Friday, August 23

Safari yangu ndani ya Habarileo kama mhariri msanifu

0
Nilijiunga na  gazeti hili wiki kadhaa kabla ya kuanza uchapishaji wake. Nilipokewa kwa namna ya ajabu na mchanyato wa waandishi waliokuwa wameajiriwa kuanza libeneke hili la serikali.
Mchanyato huu waandishi  mikiri kuwa niliona kuwa bora katika muda huo, na hata nilipokutana na moto wa Gwiji la habari, niliafiki kwa kuwa lilikuwa kundi la vijana wanaojiamini sana
Walipelekwa katika semina ya kuwaweka sawa ili wajue wajibu wao, walifika chumba cha habari baadaya semina hiyo wakiwa wameiva barabara kwa namna inavyofaa, na kwa namna walivyoona inafaa.
Wakati naingia nilikuwa natokea Jumba kubwa la magazeti  kitaani, yaani the Guardian Limited. Na hata Guardian Limited haikuwa mahali pangu pa kwanza kama msanifu, la hasha nilitokea televisheni ya CTN  baadaya kumaliza mkataba wangu wa mwaka mmoja.
Awali nilikuwa Media Holdings wachapishaji wa Mwananchi na The Express ambako niliajiriwa kama Naibu Mhariri Msanifu Mkuu wa Media Holdings kabla sijawa Mhariri wa Mwananchi, nikichukua nafasi ya mzee  Barnabas Maro.
Nikiwa mwananchi, CTN na  Nipashe  nilijifunza mengi sana kuhusu uendeshaji wa vyombo vya habari binafsi, kwani historuia yangu ilianzia katika vyombo vya serikali na baadaye ya chama tawala.
Nikiwa na uzoefu wa kutosha wa magazeti binafsi nilijikuta naingia katika chombo cha serikali chenye mchanganyiko mkubwa wa falsafa ya vyombo binafsi, ambayo mimi nilikuwa nimeibatiza jina la kanyaga twende ili mradi una ushahidi.
Kila mwajiri ana vitu vyake anavyotaka na hili ndilo muhimu sana kwa mhariri msanifu kujua kwani lile ambalo unaambiwa mara kwa mara katika mafunzo ya kujua dunia ipasavyo na hasa sheria za vyombo vya habari ni kitu kinachoeleweka  lakini hiki cha pili ni busara inayokuongoza.
Nakumbuka wakati tunaanza, vijana walilalamika kwamba kuna wazee wamewekwa pale  kurudisha nyuma  libeneke na wao wanataka kutoka kushindana na magazeti mengine kuonesha kwamba wao si mchezo hata kidogo na hasa ukizingatia kwamba wao ndio walikuwa mastaa walikotoka.
Naam, kwa mimi ambaye nilikuwa nimeshakaa katika vyombo vya serikali na vya  chama (nilikuwa Radio Tanzania na  Uhuru na Mzalendo) kwa takaribani miaka nane nilijua watajifunza kwamba utumishi wa umma katika staili wanayokwenda nayo ina ukakasi.
Na ndio maana  nilipompelekea toleo la kwanza baba yangu (naye ilitokea ni mtu wa habari) aliponiuliza kama tutaweza kuendelea na ubora wa gazeti  anaouona pale nilimjibu sijui kwa kuwa ni gazeti la kila siku na hili limeandaliwa kwa muda mrefu ili tutoke na Kishindo!
Alifurahishwa sana  na uchaguzi wa stori lakini alivutiwa sana na makala zilizokuwa zimeshiba kisawasawa.
Hata mimi niliona kuwa nguvu ya gazeti ni katika siku za usoni ni makala na habari za vijijini kama zityafanyiwa kazi kwa kuwa ushindani wa kawaida wa kisiasa na udaku ni kinyume na utamaduni wa chombo cha serikali.
Hii inatokana na ukweli kuwa nguvu ya maandishi katika gazeti hili ni kubwa hasa kutokana na kuwa gazeti la rejea.
Kazi ya usanifu
Nina kawaida ya kuwaambia watu wengi wanaoandika usimpe nafasi mhariri msanifu kuharibu stori yako na kuondoa fleva ambayo unataka iwepo.
