Monday, August 26

Rais Magufuli afanya Ziara Rasmi ya Kitaifa nchini Namibia,afungua mtaa mkubwa uliopewa jina la Mwl. Nyerere

0


Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza
Mawaziri wa Tanzania kuitisha kikao cha Kamati ya Pamoja ya Tanzania na Namibia
(
Joint Permanent Commission – JPC)
ndani ya kipindi cha miezi 2 ili kujadiliana juu ya fursa mbalimbali za
ushirikiano wenye manufaa kwa nchi hizo.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 27 Mei, 2019 wakati wa mazungumzo
rasmi kati yake na Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Dkt. Hage Geingob
yaliyofanyika katika Ikulu ya Windhoek nchini Namibia ambako ameanza Ziara
Rasmi ya Kitaifa ya siku 2 nchini humo.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo baada ya yeye na Mhe. Rais Geingob kupokea
taarifa kuwa kikao cha JPC hakijafanyika tangu mwaka 1999 na kusababisha
masuala mengi yakiwemo ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kutopata msukumo
wa kutosha.
Amebainisha
kuwa licha ya uhusiano wa kihistoria na kidugu wa Tanzania na Namibia
ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Rais wa
Kwanza wa Namibia Mhe. Sam Nujoma, nchi hizo zimekuwa na kiwango cha chini cha
ushirikiano wa kibiashara baina yake ambapo katika mwaka uliopita biashara
iliyofanyika ilikuwa na thamani ya shilingi Bilioni 59.556 tu na kwamba nchini
Tanzania kuna kampuni 2 tu za Namibia zinazofanya biashara.
Pamoja
na kutoa maagizo hayo Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Geingob kwa
kumualika kufanya Ziara Rasmi ya Kitaifa nchini Namibia na amemhakikishia kuwa
Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano wowote unaohitajika ikiwemo kushirikiana
katika masuala ya kilimo, ufugaji, uvuvi, utalii, usafiri wa anga, biashara,
uwekezaji, utamaduni na kufundisha lugha ya Kiswahili ambacho baadhi ya nchi za
Afrika zimeridhia kianze kufundishwa katika shule zake.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amesema kwa kutambua uhusiano wa kihistoria na kidugu,
Tanzania inakamilisha maandalizi ya kufungua Ubalozi wake Jijini Windhoek ili
kurahisisha masuala mbalimbali ya uhusiano, hususani katika uchumi ambayo yapo
nyuma.
Kwa
upande wake Mhe. Rais Geingob amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kufanya ziara
hiyo na amesema Namibia inatambua na kuenzi mchango mkubwa wa Baba wa Taifa
Hayati Mwl. Nyerere na Watanzania katika juhudi za ukombozi wa Namibia.
Amefafanua
kuwa wakati wa kupigania uhuru wa Namibia, wapigania uhuru wa Namibia walipata
nafasi ya kuweka kambi yao huko Kongwa Mkoani Dodoma ambako licha ya kupiga
kambi walisaidiwa kupata mafunzo ya kijeshi na waliishi vizuri na wananchi wa
eneo hilo jambo ambalo hawatasahau.
Mhe.
Geingob ameungana na Mhe. Rais Magufuli kusisitiza umuhimu wa kutekeleza
makubaliano yatakayowekwa katika kikao cha JPC na kwamba Namibia ipo tayari
kuyatekeleza kwa maslahi ya Wanamibia na Watanzania.
Kabla
ya kufanya mazungumzo rasmi, Mhe. Rais Magufuli amefanyiwa mapokezi rasmi
ambapo amepigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi liliandaliwa kwa heshima
yake katika viwanja vya Ikulu Jijini Windhoek.
Halikadhalika,
Mhe. Rais Magufuli ametoa zawadi ya vitabu vya kusoma na kufundishia lugha ya
Kiswahili na amemhakikishia Mhe. Rais Geingob kuwa Tanzania ipo tayari kutoa
walimu na vitabu vya kufundishia Kiswahili nchini Namibia.
Nyakati
za jioni Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Geingob wamefungua rasmi mtaa mkubwa
uliopo katikati ya Jiji la Windhoek ambao umebadilishwa jina na kupewa jina la
Julius K. Nyerere ikiwa ni kuenzi mchango wake mkubwa katika ukombozi wa
Namibia na Bara zima la Afrika.
Akizungumza
katika hafla ya ufunguzi wa mtaa huo Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Rais wa
Namibia Mhe. Dkt. Geingob na Wanamibia wote kwa heshima hiyo na ameeleza kuwa
Watanzania wanajisikia faraja kuona Namibia inatambua mchango mkubwa wa Hayati
Mwl. Nyerere na Watanzania katika ukombozi wa nchi yao.
Mhe.
Rais Magufuli amebainisha kuwa Hayati Mwl. Nyerere alikuwa kiongozi shupavu, aliyepambana
na ukoloni, ubaguzi wa rangi na kupigania usawa, na ametoa wito kwa viongozi wa
Afrika kumuenzi Hayati Mwl. Nyerere na viongozi wengine wa Afrika waliotoa
mchango mkubwa wakati wa ukombozi kwa vitendo.
Meya
wa Jiji la Windhoek, Mhe. Muesee Kazapua amesema Namibia imeamua kulipanga upya
Jiji hilo na kubadili majina yote ya mitaa na kuyapa majina ya viongozi wa
Afrika waliotoa mchango mkubwa katika ukombozi na maendeleo, na kwamba mtaa
uliopewa jina la Julius K. Nyerere unaungana na mitaa mitatu yenye majina ya
viongozi waliotoa mchango mkubwa katika ukombozi ambao ni Robert Mugabe, Jan
Jonkerweg na Mandume Ndemufayo.
Katika
hafla hiyo, Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha
Mapinduzi (
CCM)
Ndg. Philip Mangula na Mtoto wa Baba wa Taifa Ndg. Makongoro Nyerere ambaye
katika salamu zake kwa niaba ya familia ameishukuru Namibia kwa kuendelea
kumuenzi na kumpa heshima Hayati Mwl. Nyerere na kwamba wanafamilia wanapokea
heshima hiyo kwa umuhimu mkubwa.
Jioni
hii, Mhe. Rais Magufuli amehudhuria Dhifa ya Kitaifa iliyoandaliwa na mwenyeji
wake Mhe. Rais Geingob kwa heshima yake. Hafla hiyo imehudhuriwa na Mke wa Rais
wa Namibia Mhe. Mama Monica Geingos, Rais Mstaafu wa Kwanza wa Namibia Mhe. Sam
Nujoma na Rais Mstaafu wa Pili wa Namibia Mhe. Hifikepunye Pohamba.
Kesho,
Mhe. Rais Magufuli atamaliza Ziara Rasmi ya Kitaifa nchini Namibia ambapo
atatembelea kiwanda cha Nyama kilichopo Jijini Windhoek na kisha ataondoka
kwenda nchini Zimbabwe ambako atafanya Ziara Rasmi ya Kitaifa kwa mwaliko wa
Rais wa Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa.

