Sunday, August 18

MBUNGE VULLU NA DAU WATOA MSAADA WA VIFAA MAFIA

0


NA MWAMVUA MWINYI,  Mafia

MBUNGE wa viti maalum Mkoa wa Pwani ,Zaynabu Vullu, ametoa kitanda na vifaa tiba katika zahanati ya Kijiji cha Malimbani ,wilayani Mafia.

Aidha mbunge wa Jimbo la Mafia Mbaraka Dau nae amekabidhi mashine ya kusambazia maji, kata ya Kiegeani ili kuwarahishia wakazi hao kupata huduma hiyo kupitia kisima kilichochimbwa eneo hilo.

Vullu alikabidhi vifaa hivyo ,wakati alipokuwa kwenye ziara ya siku mbili wilayani Mafia, kwa lengo la kutimiza ahadi yake ya kukabidhi vifaa hivyo vinavyolenga kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wakazi hao, ambapo alipokelewa na mwenyeji wake Dau.

Alisema , anaunga mkono juhudi za serikali  kwa kununua kitanda, na vifaa tiba vitavyosaidia wagonjwa wataokwenda kupatiwa huduma kwenye zahanati hiyo.

“Niwapongeze kwa umoja, upendo na mshikamano ambao mnaendelea kuuonyesha katika kujiletea maendeleo, nami leo nimekuja kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuelekeza nguvu katika kuboresha sekta ya afya” alisema Zaynab.

Nae Dau alielezea kwamba ,amenunua mashine hiyo inayolenga kuboresha upatikanaji wa maji katika kisima kilichopo, ambacho kwa sasa ni cha mdundiko.

Alielezea, baada ya kufungwa mashine maji yatakuwa yanasambazwa umbali wa mita 1,000. Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwajupi Abdallah Sharifu aliwashukuru wabunge hao kwa namna walivyojitoa katika sekta hizo.

Share.

About Author

Leave A Reply