye awali tukiwa na umri mdogo (miaka 7 hadi 18). Mother Fii alitujengea msingi imara katika kusali, kujali wengine, kujiamini, kuongoza, kuelimika na uwajibikaji. Vile vile misingi katika kupongeza na kushukuru. 

Mother Fii ni mama wa ukweli, alikuwa mwepesi kupongeza na kukemea kila wakati bila upendeleo, kiukweli usawa kwake ulikuwa muhimu. Kwa Mother Fii nidhamu ya muda ndio msingi wa kuishi kwa amani na kutimiza ahadi zote za msingi. Alitupa Kanuni ya Dhahabu, “Usimtendee mwenzako usichopenda kutendewa wewe.”

Mother Fii pia alitupa fursa ya kuendeleza vipaji mbalimbali. Tuliweza kumudu elimu, kazi za nyumbani na sasa hata  tunaendeleza msingi huu tulioupata kitambo. Wote tuliosoma Kifungilo tuna fahari kuwa familia kubwa inayojali utu wa kila mtu kutokana na uwezo na kipaji chake tu, sio fedha, mali au cheo. 
Kweli Mother Fii alikuwa zaidi ya Mwalimu kwani kama wanawake alitupatia ufunguo mkubwa katika maisha yetu.

Kweli Mother Fii mwendo umeumaliza, nasi umetuachia jukumu la kuwafundisha watoto, hasa watoto wa kike, umuhimu wa kufanya kila jambo kwa umakini. Tumekuwa viongozi, waalimu, madaktari, wanasheria, wajasiriamali na chochote tunachotaka kupitia misingi uliyotulea.

Asante sana kwa mambo yote mema 

Sr.   Fidesta (Mother Fii). 

Tutakuenzi Daima.

Pumzika kwa Amani Mama

WanakifungiloRead More

Share.

About Author

Comments are closed.