Sunday, April 21

CHUO KIKUU MZUMBE CHAANZISHA SAFARI YA MABADILIKO WEZESHI SEKTA YA AJIRA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI

0


 Akizungumza
katika uzinduzi wa warsha hiyo inayoendelea katika hoteli ya Morogoro,
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.Lughano Kusiluka amesema Chuo
Kikuu Mzumbe ni mahiri katika kufundisha masomo ya biashara na
menejimenti na sasa kinakwenda hatua ya mbele zaidi kwakuwaandaa
wahitimu wa ndani na hata nchi nyingine kutengeneza ajira kabla ya
kuhitimu masomo yao. 

Prof.Kusiluka
ameeleza kuwa kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa waajiri dhidi ya
wahitimu wa vyuo vikuu nchini na kuonekana kutokuwa na ujuzi wa kutosha
na umahiri katika fani walizosomea pindi wanapotaka kuajiriwa. Hivyo,
Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma na vyuo
vikuu viwili kutoka Uganda (Uganda Martys na Gulu), pamoja na asasi za
AFELT, LIWA, ASHOKA kutoka Kenya na INASP kutoka Uingereza, wameanza kwa
kuwajengea wahadhiri ili kubadili mbinu za ufundishaji
zitakazowawezesha wahitimu kuwa na maarifa, ubunifu na ujuzi zaidi
kutambua na kutumia fursa zilizopo ili kutengeneza ajira au kuajiriwa. 

Kwa
upande wake mwezeshaji wa warsha wa asasi ya umoja wa Vyuo vikuu
vinavyofundisha mbinu zinazohitajika katika kuboresha ufundishaji Afrika
Mashariki (AFELT) na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Daystar cha Kenya Prof.
Charles Kingsburry, amesema ni muhimu sasa kubadili mfumo wa
ufundishaji unaowafanya wahitimu kujua vitu kulingana na elimu
wanayofundishwa darasani pekee na kwa kutegemea mitandao ya intaneti na
badala yake mbinu mpya za ufundishaji ziwajenge katika ubunifu
,maarifa,mbinu na stadi halisia zitakazowawezesha kujiajiri wao na
kuweza kuajiri watu wengine. 

Hii
ina lengo si tu la kuwafanya wahitimu kujua vitu tofauti bali kuwajenga
kuwa watu tofauti wanaoleta mabadiliko chanya kwa jamii nzima na
kujinufaisha wao na jamii zinawazunguka kupitia elimu waliyopata. Naye
mwezeshaji mwingine toka Asasi ya AFELT na mhadhiri wa Chuo Kikuu,
Afrika Nazarene cha nchini Kenya Dkt. Kendi Muchungi amesema wahitimu wa
Vyuo Vikuu vyote vya Afrika Mashariki hawatofautiani na wamekuwa
wakikosa uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa na hivyo kushindwa kuisaidia
jamii katika suala la ajira kupitia elimu waliyopata,badala yake
wamekuwa wakitegemea kuajiriwa. 

Hivyo
ni imani yake kuwa mpango huo utaleta mabadiliko kwa wahadhiri wa vyuo
vikuu katika ufundishaji na kunufaisha jamii nzima ya Afrika Mashariki
kupitia wasomi wachache. Wakati huo huo mratibu wa Mradi wa ‘TESCEA’
kutoka Chuo Kikuu Mzumbe,Dkt.Albogast Musabila amesema pamoja na lengo
kuu la mpango wa mradi huo la kuwajengea wahitimu uwezo wa kujiajiri na
kuajiri,Chuo Kikuu Mzumbe kwa ushirikiano na wadau wa Sekta ya ajira,
wahadhiri na wanafunzi kimeanza mchakato wa kukusanya maoni ya wadau kwa
ajili ya kuandaa mapendekezo yatakayozingatiwa wakati wa kuboresha
mitaala na kuanzisha mitaala mipya. 

Share.

About Author

Leave A Reply