Friday, August 23

MAKATIBU WAKUU TANZANIA NA UGANDA WAKUTANA KUJADILI CHANGAMOTO

0


Katibu Tawala Mkoa wa kagera Profesa Faustin Kamuzora akizungumza wakati wa mkutano wa mahusiano kujadili changamoto zinazozikabili nchi za Tanzania na Uganda unaofanyika Bukoba mkoani Kagera, wa pili kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Faraja Mnyepe, kushoto ni Balozi Paul Mkumbya kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda na kulia ni Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Paul Makelele.

Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa Mahusiano kujadili changamoto zinazozikabili nchi za Tanzania na Uganda unaofanyika Bukoba mkoani Kagera wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Faraja Mnyepe (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa siku mbili.

Sehemu ya washiriki wa mkutano wa mahusiano kujadili changamoto zinazozikabili nchi za Tanzania na Uganda unaofanyika Bukoba mkoani Kagera.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dorothy Mwanyika (kulia) akisisitiza jambo kwa wajumbe wa Tanzania wanaoshiriki mkutano wa mahusiano kujadili changamoto zinazoikabili nchi za Tanzania na Uganda unaofanyika Bukoba mkoani Kagera. Wa tatu kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo Elisante Ole Gabriel na anayemfuatia ni Katibu Mkuu Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Faraja Mnyepe.

Balozi wa Tanzania nchini Uganda Dkt Aziz Mlima (Kushoto) akimsikiliza Mpima Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Julius Msofe (wa pili kulia) wakati wa mkutano wa mahusiano kujadili changamoto zinazozikabili nchi za Tanzania na Uganda unaofanyika Bukoba mkoa wa Kagera. Kulia ni Mthamini Mkuu wa Serikali Evelyne Mugasha.

Balozi wa Tanzania nchini Uganda Dkt Aziz Mlima (wa tatu Kulia) akizungumza wakati wa kujadiliana na ujumbe wa Uganda katika mkutano wa mahusiano kujadili changamoto zinazozikabili nchi za Tanzania na Uganda unaofanyika Bukoba mkoani Kagera. Kulia ni Mthamni Mkuu wa Serikali Evelyne Mugasha. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI).

Na Munir Shemweta, WANMM BUKOBA

Makatibu Wakuu wa Tanzania na Uganda wanakutana mjini Bukoba mkoani Kagera katika mkutano wa mahusiano kujadili changamoto zinazozikabili nchi hizo ikiwemo Uimarishaji Mpaka wa Kimataifa pamoja na Matumizi endelevu ya rasilimali za Bonde la mto Kagera..

Mkutano huo wa siku mbili umeanza tarehe 29 April 2019 mjini Bukoba na kuwakutanisha Makatibu Wakuu wa nchi hizo mbili kutoka Wizara za Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Maji pamoja na Wizara ya Nishati.

Kabla ya mkutano huo, Wataalamu wa sekta shiriki kutoka Tanzania na Uganda walikutana na kujadiliana kuhusiana na changamoto zinazozikabili nchi hizo mbili kwa nia ya kuwasilisha mapendekezo yaliyofikiwa kwa Makatibu Wakuu wa nchi hizo.

Baadhi ya Changamoto zinazojadiliwa  kwenye mkutano huo, ni pamoja na Uimarishaji na Uthamini wa Mpaka wa Kimataifa wa Tanzania na Uganda, Mpango kabambe wa utunzaji mto Kagera na Matumizi endelevu ya rasilimali kati ya Tanzania na Uganda katika Bonde la Mto Kagera.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Faraja Mnyepe alisema mkutano huo ni mfululizo wa mikutano kati ya nchi hizo mbili wenye lengo la kutatua changamoto zinazozikabili nchi hizo kwa nia ya kuleta maendeleo.

Alisema, pamoja na kuwepo changamoto kadhaa lakini Tanzania na Uganda zinaendelea kufurahia mahusiano mazuri yaliyopo kwa kukutana na kujadiliana masuala mbalimbali yenye lengo la kuleta manufaa kwa nchi na watu wake.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Profesa Faustin Kamuzora aliuzungumzia mkutano huo kama njia ya kuzifanya nchi husika kufanya kazi pamoja na kuzidisha ushirikiano wenye nia ya kuleta maendeleo na kusisitiza kuwa, utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa unapaswa kufanywa kwa wakati.

Share.

About Author

Leave A Reply