Sunday, August 25

AFRAA, ATCL kukutanisha wadau wa anga Z’bar

0
 Mkutano wa siku mbili wa wadau wa sekta ya anga barani Afrika ulioandaliwa na Umoja Wa Mashirika ya Ndege barani Afrika (AFRAA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Ndege nchini (ATCl) unatarajiwa kufanyika visiwani Zanzibar mwezi ujao.
Kwa mujibu wa tovuti ya AFRAA, mkutano huo utafanyika kwenye hoteli ya Zanzibar Beach kuanzia Aprili 8 – 10, mwaka huu ambapo zaidi ya wajumbe 300 wanatarajiwa kuhudhuria.
Baadhi ya wadau wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo ni pamoja na mashirika ya ndege, watengenezaji wa ndege, watoaji wa mafunzo katika vyombo vya usafiri wa anga, watengenezaji wa injini za ndege, washauri na wanataaluma ya usafiri wa anga na wasambazaji wa vifaa vya hali ya hewa.
Wengine watakaohudhuria mkutano huo ni taasisi za fedha, kampuni zinazotoa huduma ya mizigo na vyakula na watoaji wa huduma za mawasiliano.
Kulingana na tovuti hiyo mkutano utaenda sanjari na maonyesho ya bidhaa na huduma mbalimbali zinazotolewa na wadau wa sekta ya usafiri wa anga barani Afrika.
Mkutano huo unatarajiwa kujadili mambo mbalimbali yanayohusu sekta hiyo.
“Mkutano huu ni sehemu ya juhudi za kuwaweka pamoja waendeshaji na watoa huduma katika sekta ya usafiri wa anga barani Afrika kwa lengo la kuchochea mjadala katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuongeza mazingira ya ushindani,” imeeleza tovuti hiyo.
Mkutano huo pia utajadili namna ya kujenga mifumo endelevu katika mnyororo wa usambazaji na kuweka mazingira ya ushindani wa biashara ya usafiri wa anga.
Mada mbalimbali zinatarajiwa kuwasilishwa na kujadiliwa katika mkutano huo wa siku mbili baadhi yake ni maendeleo endelevu ya mikundombinu ya usafiri wa anga barani Afrika, matumizi ya takwimu katika kufanya mageuzi ya biashara ya usafiri wa anga Afrika na ongezeko la mahitaji ya usafiri wa anga na gharama zake.
Source: Said MmangaRead More

Share.

About Author

Comments are closed.