Tuesday, August 20

MBUNGE MAVUNDE ATATUA CHANGAMOTO YA KIVUKO KATA YA MIYUJI JIJINI DODOMA.

0


Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh Anthony Mavunde leo ametembelea eneo la Mathias Kata ya Miyuji Jijini Dodoma kujionea adha na changamoto ya kivuko wanayopata wananchi wa eneo hilo kutokana na uwepo wa korongo kubwa ambalo hupitisha maji mengi kipindi cha mvua na hivyo kukatisha mawasiliano kati ya eneo hilo na maeneo mengine.

Akiongea kwa niaba ya wananchi wa eneo hilo,Diwani wa Kata ya Miyuji Mh David Mgongo ameeleza changamoto hiyo kubwa kiasi cha kupelekea wanafunzi kushindwa kwenda Shule kipindi cha Mvua na wananchi kukosa huduma muhimu kutokana na adha hiyo.

Mbunge Mavunde amewahakikishia wananchi hao kujengwa kwa kivuko hicho ndani ya muda mfupi kama ambavyo aliahidi wakati wa Kampeni na kwamba mkandarasi amepatikana na fedha kiasi cha Tsh 199,000,000 zitatumika kwa ajili ya ujenzi huo chini ya TARURA na shughuli rasmi za Ujenzi zitaanza wiki ya Tarehe 3.06.2019 ,pia Mbunge Mavunde ameahidi kujenga kivuko kidogo cha watembea kwa miguu ambacho kitajegwa mita 70 kutoka kivuko kikubwa kinapojengwa.

Wananchi wa eneo hilo wamemshukuru sana Mbunge Mavunde kwa namna ambavyo amekuwa mstari wa mbele kushughulikia matatizo yao na kuahidi kujitolea nguvukazi wakati wa zoezi lote la ujenzi ili na wao kuunga mkono juhudi za Mbunge huyo.


Share.

About Author

Leave A Reply