Sunday, August 25

WAZIRI MKUU SRI LANKA ASEMA VYOMBO VYA UPELELEZI NCHINI MWAKE NI DHAIFU

0


Colombo, SRI LANKA.

Waziri Mkuu wa Sri Lanka, Ranil Wickremesinghe, amekiri kwamba vyombo vya intelijensia vya nchi yake ni dhaifu, kutokana na miripuko ya kigaidi ya hivi karibuni katika mji mkuu wa nchi hiyo Colombo.

Wickremesinghe ameyasema hayo leo Aprili 24, 2019 wakati akizungumzia miripuko ya hivi karibuni ya kigaidi mjini Colombo na kuongeza kwamba licha ya kwamba awali serikali ya India ilikuwa imeipatia Sri Lanka taarifa za kiitelijensia kuhusiana na hatari ya kujiri hujuma hizo, lakini maafisa wa upelelezi wa nchi hiyo walishindwa kuzifanyia kazi kwa wakati.

Waziri Mkuu huyo wa Sri Lanka ameongeza kwamba, kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana hadi sasa, wahusika wa mashambulizi hayo ni kundi moja la raia wa nchi hiyo wenye mahusiano na pande za kigeni.

Jumapili iliyopita tarehe 21 Aprili kulijiri miripuko kadhaa ya kigaidi katika makanisa na hoteli kadhaa mjini Colombo ambapo kwa idadi ni watu 359 ambao waliuawa na wengine zaidi ya 500 kujeruhiwa.

Hapo jana pia kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) lilitangaza kuhusika na matukio ya milipuko hiyo.

Aidha, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Sri Lanka, Ruwan Wijewardene, amesema kuwa, watu wawili miongoni mwa waliohusika na miripuko ya mabomu mjini Colombo walikuwa ni wanafunzi wawili waliosomea Uingereza na Australia.

Waziri Wijewardene amesema kuwa watu 08 kati ya waliohusika na milipuko hiyo tayari wametambuliwa, ambapo wawili kati yao ni wanafunzi wawili waliosomea nchi zilizotajwa.

Mbali na hivyo, ameongezea kuwa hadi sasa idadi ya watu waliotiwa mbaroni kwa kuhusishwa na mashambulizi hayo imefikia 58.


Share.

About Author

Leave A Reply