Friday, August 23

DHIBITI MATUMIZI YA MITANDAO YA KIJAMII ILI UONGEZE UFANISI KAZINI – Kelvin Mwita

0


Mitandao kijamii imekuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Teknolojia imetusaidia sana katika kuwaweka karibu wale walio mbali huku tukipata taarifa na kuburudika kupitia mitandao ya kijamii inayowezeshwa na simu zetu za mkononi na vifaa vingine vya kielectroniki. Pamoja na uhumuhi wa teknolojia hii matumizi mabaya au yaliyopitiliza yamekuwa na athari sana katika utendaji kazi wa watumiaji. Kwa watu wengi mitandao ya kijamii imekuwa ikiwatawala badala ya kuitawala na kuathiri utendaji katika shughuli nyingine.

Mutumizi ya mitandao ya kijamii yaliyopitiliza hukera watu wengi sana hasa wale unaowahudumia. Umeshawahi kwenda benki, umechoka upo kwenye foleni ndefu halafu muhudumu kasitisha kutoa huduma huku macho yake yakiwa kwenye simu yake.

Utajuaje kama una matumizi yaliyopitiliza ya Mitandao ya kijamii

Wengi ni wahanga wa matumizi ya mitandao ya kijamii lakini hawajajua kuwa wameshakuwa ‘mateja’ wa teknolojia hii. Moja ya namna ya kujua kuwa matumizi yako siyo ya kawaida ni kuangalia kama matumizi ya mitandao ya kijamii ni kitu cha kwanza siku yako inapoanza. Ukiamka hakuna kingine unachowaza kufanya zaidi ya kufungua WhatsApp, Instagram, facebook au mtandao wowote kuperuzi.

Kitu kingine ni kuwaza kinachoendelea katika mitandao ya kijamii hata kama unashughuli nyingine tofauti kabisa. Ukiona mara kwa mara unapokuwa unafanya shughuli zako mawazo yako yanakuwa kwenye yale yanayoendelea kwenye mitandao ni dalili kuwa umeshakuwa mtumwa wa teknolojia hii.

Dalili nyingine ni kushindwa kujizuia kuingia kwenye mitandao hiyo hata kama unashughuli nyingine za kufanya. Kwa kifupi, mitandao ya kijamii inakuwa sehemu ya kila kitu unachokifanya. Wakati ukiendelea kutoa huduma au ukifanya shughuli fulani haiwezi kukamilika bila kuingiliwa na matumizi ya mitandao.

Madhara

Madhara ya matumizi yaliyokithiri ni mengi sana. Kwanza, ni kupoteza muda ambao ungeutumia katika kazi au shughuli unayoifanya. Hebu tafakari ni muda kiasi gani unautumia katika mitandao ya kijamii kwa siku halafu tafakari ingekuwa vipi kama muda huo ungeutumia katika kazi au shughuli unazofanya. Ifamike kuwa matumizi ya mitandao ya kijamii si kitu kibaya lakini matumizi yaliyo pitiliza.

Kukosekana kwa umakini katika kazi ni athari nyingine katika utumiaji uliokithiri wa mitandao hii. Ili kazi ifanywe kwa ufanisi na ufasaha inahitaji mtu anayeifanya azingatie umakini huku akili yake ikiwa tulivu. Kwa watu wenye matumizi ya mitandao ya kijamii iliyopitiliza hili suala ni gumu kwao kwani wakati wanafanya shughuli zao akilini mwao wanawaza yale yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii.

Matumizi ya aina hii pia uathiri mahusiano maeneo ya kazi na wale unaofanya nao kazi. Kitu ambacho wengi uwa hawakigundui ni ukweli kwamba mara nyingi matumizi ya mitandao ya kijamii huwaleta karibu wale walio mbali na kuwaweka mbali wale walio karibu. Watu wenye matumizi yaliyopitiliza ya mitandao ya kijamii wapo kwenye hatari ya kuathiri mahusiano mazuri na wale wanaofanya nao kazi. Ni kitu kinachokera sana ukiwa unaongea na mwenzako ukimueleza mambo ya msingi lakini yeye anajishughulisha na simu yake.

Namna ya kukabiliana na matumizi yaliyokithiri

Kwanza, kabla ya kuanza kulishughulikia tatizo hili muhanga wa tatizo hili anatakiwa akubali ukweli kuwa kuna tatizo. Ni vigumu kukabiliana na tatizo ambalo haujakubali kwamba lipo. Ukweli huu unatoa wito kwa mtu binafsi kujitathmini na kuangalia mwenendo wake katika matumizi ya mitandao ya kijamii na kuona kama si ya kawaida. Waweza pia kuwauliza wale walio karibu yako kusikia wanasemaje juu ya matumizi yako.

Endapo unaona au utaona matumizi yako yamezidi kiasi ni vyema kuchukua hatua mapema kwa kuwa na nidhamu ya matumizi. Si muda wote ni lazima ushike simu yako au kifaa chochote cha kielectroiniki kinachoweza kurahisisha matumizi ya mitandao ya kijamii.  Anza kwa kupunguza muda unaoutumia katika mitandao kidogo kidogo; mara nyingi siyo rahisi kuacha ghafla.

Jizoeshe kushika simu yako unapokamilisha shughuli fulani au kipindi cha mapumziko ili upate muda wa kufanya kazi yako kwa umakini na kuondoa muingilianao unaosababishawa na mitandao ya kijamii.

Vifaa vya kielectroniki tunavyovitumia vinauwezo wa kudhibiti mtandao unaowezesha matumizi ya mitandao ya kijamii. Pale unapokuwa unashughuli zako ni vyema kudhibiti au kuzuia mtandao wa intaneti ili jumbe zisiingie kwa wakati fulani.

Njia nyingine ni kujiondoa kwenye makundi yasiyo na tija mtandaoni. Teknolojia katika mitandao ya kijamii inawezesha watu kuunda makundi yenye malengo mbali mbali. Ukweli ni kwamba siyo makundi yote uwa na tija na kukujenga kwa namna yoyote ile zaidi ya kupiga soga na kujadili mambo yasiyo na maana na pengine maadili.

Kwa kawaida akili ya mwanadamu ni ya kidadisi; hata kama kundi halina mambo ya maana ni dhahiri utasukumwa kutaka  kujua nini kinaendelea kwenye kundi fulani. Suala hili husababisha kuwa mtu wa kuzunguka kundi baada ya kundi na kujikuta ukipoteza muda mwingi mtandaoni. Hakikisha makundi uliyopo una sababu za msingi za kuwa humo na kama kundi halina nidhamu ya kuongoza mijadala si lazima uendelee kuwepo humo.

Jambo jingine la msingi na la kuzingatia; siyo lazima kila ufanyacho, uwazacho au uonacho ni lazima ukiweke mtandaoni. Jifunze kuyaacha mengine yapite tu. Kitu kinachotuponza mara nyingi ni kuweka picha zetu kwenye mitandao ya kijamii kila tunapojisikia kufanya hivyo. Madhara yake ni kutaka kujua mrejesho wa hicho tunachokifanya na mwisho kujikuta walevi wa mitandao hii na kutupotezea umakini kwenye kazi zetu na umakini ambao ni muhimu sana katika utendaji na ufanisi kazini.

The post DHIBITI MATUMIZI YA MITANDAO YA KIJAMII ILI UONGEZE UFANISI KAZINI appeared first on Kelvin Mwita.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.