Thursday, August 22

MAHAKAMA YAMTEUA KABIDHI WASII MKUU KUWA MSIMAMIZI WA MIRATHI YA MAREHEMU MTUI

0


MAHAKAMA ya Mwanzo ya Maji ya Chai wilayani Arumeru,mkoani Arusha imemteua Kabidhi Wasii Mkuu,kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu Anderson Mtui na kumpa muda wa miezi minne kutambua,kukusanya na kugawanya mali za marehemu kwa warithi stahiki.

Baada ya mgao huo atatakiwa  kupeleka taarifa ya mgawanyo na hesabu mahakamani hapo.Aidha Mahakama hiyo imemvua usimamizi wa mirathi,Aunieli Mtui baada ya kuandika jina marehemu(baba yake mzazi),Anderson Mtui,kama moja ya mashahidi wake waliofika mahakamani hapo wakati wa kufungua mirathi.

Katika shauri hilo la mirathi namba 39 la mwaka 2008,waombaji Royson Mtui na Rehema Mtui,ambao pia ni watoto wa marehemu waliiomba  Mahakama hiyo imtengue Aunieli  kuwa Msimamizi wa mirathi ya marehemu Anderson Mtui kwa madai kuwa msimamizi huyo siyo muaminifu kufanya kazi hiyo.

Akitoa hukumu hiyo juzi,Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo,Rweyemamu Kashero,alisema Mahakama hiyo imeamua kumteua Kabidhi Wasii Mkuu huyo baada ya Aunieli kuonesha taswira mbaya ya kushindwa kusimamia na kugawa kwa usawa mali za marehemu.

Alisema baada kwa kuzingatia wingi na thamani ya mali za marehemu,Mahakama hiyo inamteua Kabidhi Wasii Mkuu huyo kuwa msimamizi na kugawanya mali hizo ili mirathi hiyo ili iweze kufungwa.

Aidha baada ya Mahakama hiyo kumtengua msimamizi wa awali ya mirathi hiyo, ilimwagiza msimamizi huyo(Aunieli),kurudisha nyaraka zote alizopewa na Mahakama hiyo kuhusiana na mirathi hiyo ndani ya siku 14 kuanzia sasa.

“Kwa kuzingatia kwamba marehemu alikuwa amezaa watoto wake na wamama wanne tofauti na msuguano uliopo katika familia hii ambao unathibitishwa na shauri hili,ni vigumu kumpata msimamizi wa miirathi asiyekuwa na upande katika  familia hii,si tu kwamba haki itendeke bali ionekane kuwa imetendeka namteua Kabidhi Wasii Mkuu kuwa msimamizi wa mirathi hii,”alisema.

Alisema Mahakama imefikia uamuzi hul baada ya kusikiliza hoja za mashahidi  wa pande zote ambapo mahakama iliona msimamizi wa mirathi hakuwa sahihi kwani alitumia majina ya marehemu kama shahidi wakati wa kufungua mirathi.

“Kwa namna yoyote ile marehemu asingeweza kufufuka na kuja kutoa ushahidi katika mirathi yake mwenyewe,”alisema Hakimu huyo

Hakimu Kashero alitaja sababu za kumtengua msimamizi huyo ni pamoja na kwenda tofauti na mashahidi wake kuhusiana na baadhi ya mali za marehemu pamoja na msimamizi huyo  kufanya  kinyume na masharti ya usimamizi wake kwa makusudi ikiwemo kushindwa kuwa msimamizi na kumkasimisha mama yake ambaye ni mke mkubwa kuwa msimamizi wa mali hizo.

Hakimu huyo akirejea ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo,alisema mahakama imebaini msimamizi wa awali alichanganya mali ambazo hazikuwa za marehemu,ambapo mali hizo marehemu alizigawa kabla ya kifo chake.

Hakimu Kashore alisema suala la msimamizi kujiamulia mali zote ni za mama yake kwa kigezo kuwa ni mke wa marehemu hivyo mali hizo walizitafuta wote siyo sawa kwa sababu suala lililopo mbele ya mahakama hiyo ni la mirathi halipaswi kuchanganywa na suala la ndoa.

“Kwa kuzingatia kwamba marehemu alikuwa amezaa watoto 14 na wamama wanne tofauti,kwa kusingatia msuguano uliopo katika familia hii ambao unathibitishwa na shauri hili,ni vigumu kumpata msimamizi wa mirathi asiyekuwa na upande katika familia hii,”alisema na kuongeza

“Kwa kuzingatia wingi na thamani ya mali za marehemu mahakama hii inamteua Kabidhi Wasii Mkuu kuwa msimamizi wa mirathi kuanzia leo na kumpa muda wa miezi minne kutambua,kukusanya na kugawanya mali za marehemu kwa mujibu wa sheria kwa warithi stahiki na kuleta taarifa ya mgawanyona hesabu ili mirathi hii ifungwe,”

Awali waombaji hao waliiomba Mahakama imtengue kuwa msimamizi wa mirathi kwa madai kuwa hakutenda haki,hajawahi kuwaonyesha mali zao huku akigawa mali kwa kuwapendelea watoto wa familia ya mke mkubwa ambaye ana wa watoto saba na kuwabagua watoto wengine saba waliozaliwa na mama watatu tofauti.

Share.

About Author

Leave A Reply