Wednesday, August 21

NAIBU WAZIRI NISHATI AAGIZA TANESCO NA REA KUTATUA SINTOFAHAMU YA NGUZO MKOANI MOROGORO

0


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ametoa wiki moja kwa wasimamizi wa mradi wa usambazaji umeme vijijini mkoani Morogoro kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), na TANESCO kuhakikisha kuwa wanatatua changamoto ya nguzo mkoani Morogoro.

Naibu Waziri ameyasema hayo akiwa katika Kijiji cha Dibamba wilayani Mvomero ambapo alifika kukagua kazi ya usambazaji umeme na kuwasha rasmi umeme katika Kijiji husika.

Mhe. Subira ametoa agizo hilo baada ya sampuli ya nguzo za mkandarasi wa umeme mkoani Morogoro kupimwa na TANESCO na kuonekana kuwa hazina vigezo huku Mkandarasi huyo akidai kuwa sehemu ya nguzo zake zinafaa kwa matumizi ya umeme.

” Hatutaki kuona mivutano kati ya wakandarasi na wasimamizi wa miradi ya umeme vijijini kwani inachelewesha upelekaji umeme kwa wananchi hivyo nawaagiza mtatue suala hili kwa kupima nguzo zote na Wizara ipate taarifa ndani ya Wiki Moja,” amesema Mgalu

Kuhusu kasi ya usambazaji umeme ya mkandarasi State Grid, Naibu Waziri ameeleza kutoridhishwa na kasi ndogo ya mkandarasi na kusema kuwa Serikali itamchukulia hatua asipotekeleza kazi kwa mujibu wa mkataba.

Aidha amewaagiza Wasimamizi wa miradi ya usambazaji umeme vijijini kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO na REA kuwasimamia wakandarasi kikamilifu kwani nao watachukuliwa hatua kutakapokuwa na uzembe wa kazi.

Akiwa katika Kijiji cha Dibamba, Naibu Waziri amemuagiza mkandarasi kutoondoka katika Kijiji hicho kwa kuwa kati ya kaya 98 za awali zilizopaswa kuunganishiwa umeme, ni kaya 14 tu ndio zimeunganishwa umeme.


Share.

About Author

Leave A Reply