Friday, March 22

Wakili Medium Mwale Ahukumiwa Kwenda Jela Miaka 5 Au Kulipa Faini Ya Milioni 200

0


Image result for wakili medium mwale

WAKILI maarufu Medium Mwale, aliyesota mahabusu kwa zaidi ya miaka saba kwa mashtaka 30 yakiwamo ya utakatishaji fedha na kughushi, amehukumiwa kulipa faini ya Sh. milioni 200, baada ya kukiri makosa.

Mwale alihukumiwa adhabu ya kulipa faini ya Sh. milioni 200, kwa mashtaka mawili ya utakatishaji fedha.

Aidha, alihukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka saba kwa mashtaka 28 yakiwamo ya kughushi nyaraka, kuandaa na kughushi nyaraka za uongo na kukutwa na mali zinazosadikiwa kuwa batili.

Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Isa Maige wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha jana.

Hata hivyo, Jaji Maige, alisema kwa kuwa mshtakiwa tayari amekaa mahabusu tangu mwaka 2011, hivyo, anahesabiwa kuwa amemaliza kutumikia kifungo cha miaka saba jela, lakini, atatakiwa kulipa kiasi hicho cha faini.

Hadi Nipashe inaondoka mahakamani hapo jana jioni, Wakili Mwale alikuwa bado hajafanikiwa kulipa kiasi hicho cha fedha.

“Kwa hiyo hapa mtuhumiwa amekaa miaka saba ndani na amekiri makosa yake, hilo ni jambo jema ambalo amesaidia serikali kuondokana na gharama za kuleta mashahidi 59 wa ndani na nje ya nchi,” alisema Jaji Maige.

Pia alisema hukumu imezingatia maombi ya mshtakiwa kuwa ana mtoto wa miaka minane na mama mzazi wa miaka 78 ambao wanamtegemea.

“Kosa la utakatishaji fedha ni kubwa na halikutegemewa kufanywa na wakili mwenye maadili na kioo cha jamii, hivyo, hukumu yake alipe faini ya Sh. milioni 100 kwa kila kosa, kwa makosa mawili atatakiwa kulipa Sh. milioni 200,” alisema.

Alisema mshtakiwa ni wakili ambaye katika jamii alitakiwa kuwa mfano wa kuiga na mahakama imetoa adhabu hiyo kutokana na mshtakiwa kukiri kwa hiari yake na kwa kufanya hivyo sawa na kujutia makosa aliyofanya na kufanya maungamo ili aokoke.

Aidha, alisema faini hiyo imetolewa kufuatia maombi ya wakili wa utetezi kuwa hali ya uchumi kwa mshtakiwa ni duni kutokana na kukaa ndani miaka saba bila kufanyakazi na kuacha kufanya shughuli za uwakili.

Kuhusu shtaka la kumiliki mali kinyume cha sheria na ombi la serikali kuomba ataifishiwe mali hizo, Jaji Maige, aliwataka upande wa Jamhuri kuandaa maombi na kuorodhesha mali hizo ambazo kwa sasa hawajafanya hivyo, kisha wataangalia cha kufanya.

Mwale alikuwa akitetewa na Wakili Omari Omari na Innocent Mwanga, Novemba 27, mwaka huu, mshtakiwa (Mwale) alikiri kutenda makosa 30.

Upande wa Jamhuri ulikuwa ukiongozwa na Wakili Oswald Tibabyemkomya.

Mapema Septemba 18, mwaka huu, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo Donbosco Gichana, ambaye ni raia wa Kenya, aliachiwa huru katika kesi hiyo baada ya Septemba 13, mwaka huu, kukiri kosa la utakasaji fedha.

Gichana alihukumiwa kulipa faini ya Sh. milioni 300 ambazo alizilipa na hivyo kurudi nchini kwake.

Wakati huohuo, washtakiwa wawili ambao ni Meneja wa Benki CRDB tawi la Mapato jijini Arusha, Boniface Mwimba na Elias Ndejembi, wataendelea na kesi yao Desemba 12, mwaka huu, baada ya kukana makosa yao.

Akiomba kuahirishwa kwa kesi hiyo, Wakili wa Serikali Tibambyekomya, alisema wanahitaji muda wa kukaa na kupunguza makosa na mashahidi kulingana na makosa yanayowakabili washtakiwa waliobaki katika kesi hiyo na hasa baada ya mshtakiwa namba moja kuhukumiwa.

Mwale na wenzake walikamatwa kwa kula njama, kughushi, kutakasa fedha za Dola za Marekani milioni 18 sawa na zaidi ya Sh. bilioni 40, makosa wanayodaiwa kuyafanya kati ya mwaka 2011 na 2012.

Share.

About Author

Leave A Reply