Saturday, August 24

MATABAKA NA ATHARI ZAKE NDANI YA TAASISI – Kelvin Mwita

0


Taasisi yoyote ile inajengwa na watu wengi wenye sifa na utofauti wa aina nyingi na ukweli huu ndio unaofanya taasisi yoyote iwe imara. Hii inajumuisha utofauti katika fani, uwezo, vyeo, fikra, jinsia, makabila na mambo mengine mengi. Kwa bahati mbaya wapo baadhi ya watu wanaodhani kuwa pengine wao ni bora kuliko wengine kwa sababu tofauti wanazozitumia katika kutathimini ubora na umuhimu wao.

Ukweli ni kwamba mtu yoyote katika taasisi akisitisha huduma au kuyafanya majukumu yake vibaya bila kujali udogo au ukubwa wa nafasi yake ni dhahiri kuwa taasisi nzima itaahirika kwa namna moja ama nyingine. Pengine uwa unampita mlinzi wa ofisini kwako bila hata kumsalimia lakini ukikutana na bosi wako unaulizia mpaka watoto wake kama ni wazima. Inawezekana unadhani mlinzi huyo hana thamani au hana umuhimu sana kwenye kazi au maisha yako-utawaza hivyo mpaka siku awe ndiyo mtu pekee anayeweza kuokoa maisha yako.

Taasisi nyingi zimejikuta zikiweka matabaka ya nyadhfa, makabila na hata matabaka yatokanayo na majukumu ya kikazi. Hili limefanya taasisi zigawanyike na kuondoa nguvu ya utimu ndani taasisi na kuwaacha wengine na maumivu.

Matabaka Hujengwa vipi?

Unaweza ukawa unajiuliza kuwa ni kwa jinsi gani matabaka hutokea ndani ya taasisi wakati kila mmoja anafaanya kazi ili kusaidia malengo ya taasisi yafikiwe. Jibu ni rahisi sana, mahali popote makundi hujengwa kirahisi zaidi miongoni mwa watu wanaoshabiiana au kufanana kwa aina fulani. Unaweza jikuta upo karibu na mtu fulani kwa sababu tu mlisoma chuo kimoja, mpo idara moja au baada ya kazi hukutana kijiwe kimoja kwa ajili yakupiga soga au kupata kahawa.

Kwa kifupi utagundua kuna sababu kadhaa za kutugawa na pia zipo za kutuunganisha. Mara nyingi watu wengi huegemea zaidi kwenye sababu za kutugawa na kuachana kabisa na zile za kutuunganisha na hapo ndipo tatizo huanza.  Mfanyakazi mwenzako anaweza pata tatizo kubwa mathalani kufiwa na mtu wa karibu lakini ukashindwa kumtembelea na kumpa pole eti tu kwa sababu anatoka idara tofauti na yako lakini ungeweza kutafuta sababu ya kuwaunganisha  kwa kuzingatia tu ni mfanyakazi kutoka taasisi unayofanyia kazi na hivyo ukaoneshaupendo na kumjali.

Kama tulivoona awali, mara nyingi matabaka huibuka kwa sababu tu mtu fulani au kikundi fulani kimejiona ni bora au muhimu kuliko kikundi kingine. Lakini kiuhalisia uthamani au ubora wa kikundi hicho hauwezi kuonekana bila ya msaada wa kikundi kingine kinachoonekana pengine siyo muhimu sana. Haya yanaweza kudhiirika kupitia mahusiano kati ya makundi haya mawili hasa kupitia kauli na matendo yao.

Nini kifanyike?

Ukweli ni kwamba kuwepo kwa matabaka kunaanza na mtu mmoja mmoja kabla haujawa ugonjwa wa kitaasisi vivyo hivyo katika kuondoa matabaka haya kunahitaji nia ya mtu mmoja mmoja. Hakuna sababu ya kujiona wewe ni bora kuliko mwingine au kumchukulia kama hana thamani katika taasisi husika. Wote tukiwa wakurugenzi nani atafanya usafi kwenye hizo ofisi tunazozitumia? Penda kila mtu bila kujali tofauti yoyote aliyonayo.

Katika ngazi ya taasisi ni vyema viongozi wakatambua kuwa wao wanamchango mkubwa sana katika kuiunganisha au kuigawa taasisi. Hii huanzia kwenye kauli za viongozi juu ya mtu au kikundi fulani. Matukio yanayo andaliwa na taasisi wakati mwingine yanawagawa watu bila kujua kwani kiasili yanachagua baadhi ya watu kuyashiriki huku wengine wakiwekwa kando kutokana tu na nafasi waliyonayo katika taasisi husika.

Pia katika kutambua mchango wa watu mbali mbali kwenye mafanikio ya taasisi mara nyingi kuna baadhi ya makundi ya watu kwenye taasisi usahaulika kutokana na ukweli kwamba uonekana kuwa hayana umuhimu au mchango wao ni mdogo japo kuwa kazi zao huzifanya kwa ufanisi mkubwa sana. Mifumo ya kitaasisi inatakiwa iweze kutambua mchango wa kila  mtu ili kusaidia wengine wasionekane kama ni ziada katika ufanyaji wa kazi.

Kwa kifupi upendo unatakiwa kuwepo myoyoni mwa watu na udhihirike kupitia vitendo na si vinginevyo. Kujuliana hali kusiangalie tabaka au cheo cha mtu yoyote na kwenye kusaidiana vivyo hivyo. Mara nyingi hili suala ni la kitamaduni zaidi; utamaduni unao jengwa na taasisi. Kwa mantiki hiyo, ni kitu kinachoweza kuanzishwa au kuzaliwa, kukua na kisipoangaliwa vizuri kikafa.

Ushirikiano na Ufanisi

Ushirikiano na ufanisi katika maeneo ya kazi ni vitu vinavyoenda pamoja; sehemu yoyote yenye matabaka yasiyo ya lazima chuki hujengwa na watu kuona eneo lao la kazi si rafiki. Injili ya upendo na ushirikiano isipohubiriwa vizuri maeneo ya kazi na watu kuiishi utendaji wa mtu mmoja mmoja ndani ya taasisi na taasisi kwa ujumla utaathiriwa vibaya.

Mtu yoyote anayehisi kubaguliwa na kutengwa na mtu, watu au mfumo ndani ya taasisi hawezi kutoa huduma kwa wateja wake kwa ufanisi. Matatizo mengine huanza ndani ya taasisi yenyewe na kutoka nje mpaka kuathiri wadau wengine muhimu. Ufanisi na utendaji kazi huathiriwa na mambo mengi na mengine huonekana madogo kabisa.

Angalizo

Pamoja na kusisitiza suala ushirikiano ili kuondoa matabaka ndani ya taasisi ni vyema watu kutambua na kuelewa ukweli kuwa kuna mazingira kwa namna moja ama nyingine yanaweza kusababisha baadhi ya watu kuwa karibu zaidi kuliko wengine. Kama tulivyoona awali, vikundi hujengwa kirahisi kwa sababu mbali mbali na nyingi zikiwa ni za kijamii. Ni rahisi watu wanaofanya kazi idara moja au ofisi moja kuwa karibu zaidi kwa sababu hutumia muda mwingi pamoja na hivyo kufanya umoja wao kuimarika zaidi. Pamoja na hayo hii haitakiwi kuwa sababu ya kuwatenga na kuwanyanyapaa wengine.

The post MATABAKA NA ATHARI ZAKE NDANI YA TAASISI appeared first on Kelvin Mwita.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.