Monday, August 19

KAULI ZINAVYOWEZA KUJENGA AU KUHARIBU SIFA NJEMA MAHALA PA KAZI – Kelvin Mwita

0


Kuna msemo unaosema siyo unachosema bali namna unavyosema ndiyo huleta maana. Msemo huu una maana kubwa sana na umejaa busara ambazo wengi wakiuzingatia wanaweza kujiepusha na matatizo mengi sana siyo tu maeneo ya kazi lakini katika sehemu nyingine nyingi.

Umewahi kutafakari kuwa kuna uwezekano ujumbe wa aina moja wenye lengo moja unaweza kuletwa na wawili tofauti lakini mmoja akaeleweka na mwingine asieleweke na pengine wazo likakataliwa kabisa. Mawasiliano ni sanaa na kila sanaa inahitaji ujuzi kukamilika na wengi wamekosa ujuzi muhimu katika mawasiliano suala linalowafanya washindwe kueleweka, wakose ushawishi na wakati mwingine wachukiwe kabisa na wengine.

Hii inatukumbusha kuwa makini na kufikiri kabla ya kusema chochote. Kuna haja ya kutafakari madhara yanayoweza  kuambatana na kauli zetu kabla ya kuziwakilisha. Je, ni vitu gani vya kuzingatia katika kauli zetu?

MATUMIZI YA KAULI ZENYE UBINAFSI AU JUMUISHI KWA

Hebu jiulize swali dogo tu; kati ya bosi anayetumia kauli kama hii anapoongea na wafanyakazi wake ‘ofisi yangu haitamvumilia mtu mzembe’. Kisha tafakari bosi mwingine mwenye lengo la kufikisha ujumbe ule ule lakini yeye akasema ‘ofisi yetu haitamvumilia mtu mzembe’. Kwa kifupi utapenda kufanya kazi na huyu wa pili kwani kupitia kauli zake anaonesha kunyenyekea lakini anakubali kuwa yeye ni miongoni mwa wengi na siyo mtu aliyejitenga na wengi.

Viongozi wenye kauli jumuishi wana nafasi kubwa sana ya kujijengea ushawishi na kukubalika na wafuasi wao na hivyo kupunguza uwezo wa kujenga hoja zitakazo eleweka na kuungwa mkono na wafuasi wao. Kila mtu anapenda kuongozwa na ‘kiongozi wa watu’ yaani kiongozi anayeonekana ni sehemu ya timu kubwa na siyo mtu wa pembeni anayetazama nini kinafanyika.

KAULI ZA UWAJIBIKAJI

Timu inapocheza uwanjani uwa na wachezaji tofauti wenye uwezo tofauti tofauti na majukumu tofauti pia. Pamoja na hayo lengo la timu uwa ni moja. Inapotokea mchezaji mmoja katika timu amefanya vibaya timu uwa inawajibika kwa ujumla wake na uwa si vyema kutafuta nani mchawi ili atupiwe lawama huku mchezo ukiendelea. Pamoja na hayo yule ambaye kwa namna moja ama nyingine anaweza kuwa alisababisha kushindwa kwa timu anapaswa kuwajibika kwa kosa lake kwa lengo la kumjenga na kujenga timu.

Timu ikifungwa na kisha ukamsikia kocha anasema ‘makosa mliyo yafanya yamesababisha mfungwe’ huyu si kocha mzuri kwani ameshindwa kuwajibika pamoja na timu. Viongozi wenye kauli kama hizi kwenye taasisi yoyote ile hawafai kuitwa viongozi bora. Kiongozi ambaye taasisi ikifanya vizuri anasema ‘nmefanya vizuri’ lakini ikifanya vibaya anasema ‘mmefanya vibaya’ anaondoa hamasa kwa wafuasi wake na bila kujua anarudisha timu yake nyuma badala ya kuipeleka mbele.

Hii haimaanishi kuwa mtu mmoja mmoja anapokosea asiambiwe au kuwajibishwa lakini uwajibikaji lazima ugawanyike kwenye uwajibikaji wa jumla na uwajibikaji wa mtu mmoja mmoja. Na katika uwajibikaji wa mtu mmoja mmoja kuna haja ya kutumia busara ili kuhakikisha watu hawapotezi motisha na ari ya kufanya kazi.

UKOSOAJI

Kila mtu hukosea na  ni njia nzuri sana ya kujifunza lakini kwa wengine mafunzo haya huambatana na maumivu ya nafsi yasiyo ya lazima. Kwa kifupi watu hawapendi kufanya makosa na kufanya makosa huwaumiza watu wengi sana. Kwa kuzingatia hili tunapowakosoa kuna haja ya kutumia busara sana. Hii siyo kwa viongozi pekee bali hata wafuasi kwa viongozi wao na kati ya mfuasi mmoja na mwingine. Umefanya jambo la kijinga sana, sijawahi kuona mpuuzi kama wewe, ulishindwa hata kutumia akili kidogo? Na kauli nyingine kama hizi si namna bora au chanya ya kukosoa yenye lengo la kuweka mambo sawa. Jiweke wewe kwanza kwenye nafasi ya mkosolewaji kabla haujarusha maneno ya dhihaka na mauzi.

“Pole sana, najua haukudhamiria lakini haukupaswa kufanya hivyo, ulitakiwa ufanye hivi…” maneno ya namna hii ndiyo wengi hupenda kuyasikia kutoka kwa watu wetu wa karibu na siyo vingine. Kujifunza siyo lazima kuambatane na machozi na maumivu ya nafsi. Kauli za kukosoa zinaweza kuja kwa njia ya upole zinazo ambatana  na maneno ya upendo.

Hii haimaanishi kuwa viongozi na watu wengine wanatakiwa kuwachekea wale wanaofanya makosa, hapana. Wanatakiwa kuonywa na pengine kuadhibiwa lakini busara inatakiwa kutumika kwani ukali, kejeli, dharau na dhihaka katika ukosoaji mara nyingi hazijengi mahusiano mazuri na mara nyingi hazifikii lengo la kuboresha au kurekebisha makosa ili yasitokee tena.

MAHALA PA KUTOLEA KAULI

Kwa bahati mbaya wapo wanaoamini kila kitu kinaweza kuzungumzwa kila mahali. Hii imesababisha wengine kutoa kauli za faragha mbele ya kadamnasi. Kauli za kuadhibu si lazima na si vyema zisemwe mbele ya wafanyakazi wengine. Wapo wanaoamini kuwa kauli hizi zikisemwa mbele ya wengi pengine wengine watajifunza lakini tafsiri uwa ni nyingi na za tofauti. Watu wanaweza wasijifunze kwamba hawatakiwi kurudia kosa kama hilo lakini wakajifunza kuwa wewe si kiongozi mwenye staha, siri na busara na hivyo kukupunguzia heshima, kukubalika na ushawishi. Sio kila kitu kinastahili kusemwa mbele ya kadamnasi; akiba ya maneno ni muhimu sana.

Mwisho, utoaji wa kauli unatakiwa kuambatana na tafakari kabla ya kutolewa. Hiki ninachotaka kusema kama ningeambiwa mimi ningejisikiaje, ni lazima nikiseme? Kama ndiyo, ipi ni namna bora zaidi ya kukiwasilisha. Hakikisha ulimi haukuponzi wala hauwaumizi au kuwaponza wengine.

The post KAULI ZINAVYOWEZA KUJENGA AU KUHARIBU SIFA NJEMA MAHALA PA KAZI appeared first on Kelvin Mwita.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.