Monday, August 26

HALMASHAURI YAVUNJA MKATABA WA UJENZI MRADI WA MAJI SAWALA

0


Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi imevunja mkataba wa ujenzi wa mradi mkubwa wa Maji maarufu kama mradi wa Maji Sawala katika Kata ya Mtwango wenye thamani ya shilingi Bilioni 1.8 uliyokuwa ukitekelezwa kwa pamoja na Kampuni za Siha Enterprise Co. LTD na Mavonda Co. LTD za Jijini Dar Es Salaam.

Halmashauri imelazimika kuvunja mkataba huo baada ya Mkandarasi kuonesha uwezo mdogo wa kutekeleza kazi hiyo, kwani tangu asaini Kandarasi ya ujenzi mnamo mwezi Januari 2018, katika hali ya kusikitisha ametekeleza jukumu hilo kwa asilimia 30 pekee licha ya kulipwa Fedha ya awali zaidi ya shilingi Milioni 270.

Aidha, Mkandarasi huyo anatakiwa kuilipa Halmashauri kiasi cha shilingi Milioni 413, ambapo kati ya hizo shilingi Milioni 254 ni faini wakati Milioni 159 ni bakaa ya Fedha ya utangulizi ambayo alilipwa baada ya kusaini mkataba.

Uongozi wa Halmashauri unaomba radhi kwa wananchi wa Kata ya Mtwango kwa kutopata huduma muhimu ya Maji kwa wakati, hata hivyo, uongozi unawahakikishia kuwa mradi utatekelezwa kama ilivyokusudiwa kwani taratibu za kumpata Mkandarasi mwenye uwezo na utashi wa kuujenga zimeanza.

Mnamo mwaka 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ilitiliana saini na Kampuni za Siha Enterprise Co. LTD pamoja na Mavonda Co. LTD kwa kandarasi ya miezi 12 ya kujenga na kuyafikisha Maji katika makazi ya watu kwenye Vijiji nne vya Sawala, Mtwango, Lufuna na Kibao kwa shabaha ya kuhudumia watu elfu 14.

Netho Ndilito

Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi

Share.

About Author

Leave A Reply