Tuesday, August 20

TAASISI YA USIMAMIZI WA VIHATARISHI YASEMA KUNA VIHATARISHI VYA KIUSALAMA KATIKA MITANDAONI

0


*Yahamasisha Watanzania wengi kujiunga na taasisi hiyo ili kuongeza idadi ya watalaam

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

TAASISI ya Usimamizi wa Vihatarishi Tanzania(IRMT) imesema kwa sasa kuna vihatarishi vingi vya kiusalama kwa njia ya mtandao huku akieleza wazi uhalifu mtandaoni nao umeshika kasi, hivyo ameshauri ni wakati muafaka kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi ili kupata mafunzo yanayohusu Usimamizi  wa Vihatarishi.

Hayo yamesemwa na Makamu wa taasisi hiyo Buyamba Buyamba wakati wa mahafali ya tatu ya Taasisi ya Usimamizi wa Vihatarishi Tanzania(IRMT) ambayo yamefanyika leo Aprili 27, 2019 jijini Dar es Salaam ambapo jumla ya wahitimu 25 wametunukiwa vyeti vya kuhitimu. 

“Tasnia hii ya Usimamizi wa vihatarishi inagusa maeneo mengi  sana na katika kipindi hiki ambacho teknolojia ndio inayotumika zaidi katika kufanya kila jambo , ni wazi watu wenye tabia ya wizi nao wanaitumia kufanya uhalifu wa mtandaoni na ukweli vihatarishi vya kiusalama mtandaoni ni vingi.Tunafaamu pia nchi yetu malipo mengi ya Serikali yanafanyika kwa njia ya mtandao, hivyo lazima idadi ya watalamu waliobebea kwenye usimamizi wa vihatarishi ikaongezeka na bahati nzuri taasisi yetu  ipo kwa ajili ya kutoa mafunzo hayo,”amesema Buyamba.

Hata hivyo amesema kwa kuwa tasnia inayohusu majanga bado changa muamko wa Watanzania kujiunga na Taasisi hiyo kwa lengo la kupata mafunzo na hatimaye kuwa watalaam bado ndogo lakini kinacholeta faraja Serikali imeweka kipaumbele katika kuhakikisha eneo la kuangalia vihatarishi linapewa kipaumbele na ametoa mfano wa taarifa za uwepo wa kimbunga Kenneth ambapo Serikali ilichukua tahadhari zote kuhakikisha hata kikitokea madhara yanakuwa si makubwa sana.

Pia amesema wamekuwa wakitoa mafunzo kwa taasisi mbalimbali ambazo zinahitaji watumishi wake kupata mafunzo ya usimamizi wa vihatarishi ambapo amesema wamefurahishwa na hatua ambazo Mamalaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutokana na uwepo wa taarifaza kimbunga Kenneth.”Taasisi yetu ilipata nafasi ya kutoa mafunzo kwa watumishi wa TMA na hakika wameonesha ukomavu katika kuchukua tahadhari baada ya kuona kuna vihatarishi vitatokea kutokana na kimbunga Kenneth,”amesisitiza.

Kuhusu mahafali hayo amesema , mwaka huu ni mahafali ya mwaka wa tatu, na jambo ambalo linawapa matumaini idadi ya wahitimu inaongezeka mwaka hadi mwaka na kufafanua mahali ya kwanza yalikuwa na wahitimu 17 lakini safari hii idadi ya wahitimu imeongezeka na hayo ni mafanikio ambayo wanajivunia nayo.

Kwa upande wake Mgeni rasmi kwenye mahafali hayo ambaye ni Mkurugenzi wa Menejimenti ya Vihatarishi na Matekelezo kutoka Benki ya CRDB Anderson Mlabwa aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Abdulmajid Nsekela , ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa pamoja na ongezeko lilitokana na wahitimu hao bado pengo la watalaam wa fani ya Usimamizi wa Vihatarishi  bado kubwa katika sekta ya umma na bifasi.

Hivyo amesema bado jitihada zinazohusisha wadau wote zinahitajika ili kuhuisha mfumo utakaowezesha wataalam wengi zaidi  kuzalishwa  na kwamba CRDB itaendelea kushirikiana na taasisi hiyo katika kukuza taaluma hiyo hiyo kwa kudhamini wafanyakazi wao kushiriki katika mafunzo mbalimbali yanayotolewa na taasisi hiyo pamoja na kuchangia utalaam wenye lengo la kuziba mapengo ya kitaaluma kwa kadiri  watakavyohitajika na pia kudhamini matukio ya kukuza na kuendeleza taaluma ya usimamizi wa vihatarishi.