Katika kazi hii ya uandishi wa habari ambapo robo tatu ya miaka yangu(nilianza rasmi kazi hii 1985) nimeifanya kama Mhariri msanifu kuna mambo ya msingi ambayo natakiwa kuyazingatia hivyo nikiona dalili ya kutaka kupelekwa chaka, nitajitahidi  kuvaa kiatu chako na hii kama nisipokuwa mwangalifu nitaondoa fleva yako na ikifikia hapa natakiwa kitaratibu kuondoa jina katika stori yako na kuiweka kama mchangiaji chini.
Kiukweli moja ya raha ya kuw amhariri msanifu ni kule kujikuta umekwama kuendelea na kusanifu maandishi kutokana na sentensi zisizoeleweka au kutupiwa maneneo yasiyoeleweka au yalipangwa kama matofali  yenye uzito tofauti.
Lipo tatizo la wazi kabisa la watu kupanga maneno tu lakini habari yenyewe (facts) ikatupiwa mgongo au kupakwa mafuta tu ya kuteleza , ikiwa haijashiba kisha unatandikwa na maneno magumu kutoka kwa mwandishi anayetaka kuonesha kwamba anajua anachoandika kumbe chenyewe kilistahili kuwa paragrafu mbili tu kujazia mapengo ya gazeti.
Nilipokumbana na  hayo kitu change cha kwanza nilichokuwa nafikiri wakati nasoma  maandiko ni kutoa misamiati isiyoeleweka, kisha setensi zisizoeleweka halafu huna stori , unarejea tena kujaribu kuitengeneza.
Tulianza na mjengo wa ukurasa hivyo maneno yakipungua inabidi urejee tena au uitupe stori utafute nyingine, mjengo ulilazimisha vitu vingi sana vibadilike.
Mnakubaliana na mhariri wa habari kwamba mtatumia mjengo namba Fulani lakini unakuja kuletewa maandiko ambayo  yana maneno yamejaa tu yasyokuwa na maana unatengeneza maandiko yawe na maana unajikuta umeondoka katika mjengo. Uzoefu wangu  ulinifanya baadae niseme mjengo utumike kutoondoka katika ramani lakini usiwe msaafu.
Lakini kazi ya kusanifu maandiko ya Habarileo mpaka leo ni ngumu si kwa sabau ya sentensi tu bali kukosekana kwa muongozo wa nini ndio nini katika uandishi wa Kiswahili kilichobora katika gazeti la serikali. Muongozo unaotumika ni ule wa gazeti la Kiingereza, ambao kwa vyovyote vile hauna mahusiano mazri na lugha ya Kiswahili ambayo wasemaji wake ni wa Manzese na  Mgeta
Ni dhahiri kwamba unapohariri maandiko, msanifu anakuwa na  nafasi kubwa ya kuona kwamba facts (takwimu) ni kitu ambacho si cha kuchezea lakini maoni unaweza kuyafanya inavyotakiwa.
Katika kipindi cha mwanzo chini ya uangalizi mkali wa Cassian Malima, hali ilikuwa shwari akitoa nafasi ya kuboireshwa kwa gazeti kwa namna inavyofaa kwa jinsi siku zinavyozidi kusonga, huku akitoa maelekezo kwa mujibu wa uzoefu wake.
Lakini leo hii tunapozungumza kuhusu usanifu katika gazeti hili, tunazungumzia zaidi Kiswahili  katika mashindano ya kuuza gazeti.
Katika medani ya siasa ndio kuna matatizo zaidi huku maandiko ya jamii ya kawaida yakionekana kama ni daraja la chini kuliko gazeti. Huenda hili linatokana na mabadiliko makubwa ya aina ya uandishi na kitambo kirefu kukaa bila kupata  retreat kama ile ya bagamoyo.
Wapo waandishi wageni wengi ambao hawajui nini maana ya kufanyiakazi gazeti la serikali na kwanini stori zinatakiwa kuwa na vyanzo vingi vya habari na lazima kuwe na seal yaani habari yenye uthibityisho wa ukweli usiokanushika.
Wahariri wasanifu kimsingi ni watu wa mwisho wanaohakikisha usahihi wa habari na utamu wa habari kabla haujamfikia mlaji. Wapo watu wanaosema wahariri wasanifu  hawana  sababu ya kuwapo.
Wanaona kwamba kazi ya mhariri msanifu ni kuharibu kopi aliyoandika kuifanya ama ipooze au iwe na msisimko usiotakiwa au kuadika kichwa cha habari ambacho si cha kweli.
