Wednesday, May 22

Mariam afanyiwa uchunguzi kubaini ugonjwa alionao

0


Daktari Bingwa Upasuaji (plastic
surgery), Dkt. Ibrahim Mkoma wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu huduma ya
matibabu ambayo Bi. Mariam Rajab Juma ameanza kupatiwa katika hospitali
hiyo.

Na John Stephen Massawe.

Wataalam
wabobezi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo wameanza kufanya
vipimo mbalimbali vya uchunguzi kwa Bi. Mariam Rajab Juma (25) mwenye kidonda
sehemu ya mgongoni ili kubaini chanzo cha ugonjwa alionao.

Akizungumza
na Wanahabari juu ya mwenendo wa matibabu ya Mariam, Daktari Bingwa wa
Upasuaji Dkt. Ibrahim Mkoma amesema vipimo hivyo ni pamoja na
kuchukuliwa sampuli ya nyama kutoka sehemu ya kidonda na kupelekwa
maabara kwa watalaam wa patholojia ili kubaini kama kuna saratani au la. 

Aidha Mariam ameandikiwa kufanya vipimo mbalimbali ikiwemo
CT-scan ya kifua na kichwa, Ultrasound pamoja na vipimo mbalimbali vya
damu.

Dkt. Mkoma amesema kidonda kilichopo sehemu ya mgongo wa
Mariam ni kidonda sugu na kwamba hadi sasa haijabainika kama mgonjwa
huyo ana tatizo la saratani au la mpaka hapo majibu ya wapatholojia
yatakapo patikana ndani ya siku nne kuanzia sasa. 

Mariam amesema
aliwahi kuugua moto akiwa na umri wa miaka mitano ambapo alitibiwa na
kupona ingawa alibaki na kovu kubwa kuanzia sehemu ya mgongo wake hadi
kwenye kisogo. 

Amesema mwezi wa nane mwaka jana alipata kipele
kwenye kovu na baadae kipele hicho kugeuka kuwa jipu. Alipotumbua jipu
lilitoa usaha na kisha kuanza kuota kidonda kilichoendelea kuongezeka
siku hadi siku.

“Nilienda kutibiwa katika Hospitali ya Makiungu
iliyopo Manispaa ya Singida, lakini pia kutokana na wazazi wangu kutokua
na uwezo wa kifedha niliacha kwenda hospitalini na kuanza kusafisha
kidonda mwenyewe, huku nikiwaomba marafiki zangu niliosoma nao sekondari
wanichangie fedha ili niweze kununua dawa,” amesema Mariam.

Amesema
wakati anatibiwa katika Hospitali ya Makiungu wataalam walimshauri kuja
Muhimbili ili kupatiwa matibabu zaidi, lakini kutokana na wazazi wake
kukosa fedha alimtafuta rafiki yake aitwaye Seif ambaye pia alisoma naye
sekondari akamrekodi kwa simu yake na kutuma kwenye mitandao ya kijamii
na huo ukawa mwanzo wa yeye kuanza kupata msaada.

Mariam
anaishukuru Serikali kupitia kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na Menejimenti ya Hospitali ya
Taifa Muhimbili kwa kuitikia wito wa kumsaidia na kuanza kumpa huduma.

Aidha,
anawashukuru Watanzania kwa jinsi walivyompigia simu na kutaka
kumsaidia baada ya kuona picha ya video kwenye mitandao ya kijamii.

Share.

About Author

Leave A Reply