Saturday, August 24

PRESHA JUU USAJILI SIMBA SC YAZIDI KUTAWALA

0


LICHA ya kwamba usajili kwa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara haujaanza rasmi, lakini huko Simba unaambiwa mambo ni moto kwani wameamua kutuliza akili zao ili wasifanye kosa katika zoezi hilo.

Kwa kuanzia, Simba imeamua kuwaita mezani wachezaji wake muhimu wanaomaliza mikataba yao ili kuona namna ya kuwaboreshea masilahi kwa ajili ya msimu unaokuja.

Taarifa kutoka Simba zinadai kuwa John Bocco ambaye Azam wamekuwa wakimfukuzia ili kumrudisha kundini, ameshawekwa mtu kati na mabosi wa Wekundu hao wa Msimbazi na tayari wamekubaliana kila kitu.

Bocco ambaye ni nahodha wa Simba, inasemekana vigogo wa Azam FC, wamekuwa hawalali wakitafuta mbinu za kumrudisha kwenye timu yake hiyo ya zamani, lakini mipango yao hiyo inaonekana kugonga mwamba, baada ya kutengewa donge nono la kuongeza mkataba na Wanamsimbazi.

Mbali na Bocco, taarifa hizo zinadai kuwa Azam pia wanawataka Aishi Manula, Shomari Kapombe pamoja na beki kisiki, Erasto Nyoni, ambao waliamua kuwaacha kwa hiari yao wenyewe na wakadakwa na Simba.

Hata hivyo, taarifa kutoka Simba zinadai kuwa bilionea wao, Mohamed Dewji ‘Mo’, ambaye alikuwa nje ya nchi kwa shughuli zake binafsi, amerejea juzi na kukutana na wachezaji wote waliomaliza mikataba yao wakiwamo akina Bocco.

Pia Haruna Niyonzima ambaye ilisemekana angerudi kwao Rwanda baada ya kuchoshwa na maisha ya Bongo, ameshalainishwa na muda wowote ataongeza mkataba mpya sambamba na Emmanuel Okwi ambaye naye mkataba wake unafikia kikomo msimu huu.

“Taarifa za Azam kuwafukuzia wachezaji wetu tunazo sana, lakini niwahakikishie mashabiki wetu kwamba kila kitu kinakwenda vizuri na muda wowote watasaini mikataba mipya,” alisema kigogo mmoja wa Simba.

Kuhusu wachezaji wanaotemwa, taarifa zinadai kuwa, Zana Coulibaly, Jjuuko Murushid pamoja na Asante Kwasi, hawatabakia salama huku Nicholas Gyan yeye akiwa amebadilisha upepo baada ya kuanza kuonyesha kazi nzuri.

Taarifa hizo zinadai kuwa kama Zana atatemwa, Wekundu hao wa Msimbazi watamrejesha kundini beki wao wa zamani wa kulia, Haruna Shamte, anayekipiga Lipuli FC ili kupambana na Shomari Kapombe, kwenye namba hiyo.

Wenye Simba yao wanadai kwamba katika wachezaji wa ndani, huenda wakasajiliwa wawili tu akiwamo Haruna Shamte na Gadiel Michael wa Yanga, ambaye atakwenda kukabana koo na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ beki wa kushoto.

Share.

About Author

Leave A Reply