“Tumekusanyika hapa kufurahia na kushuhudia kutambuliwa rasmi matunda ya jasho la watahiniwa hawa.Ninafahamu wazi wahitimu hawa waliposajiliwa kwenye taasisi kama wanafunzi walikabiliwa na changamoto kubwa mbele yao.Kwa kuhitimu wamedhihirisha umahiri wao na kupa wasaa wa kushuhudia matunda ya juhudi zao.Hivyo sina budi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB kupogeza kwa dhati uongozi , walimu na wafanyakazi wote kwa kuwapika watalaamu hao,”amesema.

Ameongeza kama ambavyo inafahamika nchi yetu  inaelekea kwenye uchumi wa viwanda kama ilivyo kauli mbiu ya Serikali iliyotolewa na Rais Dk.John Magufuli.Hivyo uchumi wa viwanda unahitaji watalaam waliobobea wa masuala ya usimamizi wa vihatarishi ili kutoa taarifa mapema ya tahadhari za mbeleni na hivyo kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kingepotea kwa kutojua yaliyoko mbele.

“Sekta binafsi  inatambua na kufurahishwa na mchango wenu na jitihada mnazofanya hasa kwa kuzingatia mazingira magumu mnayokabiliana nayo.Kadiri idadi ya watalaamu inavyoongezeka , ndivyo tunavyosonga mbele kufikia lengo letu la kuokoa fedha nyingi katika uzalishaji kwa kutoa tahadhari ya mbele kwa ufasaha na kitaalum.Nisisitize IRMT imetengeneza mtaala wake ambao umetumika kupima watunukiwa hawa kulingana na mahitaji ya ndani ya nchi na viwango vya kimataifa na hivyo kuzalisha watalaam waliojaa vitendo zaidi kuliko nadharia kitu ambacho ni tofauti sana na taasisi nyingine za nje,”amesema Mlabwa.

Pia amesema watalaam waliohitimu leo si tu mabalozi wa Taasisi ya Usimamizi wa Vihatarishi Tanzania bali pia wanategemewa kuwa dira ya muelekeo wa taasisi hiyo na kwamba tunu zao ni dhamana , na zinabeba wajibu kwa wanataaluma hao wa kuaminiwa.Hivyo lazima wazitumie kwa uadilifu , uaminifu ,bidii na kuzingatia kanuni za nidhamu na tabia njema ikiwa ishara ya kuwa wawazi na wakweli na hivyo ndivyo vitu vinavyosisitizwa sana na Serikali.

Hata hivyo amesema wahitimu hao wanapaswa kufahamu kuwa Taifa linaamini kwamba wameandaliwa vizuri na hivyo wanaweza kujiunga na kufanya kazi kwa umahiri katika Serikali na taasisi binafsi au kuendesha shughuli zao wenyewe au kwa vikundi.Hivyo popote watakapokuwa na kwa wadhifa wowote watakaokuwa nao wasisahau matendo yao tabia, hekima zao zitakuwa kioo na taswira ya taasisi hiyo na mafunzo waliyoyapata yatapimwa kwa shughuli zao za kila siku sehemu za kazi.

Wakati huo huo amesema iwapo nchi itakuwa na watalaam wa kutosha wenye ujuzi wa namna ya kusimamia vihatarishi , Taifa litaokoa fedha nyingi  kutokana na matukio ya hatari ambayo yangeepukwa kama vile mikopo chechefu, wizi katika mitandao, mikataba mibovu , miradi isiyokwisha, manunuzi hewa, mfumuko wa bei na upotevu wa mali za umma.

Awali Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi hiyo Dk.Mashaka  Mkandawile amesema kutokana na maendeleo ya kukua kwa teknolojia, taasisi hiyo imeona haja ya kutoa mafunzo hayo ya usimamizi wa vihatarishi ili kukabiliana na kila aina ya vihatarishi nchini.”Kukua kwa teknolojia kumeongeza vihatarishi na kunachangamoto nyingi hata katika sekta ya mabenki .Hivyo ni wajibu wetu kuendelea kuandaa na watalaamu wengi zaidi watakaokabiliana na kila aina ya changamoto.

“Pia ndio wakati sahihi wa waalaamu katika usimamizi wa vihatarishi kuweka mikakati ambayo itasaidia kukomesha vihatarishi vilivyopo na kutoa muelekeo wa nini kifanyike ili tuendelee kuwa salama .Tunafahamu wanaofanya uhalifu mtandaoni kila siku wanabadili mbinu, hivyo nasi kupitia watalaam wetu wanakatakiwa kuwa na mbinu mpya ili kukabiliana na wahalifu wa mitandaoni,”amesema Dk.Mkandawile.

Share.

About Author

Leave A Reply