Sunday, August 25

Viwanda HEWA Vya Sukari Vyamkera Rais Magufuli

0


Rais John Magufuli amesema matokeo ya uchunguzi uliofanywa na kamati yake teule yamebaini kuwapo viwanda hewa vilivyokuwa vinaagiza sukari ya viwandani.


Amesema Machi 15, mwaka huu amepokea ripoti hiyo yenye idadi ya viwanda 30 huku viwanda vinane tu ndiyo vikibainika kuwa na taarifa za kweli katika uagizaji wa sukari.

Kampuni hizo nane ni ASB, Nyanza Bottlers, Bonite Bottlers Ltd, Bakhresa Group of Companies, Kazman Group, Lakailo Company, ANB Group na Kampuni ya Super ASB.

Rais Magufuli alibainisha hayo jana wakati wa Mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, yeye akiwa mwenyekiti wake.

“Niliunda kamati maalum ya kufuatilia suala la uagizaji wa sukari kutoka nje, nimepokea ripoti Machi 15, mwaka huu (Alhamisi),” alisema Rais Magufuli. “Kilichobainika humo kinasikitisha sana, kampuni zaidi ya 22 zilikuwa zinaagiza sukari kwa manufaa yao.”

Rais Magufuli alisema kamati hiyo imebaini kuwa kampuni hizo 22 zilikuwa zinaagiza sukari kuliko mahitaji yao halisi waliyokuwa wanayahitaji.

Rais Magufuli alitolea mfano wa kampuni ya Iringa Food Products iliyokuwa imeagiza tani 300 wakati mahitaji yake ni tani 190.

Alisema kuna kampuni ya Dabaga ilikuwa inaagiza  tani 2,000 wakati mahitaji halisi ni tani 1,600. Alisema kuna viwanda vimekuwa vikiagiza sukari ya viwandani lakini huibadilisha kuwa ya matumizi ya binadamu badaye.

Sukari ya viwandani kutoka nje ya nchi ina unafuu mkubwa wa kodi ya forodha kulinganisha na ile ya kawaida.

Mwenyekiti huyo wa TBNC alitoa takwimu hizo ikiwa ni malalamiko yake kwa sekta binafsi ambayo awali ilikuwa imeorodhesha kero mbalimbali za upande wa serikali zilizopo katika biashara na uwekezaji nchini.

Rais Magufuli alisema kuna baadhi ya viwanda bado havijajengwa lakini wamiliki wake wamekuwa wakiagiza hadi tani 500 na kueleza kuwa wahusika wote waliobainika wataandikiwa barua.

“Kuna kiwanda kinaitwa Maisha Bottlers kiliagiza tani za sukari 7,000 kikieleza kiko Mbeya,” alisema mwenyekiti huyo, “lakini kamati (ya uchunguzi) imeenda Mbeya, imekitafuta, haijakiona.”Hii ripoti nitamkabidhi Waziri Mkuu aipitie na achukue hatua.”

Alisema suala la sukari limekuwa likiwaweka watu wengi matatani wakiwamo mawaziri wa tangu utawala wa Rais wa tatu, Benjamini Mkapa (1995-2005).

Alisema mahitaji ya sukari nchini ni tani 590 kwa mwaka, ambapo tani 455 ni kwa matumizi ya nyumbani na tani 135 kwa matumizi ya viwandani.

Aliongeza kuwa kwa sasa kuna upungufu wa tani 130 kwa sukari ya kula na tani 135 kwa matumizi ya viwandani.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.