Mimi naamini kwamba katika mfumo wa ulinzi wa kazi zinazoandikwa kwa kasi mhariri msanifu ndio geti kuu la mwisho  na kama yeye  akiwa makini anaweza kuokoa gazeti lisionekane ni kichwa cha mwendawazimu na kiwa mwangalifu gazeti litapata sifa sana kwa kufanyakazi yake kitaaluma.
Kimsingi hakuna mwandishi anayempenda msanifu anayefanyakazi yake kitaaluma kwani mara zote humfanya mwandishi asimamie vidole ili kazi iwe na maana iliyokusudiwa.
Katika gazeti la HabariLeo usanifu ni kazi ngumu kutokana na uasili wa kazi na pia kutokana na aina ya uandishi uliopo kwa sasa katika jamii na pia katika vyombo vya habari; huku vyombo vya habari vya kijamii vikiharibu kabisa mueonkano wa dhamira njema ya uandishi wa habari, uzushi na udaku
Ninaamini  kuna mabadiliko makubwa katika uandishi na utoaji wa habari kwa HabariLeo. Tunapozungumza miaka kumi tunazungumza mtoto aliye darasa la tatu akiwa ameanza shule akiwa na  umri wa miaka mitatu akaenda msingi akiwa na miaka 7  na mtoto huyu sasa hivi anajua nini anachotakiwa kwenda sekondari na pia chuo kikuu.
Nimefanyakazi na wahariri watatu mpaka sasa huku nikiwa chini ya wasanifu kurasa wakuu wawili, tofauti za filosofia ya  usahihi na spidi zinapishana sana.
Katika chumba cha habari cha HabariLeo , sasa hivi ugomvi sio wazee wananyima njia ya kufanyakazi , wameshabaini namna bora ya kuwa mtumishi wa umma,bali ni vichwa vya habari wanavyoona vinakera sokoni.
Ukitaka kutengeneza wahariri wasanifu wa baadae, unatoa nafasi ya uhuru wa watu kufikiria nini wanadhani kinauza, kisha unapeleka, hawa walio wadogo wanafikiri ni rahisi sana kutengeneza kichwa cha habari cha kuvutia katika mazingira ya spidi ya sasa, lakini wanapotoa hoja ujkawasikiliza kesho wanakuja na kitu kizuri zaidi.
Lakini nimejifunza kitu katika safari yangu, kazi hii haihitaji unafiki, inahitaji ushirikiano na ukweli na kila dhama ina dhama zake lakini la maana ni kutambua filosofi  nyuma ya kila habari unayohariri na kuna mufda maamuzi  yetu hayawezi kabisa kufanana na mahitaji ya soko bali mahitaji ya taaluma.
Na hii inanyima nafasi ya kuwa na simulizi na vichwa vya kusisimua kwa kuwa wanazuoni hubishana katika hilo wakati walaji hudharau hilo na kuvutiwa na kile kilichowatandika haraka usoni.
Wasanifu kazi kubwa ni kusahihisha na kuna wakati  unapiga mzinga kutokana na mwandishi kushindwa kwenda moja kwa moja au wakati wmingine unapiga mzinga kwa triki na unawakasirisha wakubwa.
Hakuna anayependa kufanya uhariri wa aina hii, na waandishi vijana wasingelipenda kuwa na mhariri wa aina hii lakini katika maisha yangu ya uandishi nimegundua unahitaji watu wa kufanya marekebisho na kuzuia ujinga kuwafikia walaji wa habari ambao pamoja na kutaka kuburudishwa wanahitaji kuelimishwa.
Wanahitaji habari ambayo imeandikwa vyema imenyooshwa na haina kigugumizi na wanaoweza kufanya hivyo kwa spidi ni wachache na ndio maana uhariri usanifu ni kazi ya mwalimu zaidi kuliko kuandika habari.kwani ni yeye ambaye anaangalia kazi  kabla ya kuchapishwa ni yeye anayenyoosha setensi na kuipa guvu inayotakiwa habari andikwa na kama ilivyokazi nyingine za uandishi wa habari mhariri msanifu anatakiwa kuwa makini na kasi katika kutekeleza kazi zake na has kuhakikishakwamba muda unazingatiwa.
Katika hili naweza kusema nimefanikiwakatika safari hii ambayo huenda bado muda kidogo tutapumzika.
Kila la Heri habariLeo
Description: https://ssl.gstatic.com/ui/v1/icons/mail/images/cleardot.gifRead More

Share.

About Author

Comments are closed.