Wednesday, June 19

JE WANAFUNZI WA MAREKANI WANAO JIFUNZA KISWAHILI WANAITAZAMAJE AFRICA MASHARIKI?

0


Utafiti kuhusu mada za insha. (muhtasari tu)

Utafiti huu wa aina ya kiutendaji (action research) ulifanywa katika chuo kimoja nchini Marekani. Wanafunzi walipewa uhuru wa kuandika kuhusu mada yoyote, bora ihusiane na nchi za jumuiya ya Afrika mashariki. Matokeo ya utafiti yalionyesha kwamba 25% ya wanafunzi waliandika insha kuhusu ajali ya ndege ya shirika la Ethiopia ya hivi majuzi iliyoua watu zaidi ya 150 na iliyokuwa inatoka Ethiopia kuelekea Kenya, 16.67% waliandika kuhusu mji wa Nairobi, 8.3% za insha zilihusu nchi ya Kenya kwa jumla, 8.3% waliandika kuhusu mtaa wa Kibera, 8.3% waliandika kuhusu uongozi na haki za wanawake nchini Kenya, 8.3% zilihusu kashfa ya kitapeli ya hivi majuzi kwenye benki ya Barclays nchini Kenya, 8.3% zilihusu filamu za Kiswahili, 8.3% zilihusu ajali ya feri ya Tanzania iliyotokea katika ziwa Victoria, 8.3% zilikuwa insha kuhusu nchi ya Eritrea.

Ufafanuzi

Wanafunzi wengi waliandika kuhusu mada zinazohusiana na nchi ya Kenya. Inawezekana kwamba nchi anamotoka mwalimu wa lugha au mada anazotilia mkazo kwenye silabasi  au mtaala ziathiri mada wanazoandika wanafunzi. Pili ni kwamba tukio la hivi majuzi la ajali ya ndege ya shirika la Ethiopia lilivutia sana wanafunzi. Inawezekana kwamba wanafunzi walijinasibisha na ajali hii kwa sababu ndege iliyohusika ilitengenezewa nchini mwao hapa Marekani na kwamba waathiriwa walio wengi (wakenya) ni wasemaji wa Kiswahili wanachojifunza darasani. Asilimia kubwa ya insha vilevile ilihusu habari hasi kiasi – utapeli, ajali za ndege na feri, mtaa wa Kibera, wanawake kutokuwepo uongozini na kunyimwa haki zao pia. Kwa kweli kunayo mengi mazuri ambayo yanaendelea katika nchi za Afrika ya mashariki ila wanafunzi wengi hawakuandika kuhusu mambo hayo. Hali hii ni ya kuwafumbua macho walimu wa lugha ya Kiswahili ugenini kwamba wanafunzi wa lugha nchini Marekani wanapenda hasa kutambulishwa kwa mada zinazohusiana na changamoto zilizopo katika nchi za Afrika mashariki. Inashangaza kuona kwamba ijapokuwa nchi ya Eritrea haihesabiwi kama mojawepo ya nchi za jumuiya ya Afrika ya Mashariki, kunao wanafunzi walioandika kuhusu nchi hii. Hali hii inahitaji kuchunguzwa zaidi kwa sababu huenda imani walizo nazo wanafunzi kuhusu kinachoitwa Afrika mashariki kikawa tofauti na kile kinachojulikana na wengi. Si ajabu wanafunzi kama hawa waandike insha kuhusu Ethiopia na Somalia kama mojawepo ya nchi za Afrika ya mashariki. Mwisho ni kuhusu wanafunzi walioandika kuhusu filamu. Kutokana na deta za kibiografia kuhusu wanafunzi hawa, ilidhihirika kwamba wanafunzi hawa ni wa shahada ya pili au ya tatu na utafiti wao unahusu filamu. Hali hii inadhihirisha kwamba wanafunzi wa uzamili au uzamifu ambao wapo katika madarasa ya Kiswahili huwa na haja ya kujifunza lugha ili wafanikishe utafiti wao. Insha zao zilihusiana na utafiti wanaofanya kwa ajili ya kuandika tasnifu zao.

Share.

About Author

Leave A Reply