Sunday, August 18

HIVI MNAJUA LEO NI SIKU YA FURAHA DUNIANI?

0
Yaani leo ni siku ya furaha duniani, mimi sicheki wala sifurahi, nimetoka kusoma kwenye mtandao kuwa Wabongo hatuko hata kwenye 100 bora ya nchi zenye furaha duniani, na kwa yanayoendelea naona wazi kamwe  hatuji kushuka kuingia hata kundi la nchi mia bora  zenye furaha. Yaani kila upande nikiangalia ni masikitiko tu. Timu yangu ya soka imeshakwama kwenda mbele hapa nimebaki na masikitiko tu. Mwenyewe nilikuwa nashabikia najua mwaka huu furaha tele, wapiii. Benki niliyokuwa nimeweka mkwanja wangu nasikia imefungwa  shida tupu.   Yaani huku barabarani shida tupu, tulipoona serikali inajenga barabara ya kisasa tukakubali hata vibanda vyetu vibomolewe tukajua mbele tutafurahi, mambo yamegeuka. Zile barabara za pembeni ambazo sisi watembea miguu ilitakiwa tujidai bila bugudha zimetekwa na bodaboda na bajaji, ukizubaa unagongwa tu. Mbaya zaidi kuna sehemu machinga nao wameteka barabara basi hapo ukikwepa boda boda unakanyaga bidhaa za mmachinga, au la ujitose barabarani ukanyagwe na gari, sasa nifurahie nini?  Ukifanya kazi wiki nzima kwa bidii ukapata kamkwanja kako ukaamua wikiendi ukaburudike na muziki na bia mbili tatu, kaa chonjo ikifika saa sita kasoro robo utaona patro hiloo, wenyewe wanashuka wanakuja na mibunduki yao mpaka ndani ya baa eti zima muziki, funga baa nendeni kulala, jamani kulala wikiendi saa sita usiku mnadhani tuko kambi ya jeshi? Tena usifikiri unaambia hayo kistaarabu, ni fujo utadhani umeiba almasi, maana ukisikia sauti za hao jamaa na unajua kuwa wana silaha za moto mwenyewe unanywea, jamani sisi ni wabongo wenzenu tunataka kufurahia uhuru tulioupata mwaka 1961. Enzi zile wakati bunduki tulikuwa tunaziona siku za sikukuu wakati wa paredi, mtu akijinyima sana akanunua gari ilikuwa furaha ukoo mzima, siku hizi weeee, unatoka na gari yako kwenye yadi, hata kwenu hujafika unasimamishwa hata mara tano na gari linakaguliwa na kukutwa eti bovu na unatwangwa faini vilevile. Ile raha ya kusema utawatoa mke na watoto wako mkazunguke waende wakaonje gari haipo tena maana inaweza ikakutokea puani kwa kujikuta unafokewa na vyombo vya dola mbele ya watoto wako. Sasa kweli tutaweza kupanda chati ya nchi yenye furaha duniani kwa staili hii?Read More

Share.

About Author

Comments are closed.