Saturday, August 24

SERIKALI KUGHARAMIA MAZISHI MWANAFUNZI AQWILINA AKWILINE ALIYEKUFA KWA ALIYEPIGWA RISASI

0


Pichani kati ni Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Prof Joyce Ndalichako akizungumza mbele ya Waandishi wa habari mapema leo mchana jijini Dar,kuhusu kifo cha Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Aqwilina Akwiline ambaye amepoteza maisha baada ya kupigwa risasi Februari 16 mwaka huu eneo la Mkwajuni -Kinondoni jijini Dar es Salaam, kushoto ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni pamoja na kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Dkt. Akwilapo
Baadhi ya Waandishi wa vyombo vya habari wakiendelea kurekodi na kusikiliza yaliyokuwa yakizungumzwa na viongozi waandamizi wa Serikali kufuatia kifo cha Mwanafunzi huyo, kilichotokea kwa kupiga risasi hivi karibuni Kinondoni,jijini Dar.Picha na Michuzi Jr.

*Waziri Ndalichako asema Taifa limepata pigo kubwa, aomba utulivu

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii

SERIKALI kupitiza Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi imesema itagharamia mazishi ya mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Aqwilina Akwiline ambaye amepoteza maisha baada ya kupigwa risasi Februari 16 mwaka huu eneo la Mkwajuni jijini Dar es Salaam

Imesema kifo cha mwanafunzi huyo ni pigo kubwa kwa familia, Serikali,Wizara ya Elimu, wanafunzi, ndugu, jamaa na marafiki huku ikiomba Watanzania wote kuwa watulivu katika kipindi hiki wakati uchunguzi wa kifo hicho ukiendelea kufanywa na vyombo vya dola.

NI PIGO KWA TAIFA

Akizungumza Dar es Salaam leo kuhusu kifo cha Aqwilina aliyepigwa risasi akiwa kwenye daladala, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Profesa Joyce Ndalichako amesema Taifa limepata pigo kubwa kwa kuondokewa na mwanafunzi huyo ambaye hakuwa na hatia ya aina yoyote.

Amesema kabla ya tukio la kupigwa risasi mwanafunzi huyo alikuwa amebeba barua kwenda kuomba kufanya mafunzo kwa vitendo lakini kifo kimekatisha ndoto zake na harakati za kuisaka elimu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.

Prof.Ndalichako amesema tukio la kifo hicho kimegusa hisia za watanzania wengi na Rais, Dk.John Magufuli mbali ya kutoa pole kwa familia na wananchi wote ameonesha kuguswa na tukio hilo.

“Ni msiba mkubwa ambao umelipata Taifa letu kwa kifo cha mwanafunzi wetu mpendwa.Kifo kimetokea wakati wa kudhibiti maandamano yaliyofanyika Februari 16 mwaka huu huko Kinondoni. Tunatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji.

“Serikali imepata pigo kubwa kwani inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kuosmesha wanafunzi wa kitanzania na mwanafunzi aliyefariki ni miongoni mwa wanafunzi aliyekuwa anasoma kwa mkopo wa Serikali.Mwanafunzi huyu alikuwa mtiifu na amefariki .Ni msiba ambao hakika umetugusa sisi wote,”amesema.

SERIKALI KUGHARAMIA MSIBA

Wakati huo huo, Profesa Ndalichako amesema imeamua kuchukua jukumu la kugharamia msiba huo hadi pale mwanafunzi huyo atakapopumzishwa kwenye nyumba yake ya milele wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.

“Kama ambavyo nimetangulia kueleza hapo awali namna ambavyo kila mmoja wetu ameguswa na kifo cha mpendwa wetu lakini Serikali kwa niaba ya Wizara ya Elimu tumechukua jukumu la kugharamia msiba huu.

“Tunaomba katika kipindi hiki Watanzania wote tuungane katika kushiriki kwenye msiba wa mpendwa wetu na nitoe rai kwa wanafunzi wote wakiwamo wa elimu
ya juu kuwa watulivu wakati hatua mbalimbali zikiendelea kufanyika.Waliohusika wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria,”amesema Prof. Ndalichako.

Ameomba wananchi wote kuwa kwa sasa si vema kuanza kulaumiana na badala yake ni kuwa wamoja na wenye utulivu wa kati mwili wa mwanafunzi huyo ukisubiriwa kupumzishwa na wakati hatua nyingine za vyombo vya dola vikiendelea na uchunguzi wakeRead More

Share.

About Author

Comments are closed.