  

Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akifunua kitambaa na mwenyeji wake Rais wa Namibia Mheshimiwa Dkt. Hage Geingob kuashiria uzinduzi rasmi wa mtaa Julius K. Nyerere ulipo katika Jiji la Windhoek Nchini Namibia.Mei 27, 2019.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa mwenyeji wake Rais wa Namibia Mheshimiwa Dkt. Hage Geingob alipokuwa akimuonyesha Makongoro Nyerere mtoto wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere mtaa mpya unaoitwa JULIUS K. NYERERE uliopo katika Jiji la Windhoek Nchini Namibia.Mei 27, 2019. 

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipiga makofi na mwenyeji wake Rais wa Namibia Mheshimiwa Dkt. Hage Geingob mara baada ya kuzindua mtaa mpya wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere unaoitwa JULIUS K. NYERERE uliopo katika Jiji la Windhoek Nchini Namibia.Mei 27, 2019

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipongezana na mwenyeji wake Rais wa Namibia Mheshimiwa Dkt. Hage Geingob mara baada ya kuzindua mtaa mpya wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere unaoitwa JULIUS K. NYERERE uliopo katika Jiji la Windhoek Nchini Namibia.Mei 27, 2019

 Mtaa mpya wenye jina Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere unaoitwa JULIUS K. NYERERE ukifunuliwa rasmi mara baada ya kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na mwenyeji wake Rais wa Namibia Mheshimiwa Dkt. Hage Geingob katika Jiji la Windhoek Nchini Namibia. Mei 27, 2019

 

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimweleza Mwenyeji wake Rais wa Namibia Mheshimiwa Dkt. Hage Geingob alichokiandika kwenye kitabu cha kumbukumbu kwa Lugha ya Kiswahili Katika kuhakikisha Kiswahili kinatangazwa kimataifa mara baada ya kuwasili katika Ikulu ya Jijini Windhoek Nchini Namibia.Mei 27, 2019.

 

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akifurahi na mwenyeji wake Rais wa Namibia Mheshimiwa Dkt. Hage Geingob wakati wa hafla ya kuzindua mtaa mpya wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere unaoitwa JULIUS K. NYERERE uliopo katika Jiji la Windhoek Nchini Namibia. Mei 27, 2019 

Picha namba 9  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwapongeza Watanzania wanaoishi Namibia mara baada ya kuzindua mtaa mpya wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere unaoitwa JULIUS K. NYERERE uliopo katika Jiji la Windhoek Nchini Namibia.Mei 27, 2019.PICHA NA IKULU

Share.

About Author

Leave A Reply