Sunday, August 25

WAZIRI JAFO AWATAKA WAKURUGENZI AMBAO HALMASHAURI HAZIKUFIKA ASILIMIA 50 YA UKUSANYAJI MAPATO KUJITATHIMINI

0


Darmpya.com

Dodoma. WAKURUGENZI ambao halmashauri zao zimekusanya mapato chini ya asilimia hamsini wametakiwa kujitathimini, kutokana na kuwa katika hali ya hatari, kufuatia taarifa ya mapato ndani ni kigezo muhimu kwa upimaji wa utendeji kazi wao.

Hayo yamesemwa leo Aprili 26 na Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, wakati akitoa taarifa ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa kipindi cha robo ya tatu Julai/Machi, 2019 kwa mwaka wafedha 2018/19.

“Kuna halmashauri zingine hazitumii mfumo wa kielektoniki na badala yake wanatumia mifumo ya kizamani hali ambayo inasababisha kutokuwa na ripoti nzuri za mapato,” amesema waziri Jafo.

Waziri Jafo amezitaja halmashauri 5 zinazoongoza kwa kigezo cha asilimia ya mapato ya ndani yaliyokusanywa ukilinganisha na makisio ya halmashauri ya mwaka, kuwa ni halmashauri ya wilaya ya Mbozi ikiongoza kwa 113%, ikifuatiwa na wilaya ya Geita kwa 109%, wilaya ya Wanging’ombe kwa 105%, pamoja na wilaya ya Kilolo kwa 103% na halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga 92%.

Aidha, amezitaja halmashauri zilizoongoza kwa kigezo cha pato ghafi (wingi wa mapato), yaliyokusanywa ukilinganisha na makisio ya halmashauri ya mwaka, kuwa ni halmashauri ya jiji la Dodoma ikiongoza kwa shil. bil 49.9, ikifuatiwa na Ilala shil. bil 44.8 , Kinondoni shil bil 23.5, Temeke shil bil 20.6 pamoja na halmashauri ya jiji la Arusha kwa shs. bil 12.5.

Pia, amezitaja halmashauri 5 za mwisho kwa kigezo cha asilimia, kuwa ni halmashauri ya wilaya ya Newala kwa 15%, Tandahimba 15%, Momba 13%, Masasi 13% na halmashauri wilaya ya Nanyamba kwa 12%.

Mbali na hivyo, amezitaja halmashauri tano za mwisho kwa kigezo cha pato ghafi (wingi wa mapato) yaliyokusanywa ukilinganisha na makisio ya halmashauri ya mwaka, ambazo ni halmashauri ya wilaya ya Madaba shs. Mil 293.7,Newala shs. mil 268.3, Kakonko shs. mil 238.6, Buhigwe shs. mil 177.3, pamoja na halmashauri ya wilaya ya Mombi shs mil 170.4.

Katika taarifa hiyo, mikoa iliyoongoza kwa kigezo cha asilimia ya mapato ya ndani yaliyokusanywa ukilinganisha na jumla ya makisio ya halmashauri katika mkoa, ni Iringa (77%), Geita (73%), Dar es Salaam (72%), Dodoma (68%) na Songwe (68%).

Waziri Jafo amesema jiji lilizoongoza kwa kigezo cha pato ghafi (wingi wa mapato), ni jiji la Dar es saalam bil 118.4, ikifuatiwa na Dodoma bil 57.3, Mwanza bil 22.9, Arusha bilion 22.8 na mwisho ni jiji la Mbeya bil 19.8.

Mikoa iliyotajwa kuwa ya mwisho kwa kigezo cha pato ghafi, ni Manyara bil 6.5, Lindi bil 6.1, Rukwa bil 5.8, Kigoma bil 4.5 na mkoa wa Katavi bil 3.8.

Share.

About Author

Leave A Reply