Thursday, August 22

Sekretarieti Ya Ajira Yaboresha Mfumo Wa TEHAMA Katika Maombi Ya Kazi.

0


Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yanazidi kukua kadri teknolojia inavyobadilika. Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma katika kuboresha utendaji kazi wake ilianzisha mfumo wa kielektroniki unaojulikana kama ‘Recruitment portal’ unaopatikana kwa anuani ya http://portal.ajira.go.tz ambao unamsaidia muombaji kazi kuingiza taarifa zake na hatimaye kutuma maombi ya kazi kupitia mfumo huo.

Baada ya kuanza kutumia mfumo huo mwaka 2014 Sekretarieti ya Ajira imekuwa ikitoa fursa ya kupokea maoni ya wadau mbalimbali hasa watumiaji na kubaini changamoto kadhaa ambazo zimefanyiwa kazi kwa lengo la kuboresha mfumo ili kuongeza ufanisi.

Kwa mujibu wa Naibu Katibu anayesimamia TEHAMA katika Sekretarieti ya Ajira Mhandisi Samwel Tanguye amesema changamoto katika mfumo huo zilizojitokeza zilihusu maeneo matatu ikiwemo eneo la kuingiza taarifa Binafsi, Taarifa za Anuani, Taarifa za kielimu sambamba na maeneo mengine ambayo imeonekana kuna umuhimu wa kuyaboresha katika mfumo huo ili kukidhi mahitaji ya wadau ikiwa ni pamoja na watumiaji wa mfumo ili kuleta tija katika utendaji kazi wa Sekretarieti ya Ajira.

“Tumefanya maboresho katika mfumo wetu ili kukidhi hitaji la wateja wetu lakini pia ikiwa ni hatua ya  kuendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia, nitumie fursa hii kuwaomba waombaji kazi ambao tayari wana akaunti kwenye ‘portal’ ya ajira (portal.ajira.go.tz) wapitie akaunti zao na kuboresha taarifa zao hasa katika maeneo matatu ambayo ni eneo la taarifa binafsi, taarifa za anuani na taarifa za kielimu ili kuendana na mabadiliko, amefafanua Tanguye”.

Ameongeza kuwa katika maboresho hayo, mfumo huo hautamruhusu mwombaji kazivmwenye elimu ngazi ya astashahada kuomba kazi ambazo zinawahusu wenyevstashahada, mwenye stashahada kuomba kazi zinazowahusu waombaji wenye shahada na pia mwenye shahada hawawezi kuomba kazi zinazohitaji waombaji wenye sifa za stashahada, ama mwenye stashahada hataweza kuomba kazi ya astashahada.

Aidha, maboresho ya Mfumo huo yanawezesha kuwachuja waombaji kazi kulingana na sifa za msingi zilizotolewa katika tangazo la kazi. Kwa mfano endapo moja ya sifa ni umri ama uzoefu, mfumo utawaruhusu wale tu wenye sifa stahiki kuomba kazi hiyo. Pia, endapo tangazo linahusu taaluma “professionals”, basi wasio na “professional” hiyo hawataweza kuomba. Mfano, endapo tangazo linawataka wahasibu wenye CPA, Wahandisi wenye cheti cha Usajili wa bodi ya makandarasi (ERB), Wauguzi wanaopaswa kuwa na cheti ya Bodi ya Wafamasia na Taaluma nyingine zinazofanana na hizo kama hawana vyeti hivyo hawataweza kuomba kazi hiyo.

Na Kassim Nyaki 

Afisa Mawasiliano Sekretarieti ya Ajira.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.