Wednesday, August 21

DKT MWAKYEMBE, MONGELA WAKIRI UDHAIFU

0


Juzi kwenye mada zilizoandaliwa katika jukwaa la Tafakuri la pili ziliyohusu uafrika wetu, Naibu Natibu Mkuu Mstaafu wa umoja wa mataifa Getrude Mongella na Waziri wa habari, michezo, sanaa na utamaduni Dk. Halson Mwakyembe wamekiri kuwa viongozi wa sasa baada ya timu ya Nyerere waliisaliti misingi ya watangulizi wao.

Kauli hii wamezitoa kwa wakati tofauti baada ya maswali ya msingi kutoka kwa vijana wa leo (wasomi) machachari kuhoji juu ya misingi waliyofundishwa viongozi hao kutoka kwa akina Nyerere kuhusu, utaifa, uzalendo nk kwamba ilikuwaje wao wenyewe hawakuifuata na kuiendeleza hadi leo ili nao waweze kuwarithisha vijana wa leo badala ya kuwataka vijana tu ndio wawe wazalendo?.

Getrude Mongella katika kujibu swali hilo aliishia kusema: “…nadhani tulikosea sehemu/pahala”

Ni maswali magumu kutoka kwa vijana yalijitokeza kuuliza baada ya viongozi na wanazuoni kujikita kufafanua juu ya Utaifa, Uzalendo, Uafrika na utamaduni wetu.

Kutoka Zanzibar mwanamama mmoja machachari alielezea juu ya kuporomoka kwa Maadili ya vijana huku akilaani vitendo vya viongozi kuyafumbia macho mambo ya kipumbavu.

Mfano mkuu alioutumia ni zile hamasa za taasisi za mataifa ya nje zinazotetea ushoga na tamaduni nyingine za ovyo zinazoingizwa nchini ili kuuwa tamaduni na tunu za taifa letu hususani uafrika wetu, alieleza sababu za vijana kushabikia upumbavu huo kuwa ni pamoja na vijana kutoandaliwa kuheshimu mila na desturi za Kiafrika.

Hivyo huwafanya vijana wasipende hata kufanya kazi kama za kilimo na viwandani na kuona ni heri kushiriki mambo kama hayo ya ovyo ili kujipatia fedha kirahisi kuliko kuhangaika na kilimo au kazi za viwandani ambazo mshahara wake ni kwa mwezi na usitoshe kulingana na kazi wanazofanya.

Lakini pia aliongeza kusema kwamba, wale wazungu walishatuibia mila na desturi zetu waafrika na kwenda kuzifanyia maboresho huku wenye misingi hiyo tukiipuuza na kudakia mila za ovyo wanazotuletea ili wafanikishe lango lao Maovu.

Sasa hapo ndipo yalipoibuka maswali kibao kutoka kundi la vijana wasomi, si kwamba walikuwa wakitetea mambo ya kipumbavu, lahasha!

Vijana walitaka kujua iwapo viongozi wa sasa wanaheshimu misingi yote ya Afrika ilikuwaje mambo hayo yakaingizwa nchi za kiafrika na wao wangali hai (wapo)?

Ni kwa nini vita hii wanataka ipiganwe na vijana wa sasa ilihali mambo hayo yanafanyika na kuingia nchini walikuwepo?

Ndipo ilipokuja ile methali/nahau kwamba ….uk…chutama,  Dk. na Mwalimu, Mbunge, Mjumbe wa Halmashauri ya Kamati Kuu Taifa ambaye ni miongoni mwa wajumbe walioshiriki kumtata jina la Dk. Salimu kwa madai kwamba (kwa vigezo), na amewahi kuwa Waziri, Spika wa Bunge la Afrika, Balozi wa Tanzania nchini India na vile vile Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mama mwenye wasifu wa kipekee miongoni mwa wanasiasa kuliko yeyote nchini; alishindwa kumudu hoja za vijana.

Kuzuka kwa hoja kupitia maswali hayo kulikuja kuzimwa au kutulizwa na Waziri wa Habari, Michezo Utamaduni na Sanaa Dk. Mwakyembe ambaye ndiye alikuwa Mgeni Rasimi,  alitumia Uzalendo wake kwa kuueleza ukweli kwamba:-

“Wazungu (Wakoloni) waliondoka Afrika kimkakati, Mwl. Nyerere ndiye alikuwa Rais pekee na wa kwanza kukataa kusaini mikataba yao (waingereza) ya hovyo.

Mikataba hiyo ndiyo inayowatesa nchi kama Kongo na kwingineko juu ya maliasili zao.

Kwa Nyerere alisema, “Rasilimali/Maliasili mfano madini, kwamba haziozi na watanganyika wa sasa kama hawataweza kuwa na nyenzo kwa sasa za kuvuna na kunufaika wao wenyewe, basi vitakuja vizazi vingine ambavyo vitakuwa na uwezo huo.

  Hii ni mali asili ya watanganyika.”

Kuhusu viongozi baada ya akina Nyerere, Dk. Mwakyembe amekiri kosa kwamba, “kosa la sasa katika nchi yetu baada ya watangulizi Baba wa Taifa Mwl. Nyerere ni kurusu mikataba mibovu inayotunyonya.    Wazungu hata mfumo wa elimu barani Afrika waliuacha ni wa kuwaogopa wao (wazungu).

