Tuesday, August 20

JE MNAJUA NI KOSA KWA WATU BINAFSI KUKOPESHANA KWA RIBA?.

0


Na Bashir Yakub.
+255784482959.

Ni muhimu sana kwenu kulijua hili. Anakuja mtu anaomba umkopeshe hela.Unamkubalia lakini kwa sharti la riba ya kiasi fulani.

Au mkopaji mwenyewe anakushawishi kuwa ukimpa atarejesha kwa riba. Vyovyote itakavyokuwa suala la msingi ni kuwa katika makubaliano yenu mmeweka riba.

Basi jueni jambo hili ni kinyume cha sheria na halikubaliki.Ikiwa uliyemkopa atakataa kukulipa hela yako basi utakuwa huna la kufanya.Hata ukienda mahakamani bado mahakama haiwezi kukusaidia. Haiwezi kuamuru ulipwe hiyo hela. Utakuwa umepoteza.

Na si tu utapoteza hizo za riba bali pia hata hizo ulizomkopa(principal sum). Usimkopeshe mtu kwa riba kwani akiamua asikulipe huna la kumfanya kwa mujibu wa sheria.

Wengine hukimbilia polisi kulalamika. Yumkini ni makosa. Na huyo askari anayeshughulikia kesi kama hii yupo katika makosa. Si kazi ya polisi kushughulikia masuala kama haya.

Yafaa tuyajue haya ili tuwe makini.Mahakama kuu na ya rufaa zimeamua hivyo katika kesi nyingi .

Mojawapo ni Shauri Namba 66/2007 kati ya ULF NILSON dhidi ya DR. TITO MZIRAY ANDREW . Katika shauri hili Jaji A.F.NGWALA alisema kwamba, hata kama kuna makubaliano ya maandishi kuhusu malipo ya riba bado mtu binafsi ambaye hakusajiliwa wala hana leseni ya kufanya biashara ya fedha hawezi kutoza riba.

Mwishoni alibatiliisha makubaliano yote ya huo mkopo.Kubatilishwa kwa makubaliano yote ya huo mkopo maana yake hata zile fedha ulizomkopa ambazo sio riba nazo zinakufa kwasababu mkataba mzima umebatilishwa, na mahakama imeuazimia(declare) kuwa haramu.

Unaweza kuona utakuwa umepoteza kiasi gani.

Na hali ni hii hii hata kwa kampuni ambazo hufanya biashara hizi bila leseni ya biashara ya fedha.

1. KUHUSU REHANI YOYOTE KAMA IMEWEKWA.

Yawezekana wakati unamkopa aliweka mali yoyote rehani. Iwe baiskeli,pikipiki,gari, nyumba, kiwanja au kinginecho madhali tu ni rehani. Hii nayo ni haramu na imekatazwa na sheria.

Kifungu cha 6( 1 ) cha Sheria ya Mabenki naTaasisi za Fedha kinasema kuwa mtu yeyote ambaye hafanyi biashara ya benki/fedha na hana leseni ya biashara hiyo haruhusiwi kupokea rehani kwa ajili ya mkopo kutoka kwa mtu yeyote. Kifungu kidogo cha ( 2 ) kimetangaza adhabu ya faini isiyozidi milioni 20,kifungo kisichozidi miaka mitano, au vyote kwa pamoja yaani kifungo pamoja na faini.

Kumbe basi utaona kuwa sio tu hairuhusiwi bali pia waweza kwenda hata jela. Kwa hiyo ni vyote kutoza riba, pamoja na kuomba/kupokea rehani ni makosa.

2. TUSICHOELEWA VIZURI NI HIKI.

Kuna maneno mtaani kuwa mkataba ni mkataba na makubaliano ni makubaliano ilimradi tu wahusika wote wameridhia na wameandikishana na kusaini kwa hiari zao. Mtu anategemea kumwambia mwenzake “si ulisaini hapa”. “Ulisaini ukitegemeanini”, na maneno mengine kama hayo.

Ndugu, maneno hayo hayana msaada kwako, unapoteza tu mda.Kifungu cha 10 cha Sheria ya Mikataba kinasema kuwa makubaliano yote ni mikataba kama yamefanyika kwa hiari, na wahusika wenye sifa, kwa biashara halali, na makubaliano hayo yasiwe yamekatazwa na sheria nyingine yoyote.

Utaona kifungu kinasisitiza kuwa hata kama makubaliano yatakuwa kama kifungu kilivyosema lakini bado makubaliano hayo yasiwe yamekatazwa na sheria nyingine yoyote .Kwahiyo ni kweli kabisa kuwa makubaliano ni makubaliano isipokuwa yanakuwa makubaliano kamili na halali kama hayajatangazwa na sheria nyingine kuwa haramu. Na makubaliano ya riba na rehani kwa ambao sio taasisi ya fedha na wasio na leseni yametangazwa na sheria nyingine ambayo ni Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha kuwa haramu. Kwa msingi huu ile dhana ya
makubaliano ni makubaliano tuliyoizoea mtaani inakufa na haipo tena .

Hivyo usiweke tena katika mawazo yako utetezi/kinga ya aina hiyo. Haitakusaidia .

3. KUHUSU KUSAIDIANA HELA KAMA WANADAMU.

Sheria haikatazi kusaidiana hela kwa kuandikishana. Hela mnaweza kusidiana kwa kukopana. Lakini iwe tu kiubinadamu(socially) bila ya riba wala rehani(commercially).

Msaada uwe msaada na isiwe katika mfumo wa faida,mapato au biashara. Na hapa mnaweza kuandikishana na mahakama ikasaidia kupakana haki ikiwa mkopwaji amekaidi malipo.

Kwahiyo ndugu jihadhari. Jihadhari hasa wewe mtoa mkopo.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.