Sunday, August 18

UCSAF YAPEWA SIKU 14 KUWASILISHA RIPOTI YA HALI YA MAWASILIANO PEMBA

0


 Meneja Ofisi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Zanzibar, Bi. Esuvatie-Aisa Masinga akitoa taarifa ya hali ya mawasiliano Zanzibar kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto) wakati wa ziara yake kisiwani humo.
 Meneja Msaidizi Mtandao wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Zanzibar Bwana Mohamedi Ali Haji akimuonesha Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto) njia yanakopita mawasiliano kutoka Dares Salaam kuja Zanzibar wakati wa ziara yake kisiwani humo.
 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye ( wa kwanza kulia) akisikiliza kwa makini maelezo kutok akwa mfanyakazi wa TTCL kuhusu mwitikio wa wateja kwa huduma zinazotolewa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wakati wa ziara yake Zanzibar.
 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano (kulia) akitoa maelekezo kwa mwakilishi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Bwana John Munkondya kuhusu vituo vya mawasiliano vilivyopo Zanzibar wakati wa ziara yake kisiwani humo.
 Mfanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) Zanzibar, Bwana Khalfan Mmkahirika akimuonesha Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano namna scanner inavyofanya kazi ya kukagua mizigo na vifurushi vinavyosafirishwa na Shirika hilo ndani na nje ya nchi ili kulinda usalama wa raia na taifa wakati wa ziara yake Zanzibar. Mwenye koti nyeusi ni Kaimu Posta Masta Mkuu wa Shirika hilo Bwana Hassan Mwang’ombe.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa ziara yake kwa taasisi za mawasiliano Zanzibar. Kushoto ni Kaimu Posta Masta Mkuu wa Shirika hilo Bwana Hassan Mwang’ombe na kulia ni Mkurugenzi wa Huduma wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) Bwana Hussein Selemani Nguvu.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye ameupa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) wiki mbili kwenda Pemba kukagua hali ya mawasiliano ya simu za mkononi na kuwasilisha taarifa hiyo ofisini kwake.


Mhandisi Nditiye ameyasema hayo akiwa kwenye ziara yake ya kikazi Zanzibar ya kukagua hali ya mawasiliano kisiwani humo na kutembelea taasisi za mawasiliano zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambapo suala la mawasiliano ni la muungano.

Nditiye amesema kuwa amepokea taarifa kutoka kwa wabunge wa Kisiwa cha Zanzibar kuwa hali ya mawasiliano kwenye kisiwa hicho sio nzuri na sehemu nyingine hakuna mawasiliano licha ya kuwa kuna minara ambayo inatoa huduma za mawasiliano ila kutokana na jiografia ya Pemba ambapo kuna milima na mabonde hivyo mawasiliano si ya uhakika. “Nawaagiza muende Pemba mkaainishe maeneo yote ambayo hayana mawasiliano na muwasilishe taarifa hiyo ofisini kwangu baada ya wiki mbili,” amesema Mhandisi Nditiye.

Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Ofisi ya Zanzibar Bi. Esuvatie-Aisa Masinga wakati akiwasilisha taarifa yake kwa Mhandisi Nditiye kuhusu majukumu ya ofisi yake ya usimamimizi na udhibiti wa mawasiliano na posta, amekiri kuwa yapo baadhi ya maeneo Pemba na Unguja ambapo hali ya mawasiliano sio nzuri na hairidhishi. 

Ameongeza kuwa Pemba kuna maeneo ambayo hakuna mtoa huduma na pale ambapo mawasiliano yapo bado ubora wa huduma sio nzuri. Pia ameyataja maeneo yasiyo na mawasiliano kwa upande wa Mkoani kuwa ni Kengeja na Chokochoko na kwa upande wa Micheweni ni Konde na Gando.

