Thursday, August 22

MARUFUKU MADAKTARI KUJAZA FOMU ZA UCHUNGUZI AFYA BILA KUPIMA WANAFUNZI TB-UMMY MWALIMU

0


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (MB) akisisitiza jambo mbele ya Waandishi wa Habari (Hawapo kwenye Picha), wakati wa Maazimisho ya siku ya Kifua Kikuu Duniani, tukio limefanyika mapema leo katika ukumbi wa Habari Maelezo jijini Dodoma.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia kwa ukaribu tamko la Kifua Kikuu (TB) lililokuwa linatolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (MB) katika ukumbi wa Habari Maelezo jijini Dodoma mapema leo.

Na Mwandishi Wetu.

WAZIRI wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema ni marufuku kwa madaktari kujaza fomu za uchunguzi wa afya bila kupima wanafunzi husika iwapo ana ugonjwa wa Kifua Kikuu(TB) au laa kwani kufanya hivyo ni kuliangamiza kwa makusudi Taifa kwa uzembe ambao hauwezi kuvumilika.

Pia amesema Serikali inatambua umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii katika mapambano ya kutokomeza TB na huku akieleza mpaka sasa takribani watoa huduma 1530 kati ya 5000 katika ngazi ya jamii ambao wamepata mafunzo ya muda mfupi ya Kifua Kikuu na hivyo wanaweza kuwabaini wagonjwa wa TB na kuwafuatilia watoto wanaopata matibabu katika maeneo yao.

Waziri Mwalimu ametoa kauli hiyo leo kwenye tamko lake kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya TB duniani ambayo hufanyika Machi 24 ya kila mwaka ambapo amefafanua TB ni ugonjwa wa kuambukiza ambao unaoongoza kwa kusababisha vifo vingi duniani.

Hivyo amasema ili kukabiliana na ugonjwa huo pamoja na hatua mbalimbali zinazochukuliwa amewaagiza waganga wafawidhi wote wa hospitali na vituo vya huduma kuhakikisha watoto wote wanaoanza shule za bweni wanafanyiwa uchunguzi wa TB kikamilifu kabla ya kuanza masomo.

Akifafanua zaidi anasema takwimu za Shirika la Afya Duniani(WHO) inakadiriwa zaidi ya watu milioni 10.4 huugua TB kila mwakaDuniani na milioni Moja kati ya hao ni watoto wenye umri chini ya miaka 15.

“Tafiti nyingi zinaonesha kuwa karibia theluthi moja ya Watanzania tayari wamepata maambukizo ya Kifua Kikuu na wanaishi na vimelea mwilini mwao. Kauli mbiu ya mwaka huu inasema ” Viongozi Tuwe Mstari wa Mbele Kuongoza Mapambano ya Kutokomeza TB.”

“Nchini Tanzania kila mwaka jumla ya watu 160,000 wanakadiriwa kuwa na ugonjwa wa Kifua Kikuu.Nitoe mwito kwa viongozi wa ngazi zote kuifanya vita dhidi ya TB kuwa agenda muhimu na ya kipaumbele,”amesema.

Amewakumbusha Watanzania TB inatibika na kupona kabisa, dawa zake zinatolewa bure na zinapatikana sehemu zote nchini katika vituo vya Umma na Binafsi.

Amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na tatizo la Kifua Kikuu nchini ikiwemo kuimarisha uchunguzi na ugunduzi wa Kifua Kikuu katika Vituo vya Afya.

Pia Serikali na wadau mbalimbali wanaendelea na utekelezaji wa kampeni za uhamasishaji na upimaji wa Wananchi katika maeneo ya migodi, makazi duni kwenye miji mikubwa, magereza na shule za bweni.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.