Saturday, August 17

SERIKALI YAKUSANYA KODI YA SH.MILIONI 5554 ZA TAULO ZA KIKE

0


Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)

Serikali
imesema kuwa imekusanya Sh. Milioni 3,010.5 kwa mwaka fedha 2016/17 na
Sh. Milioni 2,545.6 kwa mwaka wa fedha 2017/18 za Kodi ya Ongezeko
la Thamani (VAT) katika taulo za kike(sanitary pads) zilizozotengenezwa
nchini na zilizoingizwa kutoka nje ya nchi.

Hayo yameelezwa
Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu maswali ya Mbunge wa Viti Maalum,
Mhe. Upendo Peneza (Chadema) aliyetaka kujua Kodi ya Ongezeko la Thamani
(VAT) iliyokusanywa na Serikali katika mwaka wa fedha wa 2016/17 na
20017/18.

Dkt. Kijaji alisema kiasi hicho cha kodi kilikusanywa
kabla ya kuondolewa kwa asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani
(VAT)Juni, 2018.

Katika maswali ya nyongeza, yaliyoulizwa na
Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Dkt. Immaculate Swale kwa niaba ya Mhe.
Peneza, alisema pamoja na Serikali kuondoa baadhi ya kodi katika
uzalishaji wa taulo za kike lakini bado bei ya bidhaa hiyo ipo juu, na
kutaka kujua mkakati wa Serikali kushusha bei ya bidhaa hiyo ili
kuhakikisha inawafikia walengwa.

“Kama Serikali imeshindwa
kusimamia kushuka kwa bei, haioni kwamba iendeleze zile kodi za awali
lakini kodi hii ikusanywe na iwe refinance ili kuweza kununulia hizi
taulo za kike na izigawe bure mashuleni”, aliongeza Dkt. Swale.

Akijibu
maswali hiyo, Dkt. Kijaji alisema kuwa Serikali haijashindwa kusimamia
bei ya bidhaa hizo na kwa sasa inaendelea kupokea maoni mbalimbali
kutoka kwa wananchi ili kuona namna bora ya kuwafikia walengwa.

Alisema
Serikali inaendelea kufanya tafiti mbalimbali ndani na nje ya nchi ili
kuona namna ya kuwasaidia watoto wa kike ila kuna changamoto kodi
inakusanywa ikiwekwa kwa ajili ya kununua na kugawa taulo za kike
mashuleni.

“Yapo makundi mengine ambayo kodi zinazotozwa kwenye
bidhaa zinazotumika na makundi hayo, tutatengeneza ombwe la kila kundi
kuja kuomba kodi inayotozwa kwenye makundi hayo waweze kupewa wao”,
alisema Dkt. Kijaji.

Aidha, Dkt. Kijaji alishauri kuwa
kinachotakiwa kufanywa ni kubuni njia nyingine ili kuona watoto wa kike
wanaweza kupata bidhaa hii bila kuhusisha kodi, au tozo zozote
zinazotozwa katika bidhaa hii kwasababu imebainika kuwa inapoondolewa
kodi wanaonufaika ni wazalishaji kwa kuwa taifa lipo katika soko huria.

Imetolewa na;

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango

Share.

About Author

Leave A Reply