Wednesday, August 21

TAASISI YA TULIA TRUST YAUNGA MKONO UJENZI WA ZAHANATI KIJIJI CHA ISYONJE.

0


Na Prakseda Mbulu,MBEYA.

Jumla ya bati hamsini(50) zimetolewa na taasisi ya Tulia Trust katika kijiji cha Isyonje kata ya Isongole wilayani Rungwe,ili zisaidie katika kuezeka jengo la zahanati kijijini hapo.

Akikabidhi bati hizo,meneja wa taasisi ya Tulia Trust,Bi Jackline Boazi,amesema wameguswa na kuona hatua zilizochukuliwa na wananchi pamoja na viongozi katika kijiji hicho ya kuanza ujenzi wa zahanati ili waondokane na adha wanayoipata ya kufuata huduma za afya umbali mrefu.

Amesema hicho walichokitoa ni kidogo lakini ana imani kitasaidia na kufanyiwa kazi na endapo kutakuwa na uhitaji wa bati nyingine waone namna ya kumalizia kwa kushirikiana na wadau wengine watakaojotokeza kusaidia ujenzi huo,kwani wananchi wanaoonesha juhudi ndio wanaoungwa mkono.

Akipokea msaada huo,diwani wa kata ya Isongole,Laurence Mfwango,ameishukuru taasisi ya Tulia Trust kwa kuguswa na kuwasaidia katika mradi huo na kuongeza kuwa suala la kutopatikana kwa huduma za afya katika kijiji hicho litakuwa historia.

Nao baadhi ya wananchi waliojitokeza kupokea msaada huo,wamesema alichokifanya Dkt.Tulia na mfano wa kuigwa na wana imani zahanati itakamilika kwa wakati ili waepuke na adha ya kufuata matibabu
katika hospitali ya Igawilo jijini Mbeya pamoja na vifo vya akina mama wajazito na watoto.

“Tunamshukuru sana Dkt.Tulia,kwa kuona changamoto yetu,tumekosa huduma za afya kwa kipindi kirefu,akina mama na watoto wamekuwa wakipata tabu kutokana na kukosa huduma hiyo mpaka kupelekea vifo,tunamuomba atusaidie mpaka ukamilishwaji wa zahanati hiyo”wamesema wananchi hao.

Wameongeza kuwa kukamilika kwa mradio huo kutawasukuma,wafanye shughuli za maendeleo kwa amani kwani wamekuwa wakitumia muda mwingi kufuata matibabu nje ya kijiji chao.

Mradi wa ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho ulianza tangu Agost 2017,kwa nguvu za wananchi wakishirikiana na viongozi wao,ambapo mpaka hatua ya kupaua jengo hilo limegharimu zaidi ya shilingi milioni 11.

Share.

About Author

Leave A Reply