Friday, August 23

Shirika La AGPAHI Lakabidhi Kompyuta Na vifaa Tiba Mkoani Mwanza.

0


Shirika la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) limekabidhi mashine tano kwa ajili ya matibabu ya akina mama wanaogundulika na dalili za awali za maambukizi ya kansa ya shingo ya kizazi (Cryotherapy Machine) katika halmashauri za Sengerema, Kwimba na Ilemela mkoani Mwanza.

Pia shirika hilo limekabidhi kompyuta 18 kwa halmashauri za mkoa wa Mwanza kwa ajili ya kutunzia taarifa za matumizi ya dawa za kufubaza maambukizi ya virusi vya Ukimwi ARV’s pamoja na magonjwa nyemelezi.

Vifaa hivyo vimekabidhiwa hii jana kwenye mkutano wa wadau wanaosaidia mapambano ya Ukimwi mkoani Mwanza, uliofanyika Jijini Mwanza ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la AGPAHI Dr. Sekela Mwakyusa anafafanua zaidi kuhusiana na vifaa hivyo.

Akitoa shukurani kwa niaba ya halmashauri zinazonufaika na vifaa hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mwl.Emmanuel Kipole amelishukuru shirika la AGPAHI kwa kushirikiana na serikali ya Marekani kupitia Centres for Disease Control and Preventation (CDC) kwa kutoa vifaa hivyo.

Awali akifungua mkutano huo wa siku mbili kuanzia, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella amewahimiza washiriki kujadili sababu za maambukizi ya virusi vya Ukimwi kuongezeka mkoani Mwanza ili kutoka na maazimio yatakayosaidia kushusha kiwango cha maambukizi hayo yaliyofikia asilimia 7.2 kwa takwimu za mwaka 2016/17.

Mratibu wa shughuli za Ukimwi mkoani Mwanza Dr.Pius Masele anasema elimu juu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Ukimwi inapaswa kuendelea kutolewa katika jamii na kuhimiza vijana kushirikishwa zaidi kwenye elimu hiyo ikiwemo matumizi sahihi ya kondom pamoja na tohara salama kwa wanaume.

Na BMG Media.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.