Saturday, August 17

MVUA ILIYOKUWA IMEKWAMA NCHINI, GHAFLA YAWASILI KENYA

0


Nairobi, KENYA.

Katika hali isiyotegemewa huko nchini Kenya, hatimaye mbingu zimefunguka na jiji la Nairobi kwa mara ya kwanza limepata hali ya unyevu tangu kuanza kwa mwaka 2019.

Mvua hiyo iliodaiwa kukwama eneo la anga hapa nchini imenyesha kwa ghafla na kuwapata wakazi wengi wakiwa hawajajiandaa, ambapo wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama machinga waliokuwa wakiuza mali zao katika barabara za jiji la Nairobi wameathiriwa na mvua hiyo.

Mbali na hivyo, waendesha magari na raia pia waliokutwa na mvua hiyo, wengi wameonekana kutokujali na kutembea katika mvua bila kujali kwamba walikuwa wakinyeshewa.

Masaa mawili kabla ya mvua hiyo kunyesha, idara ya hali ya hewa nchini humo ilikuwa imetangaza kuwa mvua itanyesha jijini Nairobi, viungani mwake na maeneo mengine.

Wiki iliopita idara ya hali ya hewa nchini humo kupitia Naibu Mkurugenzi wake Bernad Chanzu ilisema kuwa hakutakuwa na mvua katika msimu huu wa mwaka huu.

Aidha, Bwana Chanzu pia aliwatahadharisha Wakenya kujiandaa kwa uhaba mkubwa wa maji ya kunywa, usafi na matumizi ya viwandani mbali na kuleta umeme.

Wiki mbili zilizopita idara hiyo ilikuwa imetangaza kuwa kiangazi kitaendelea mwisho wa mwezi huu huku mawingu ya mvua yakisalia nchini Tanzania kutokana na kiwango cha chini cha upepo wa kusukuma mawingu hayo kuelekea kaskazini.

Kaimu mkurugenzi wa shirika la hali ya anga nchini Kenya, Ni Stella Aura, alieleza kuwa mvua ndefu zilichelewa lakini inatarajiwa kuanza kunyesha mwisho wa mwezi huu.Hatahivyo amesema kuwa mvua ndefu imeanza lakini kwa kiwango kidogo katika maeneo mbalimbali.

Mwezi Aprili ndio mwezi wa mvua ndefu nchini Kenya na onyo limetolewa katika maeneo kadhaa ya Kenya kuhusu kuchelewa kwake. Mvua ndefu hunyesha miezi ya Machi, Aprili, na Mei hususan katika eneo la magharibi, bonde la Ufa na mkoa wa kati na ni muhimu sana katika sekta ya kilimo hatua inayosababisha kuwepo kwa chakula cha kutosha.

Idara hiyo imewashauri wakulima kupanda mimea inayokuwa kwa haraka na ile isiotegemea maji kwa kuwa mvua hiyo huenda isinyeshe kwa muda mrefu.

Share.

About Author

Leave A Reply