Saturday, August 17

VAR inatuachia maswali mengi kuliko majibu

0


Shirikisho la mpira wa miguu duniani FIFA limeanza kuleta mifumo ya kuwa na mareferee mpaka watano na teknolojia maarufu(Video Assistant Referee) VAR. 

Sawa ni jambo jema kutambulisha teknolojia mpya ili kupunguza makosa mchezoni lakini inaonekana ni kama vile yenyewe ndio inazidisha huo utata badala ya kuupunguza. Ni wazi waamuzi wamekuwa wanakosea sana na tukumbuke kuwa Soka ni mchezo wa haki na ni wazi kuwa FIFA wanajaribu kuufanya mchezo huu kuwa fair zaidi lakini kwa njia ipi? 

Ujio wa VAR kwa kiasi kikubwa umewagawanya sana mashabiki wa soka ulimwenguni na hapa ndipo utata wenyewe unapoanza. Kama ni haki mbona bado ni kama vile hata yule aliepewa kama kapendelewa na yule alieadhibiwa anakuwa kama kaonewa wakati mwengine kama sio kwenye kesi nyingi uwanjani? 

Mfano mzuri kabisa ni mechi ya karibuni kabisa ya Manchester United kwenye kombe la FA dhidi ya Huddersfield Town. Juan Mata alikuwa yuko sawasawa na beki wa mwisho wa The Terriers na akanyimwa goli halali. Na kuna matukio mengi tu kama haya tangu teknolojia hiyo ianze kutumika na ndio maana narudi pale pale je hii inapunguza au ndio inaongeza huo utata?

Hebu tuitazame ile teknolojia ya goli maarufu kama Goal Line technology. Hapa kwa kiasi kikubwa FIFA wamefaulu sana kwani ni wazi teknolojia hiyo imekuwa haina shaka, inatenda haki na ina ufanisi mkubwa mno. 
Mwamuzi ndani ya sekunde moja anakuwa ameshajua kama ni bao au sio bao. Hapa tena ndipo VAR inafeli. Mpaka mwamuzi afanye maamuzi inaweza kuchukua hata dakika 5 na ni wazi hii inapunguza kasi ya mpira wenyewe. Kwaiyo VAR bado na yenyewe imekuwa na utata lakini pia ina ufanisi mdogo jambo ambalo linapelekea mchezo wenyewe kupoa. 

Hebu vuta picha mpira umesimama kwa takribani dakika 5 alafu ukute VAR imekosea na maamuzi yenyewe. Ndio utatamani haki ibaki mahakamani tu ambapo na  kwenyewe huwa haitendeki wakati mwengine.

Na utata huu utazidi kuwepo sana tu mbeleni na teknolojia hii ndio itazidi kubaki njia panda. Ni wazi na ile ladha halisi ya mchezo inaondoka hebu vuta picha ni dakika ya 90 na bao halali la ushindi linakataliwa ni wazi kuwa soka itakosa hamu mbele ya hadhira kutokana na teknolojia hii. Ni wazi mikakati mbadala inatakiwa.

Hapa ndio penye tatizo. Malalamiko yamekuwa na yatazidi kuwa mengi na ni jambo ambalo naamini FIFA wenyewe linawafikia. Waamuzi wanakuwa kama sio waamuaji wa mwisho tena maana ni kama vile wanadhibitiwa na watu huko juu ambao wananguvu kubwa ya kuwashawishi kufanya maamuzi hata yasiyo sahihi wakati mwengine. Tukubali tu kuwa VAR inatuachia maswali mengi kuliko majibu.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.