Mwalimu Nyerere tumshukuru sasa, aliliunganisha taifa letu kupitia Lugha ya Kiswahili ili tuwe na sauti kubwa ya kupambana kama Taifa, hapo kabla hatukuweza kuona Mnyakyusa anapigwa na wazungu halafu Mkurya akawa na uchungu kama anayepigwa ni Mtanzania (mtanganyika) mwenzake.

Lakini baaada ya mkakati wa Nyerere kupitia lugha ya kiswahili na kuwafanya wasomi kutoka mikoa mbalimbali kwa makabila mbalimbali kukutana katika shule za Sekondari na vyuo vikuu waliweza pia kuelewana kimakabila.

Nawapongeza wote waliopigania uhuru wa Tanzania na barani Afrika, walio hai na waliotutangulia mbele za haki kwa kazi kubwa ya kutuunganisha.

Tumshukuru sana Nyerere kwa kuipigania lugha ya kiswahili na kupitishwa ktk Umoja wa wa Afrika kuwa lugha ya bara la Afrika na kwamba,  baada ya uamuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuamua kutafuta ushahidi wa na kuifadhi historia ya wapigania uhuru na ukombozi wa Afrika ambapo Tanzania ilipendekezwa na umoja huo kuwa sehemu ya utunzaji wa kumbukumbu hizo, Tanzania kwa sasa ndio Makao Makuu ya Makumbusho ya ukombozi wa Afrika pale sehemu za Kikamboni.

Haya yote ni kwa sababu ya Uzalendo na ushawishi wa Nyerere.

Nyerere na Nkurumah walifika mahala walitofautiana, Nkurumah aligoma Tanzania kuwa sehemu ya uhifadhi na makumbusho ya bara la Afrika na kupendekeza makao makuu yawe Kongo (Zaire)

Siku hiyo ya mkutano wa umoja wa nchi za Afrika Nyerere alikuwa mzungumzaji wa mwisho, aliachana na hotuba yake ya awali baada ya kuona Nkurumah analeta ushawishi wa hovyo kuwa Zaire anayoijua imekaliwa na mfumo wa kikoloni ndiyo iwe mtunza kumbukumbu za wapigania uhuru wa Afrika.!

Nyerere ilimbidi aachane na hotuba ya awali na kuandika nyingina kwa mkono wake siku hiyo hiyo  hadi alipokamilisha, hotuba iliyojaa kurasa 80.

Nyerere akaingia ulingoni kwenda kujibu hoja na kuubadili upepo wa Nkurumah.

Baada ya kuisoma hotuba ile iliyojaa hisia kali Nyerere aliungwa mkono na wajumbe wengi kwa sababu waliutambua mchango wake wa kupigania uhuru wa nchi za Afrika;  Akashinda.

Mimi kama serikali tumeanzisha program ya kufuatilia historia ya Nchi juu ya wapigania uhuru  kupitia wazee wote walioshiriki mapambano wakiwamo kina mama, nasikia mnasema kina mama walikuwa nyuma katika harakati na mapambano hayo, hapana, sio kweli, kina Mama walikuwa mstari wa mbele sana.

Katika wazee tuliowahoji, tumebaki kumhoji Mama mmoja tu nchi nzima ambaye yupo Dodoma (Manyoni) naomba ndani ya wiki mbili mtupe taarifa huyu Mama yuko wapi, asiondoke katika Dunia hii bila kuisikia kauli zake juu ya namna walivyoshiriki,  atuambie walitumia njia ipi alipozuiwa Nyerere na wakoloni kusafiri kupitia Tren kwenda mikoa mingine kuendeleza harakati, na je, baada ya Mama huyo kumvisha hijabu Nyerere akawa kama Mama alitembea kwa mikogo ipi kuingia katika behewa ili wakoloni wasimujue?”

Na nimalizie kwa kusema yafuatayo, “si sahihi kuwalaumu vijana wa leo katika changamoto zao za kimaadili, kiutamaduni na kiuchumi nk.

Ni sisi wenyewe viongozi tuliopo ndio tatizo kuu na ninampango wa kukutana na Waziri wa Elimu ili tubadili mtaala wa Elimu na kuweka somo la Uraia.”

Mzalendo Mwakyembe akahitimisha.

Kwenye Mada ya Uafrika wetu, suala la Utaifa limefafanuliwa kwamba ni jumla ya Sheria, Mila, Tamaduni na Ujamaa kwa ujumla.

Utamaduni maana yake ni yale mambo ya asili ya Jamii,  na  kuhusu Uzalendo,  Uzalendo hujengwa, kwamba mzalendo ni yule ambaye yuko tayali kufia nchi yake, kutokuyumba katika maamzi yake au ya nchi ya pamoja, kuitetea kwa maneno na vitendo.

Nampongeza sana Dk. Mwakyembe kwa kukiri na kutafuta njia ya kujisahihisha, njia pekee ya kujisahihisha ni kuweka somo la uraia katika mitaala ya elimu (mfumo wa elimu) na kuruhusu taasisi zenye muono huo kusambaa nchi nzima kwenda kutoa elimu ya uraia kwa wananchi ambao hawana elimu hii mhimu.

Huo ndio Uzalendo na Ujamaa wa kweli.

Share.

About Author

Leave A Reply