Friday, August 23

USHIRIKI KATIKA SIASA: HAKI NA MIPAKA YA WATUMISHI WA UMMA

0


Kila raia ana haki ya kuchagua chama cha siasa anachotaka. Haki hii haiwatengi watumishi wa umma katika kufurahia uhuru wa kuamua ni chama gani wajihusishe nacho. Ukweli kwamba watumishi wa umma wapo kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi bila kujali imani au itikadi ya vyama vya wananchi hao unawapa jukumu la kimaadili la kuwahudumia wananchi hao bila chembe ya upendeleo au ubaguzi kutokana na imani zozote zinazohusiana na misimamo ya kisiasa. Makala haya yataegemea zaidi katika Kanuni za Maadili ya Utendaji Katika Utumishi wa Umma za mwaka 2005 kama zilivyotungwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa katika kifungu cha 34 cha Sheria ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2002 pamoja na Kanuni ya 65 (1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003.

HAKI YA USHIRIKI KATIKA SIASA

Kanuni za maadili ya utendaji katika utumishi wa umma zinampa haki mtumishi wa Umma kushiriki katika siasa huku zikielezea namna na kiwango cha ushiriki katika siasa. Kwa mujibu wa kanuni hizi Watumishi wa Umma wanayo haki ya kidemokrasia ya kuwa wanachama wa chama chochote cha siasa. Vilevile, wanayo haki ya kuvipigia kura vyama vyao pamoja na viongozi wao wakati wa uchaguzi mkuu.

Kanuni hizi pia zinaendelea kueleza kuwa Watumishi wa Umma wanaweza kushiriki katika masuala ya siasa katika vyama vyao ilimradi kwa kushiriki kwao hawataonyesha upendeleo katika utendaji wao wa kazi.

Hii inaonesha dhahiri kuwa si kosa kikanuni wala kisheria kwa mtumishi wa umma kushiriki katika shughuli za chama chake lakini siasa au chama cha siasa kisiwe chanzo cha upendeleo katika utendaji wake katika utumishi wa umma.

MIPAKA YA USHIRIKI KATIKA SIASA

Pamoja na haki walizopewa watumishi wa umma katika kushiriki katika siasa kanuni zinawataka kuzingatia baadhi ya mambo ili kuhakikisha kuwa wanatenda haki katika kutoa huduma na kuepuka kupendelea au kubagua watu kutokana na misiamamo ya kisiasa.

Kwa mujibu wa kanuni hizi watumishi wa umma hawaruhusiwi kufanya wala kujihusisha na masuala ya siasa wakati wa saa za kazi au mahala pa kazi. Hii inatupa tafsiri kuwa imani na misimamo ya watumishi wa umma haitakiwi kuingiliana na majukumu ya msingi wa watumishi wa umma katika kutoa huduma. Tofauti za misimamo ya kisiasa haitakiwi kuonekana katika maeneo ya kazi na hata kama mtumishi wa umma ataamua kujihusisha na masuala ya siasa inampasa kufanya hivyo nje ya muda wa kazi.

Ni dhahiri kuwa mfuasi wa chama chochote cha siasa anakuwa na mapenzi na chama chake. Changamoto inayowakuta watumishi wengi ni ukweli kuwa wanaitumikia serikali ambayo hauwezi kuitenganisha na siasa moja kwa moja. Kwa mfano, kwa sasa chama tawala kinachoiongoza serikali kwa sasa nchini ni Chama cha Mapinduzi (CCM). Kwa tafsiri ya haraka watumishi wote wa Umma wanatekeleza sera na ilani chama tawala bila kujali wao ni wapenzi au wafuasi wa chama gani. Hii inaweza kuwashawishi wao kutumia utumishi wao katika kutoa taarifa zinazoweza kunufaisha vyama vyao kwa malengo ya kisiasa.

Kanuni hizi zimetoa muongozo pia ili kuhakikisha kuwa utumishi hauwi daraja la taarifa zinazowezo kunufaisha vyama vya siasa. Kwa mujibu  kanuni hizi si ruhusa kwa watumishi wa umma Kutumia taarifa au nyaraka za kiofisi wanazopata kutokana na utumishi wao kwa umma kwa manufaa ya vyama vyao.

Pia, pamoja na ukweli kwamba kanuni hizi zinawapa watumishi wa umma haki ya kuwasiliana na viongozi wa vyama vyao vya siasa pia zinatoa katazo kwa watumishi hao kutumia ushawishi wa kisiasa kuingilia mgogoro wa kikazi baina yao na serikali. Kanuni hizi pia zinawataka watumishi wa umma   kuepuka kutumia ushawishi wa kisiasa kwa manufaa yao binafsi ambayo sio sehemu ya sera za Serikali.

UTII KWA SERIKALI

Kama tulivyoona apo awali kuna muingiliano mkubwa sana kati ya siasa na serikali. Kwa kifupi serikali inaongozwa na wanasiasa japo baadhi ya watendaji wanaweza kuchaguliwa bila kuangalia misimamo na itakadi zao za kisiasa. Ajira nazo serikali hasa kwa watumishi wa umma hazipaswi kuangalia misimamo na itikadi za kisiasa za watumishi ikiwa hawavunji kanuni, taratibu, sheria na miongozo ya utumishi wa umma.

Dhana ya utii kwa serikali iliyopo madarakani bila kujali itikadi, misimamo na imani za kisiasa za watumishi wa umma nalo limeelezwa vyema na Kanuni za Maadili ya Utendaji Katika Utumishi wa Umma. Kwa mujibu wa kanuni hizi Watumishi wa Umma wanapaswa kuitii Serikali iliyopo madarakani. Watumishi wa Umma wanatakiwa kutekeleza sera na maelekezo halali yanayotolewa na Mawaziri na viongozi wao wengine wa Serikali.

WITO

Watumishi wa umma wanatakiwa kujua kuwa serikali inahudumia wananchi wote kwa ujumla wao. Katika utoaji wa huduma kwa wananchi serikali pia ina jukumu la kuhudumia wananchi wote bila kujali vyama vyao na hivyo wao kama wawakilishi wa serikali katika kuhudumia wananchi wanapaswa kulizigatia hilo na kutoa huduma kwa watu wote na kwa usawa kama kanuni zinavyoeleza.

Pia ni jukumu la kila mtumishi wa umma kutekeleza sera na miongozo ya serikali iliyopo madarakani bila chembe ya kinyongo hata kama misimamo na itakadi ya vyama wanavyoviamini ina kinzana na ile ya chama tawala ambacho ndiyo kimepewa dhamana kikatiba kuiongoza serikali.

Share.

About Author

Leave A Reply