Amefafanua kuwa sehemu nyingine za Pemba mtandao wa Zantel upo lakini ‘coverage yake’ sio nzuri. “Ili kufanya mawasiliano yawe mazuri kwa Pemba, ni muhimu ‘site’ zikaongezwa hasa ukizingatia hali ya kijiografia ya kisiwa hicho,” amesema Masinga. Mawasiliano ya kisiwa cha Pemba hayaridhishi, tunapendekeza Serikali kupitia UCSAF kuweka minara zile sehemu ambazo hakuna mawasiliano.

Naye mwakilishi wa UCSAF Bwana John Munkondya amepokea maelekezo ya Mhandisi Nditiye ambapo Mfuko huo utakwenda Pemba kukagua hali ya mawasiliano na kuwasilisha ripoti ofisini kwake ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata mawasiliano ya uhakika. “Sisi kama UCSAF tumechukua taarifa hii ya maeneo ambayo hayana mawasiliano, tutakwenda Pemba kukagua na maeneo hayo yataingizwa kwenye utaratibu wa kanda maalumu ili tuweze kufikisha mawasiliano,”amesema Munkondya.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Nditiye amekagua utendaji kazi wa moja ya scanner mpya ambazo Wizara yake imeipatia Shirika la Posta Tanzania ili ziweze kutumika kukagua mizigo, vifurushi na vipeto ambavyo vinaingia na kutoka ndani na nje ya nchi ili kudhibiti uingizaji na usafirishaji wa bidhaa na vifaa ambavyo ni hatarishi kwa usalama wa raia na taifa letu. 

Kaimu Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bwana Hassan Mwang’ombe amemweleza Mhandisi Nditiye kuwa Wizara yake imewapatia scanner nne zenye thamani ya shilingi milioni 421 ambapo tayari zimefungwa kwenye mikoa mbali mbali ili ziweze kuwasaidia kupunguza udanganyifu ambao unajitokeza ambapo baadhi ya wateja wasio waaminifu wamekuwa wakisafirisha baadhi ya vifaa na bidhaa kama vile madawa ya kulevya kinyume na sheria za nchi. 

Pia, Mhandisi Nditiye ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi, ufungaji wa samani na uwekaji wa vifaa vya TEHAMA kwenye moja ya kituo cha mawasiliano kilichojengwa na UCSAF kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma za mawasiliano. 

Munkondya amemweleza Mhandisi Nditiye kuwa UCSAF imejenga vituo kumi vya mawasiliano kwa gharama ya shilingi milioni 721 na ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 98 ambapo vituo sita vipo Unguja na vine vipo Pemba. Ameongeza kuwa UCSAF inaweka samani, vifaa vya TEHAMA pamoja na kompyuta kumi kwa kila kituo, kujenga choo na uzio ili wananchi waweze kupata huduma ya mawasiliano kwa gharama nafuu.

Naye mjumbe wa Bodi ya TPC Bi. Khadija Shaban amemuomba Mhandisi Nditiye kuwa vituo hivyo vya mawasiliano vya Pemba na Unguja visimamiwe na kuendeshwa na TPC ili viweze kudumu kwa muda mrefu kama ambavyo inafanyika hivyo Tanzania Bara.

Mhandisi Nditiye akiwa katika ziara yake kisiwani Unguja, ametembelea na kukagua mitambo ya Shirika la TTCL, hali ya biashara na namna wanavyowahudumia wateja ambapo ameona miundombinu ya Shirika hilo inavyosambaza huduma za mawasiliano kutoka Tanzania Bara kuja kisiwa cha Zanzibar. 

Nditiye ameiagiza TTCL kufunga mitambo ya mawasiliano kwenye meli za maziwa makuu na baharini ili wananchi wanaposafiri waweze kupata mawasiliano ya uhakika ya simu za mkononi na huduma za intaneti. 

Pia, ameiagiza TCRA kuwasajili watu wote wanaosafirisha mizigo, vifurushi na vipeto na kuwapatia leseni ili walipe gharama ya kufanya huduma hiyo ili wananchi wawatambue na kuwa na imani nao hasa pale ambapo mzigo unapotea waweze kulipwa na Serikali iweze kupata mapato yake.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.