Monday, June 17

Naibu Waziri Wa Fedha Na Mipango Aagiza Mfanyakazi Wa TRA Dodoma Asimamishwe Kazi Kwa Kukiuka Maadili Ya Kazi

0


Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma

NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, kumsimamisha kazi maramoja mfanyakazi wake mmoja katika Ofisi ya TRA mkoa wa Dodoma, DANIEL KINGU, kupisha uchunguzi wa kuhusika kwake na tuhuma zinazomkabili za kumbughudhi mfanyabiashara mmoja Jijini humo.

Dkt. Kijaji, ametoa maagizo hayo baada ya kufanya ziara ya kushitukiza kwenye mitaa ya Jiji la Dodoma baada ya kupata malalamiko kutoka kwa mfanyabiashara mmoja kwamba amekuwa akipokea simu za vitisho kutoka kwa mfanyakazi huyo akishirikiana na watu wengine na kumtaka ampelekee shilingi laki 7 za kulipia mashine ya kutolea stakabadhi za kielektroniki (EFD Machine) la sivyo angefungiwa biashara yake.

“Mteja wetu awe salama!! na nitaendelea kufuatilia, lakini kuanzia muda huu Kingu aondoke ofisini, hatuwezi kuwavumilia watu wa jinsi hii hata kidogo kwa sababu kazi ya kuuza EFD machine si yake na anamwambia mteja aende ofisini kwake chumba namba fulani, anafanya haya mambo ndani ya ofisi ya Serikali, akitoka nje inakuwaje?” alihoji Dkt. Kijaji

Alisema hatasita kuchukua hatua hizo kwa wafanyakazi wengine wa Mamlaka ya Mapato popote walipo nchini wanaojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili.

Naibu Waziri huyo wa Fedha na Mipango, amewataka watendaji wa TRA nchini kote kufanyakazi zao kwa kuzingatia maadili yao ya kazi, kukadiria kodi kwa haki,  watumie lugha nzuri kwa wateja wao na kutoa elimu kwa umma kuhusu haki na wajibu wa wafanyabiashara katika masuala ya kodi badala ya kuwakadiria kodi kubwa isiyolipika.

“Ni lazima tuwalee wafanyabiashara hawa wadogo na ndio watakaotulipa kodi kubwa huko mbeleni badala ya kuwaumiza tangu wanapoanza biashara zao na ni lazima tuangalie viwango vyetu vya kodi tunavyotoza” Alisisitiza Dkt. Kijaji

Meneja wa TRA mkoa wa Dodoma, Bw. Thomas Masese, ameahidi kutekeleza maagizo hayo na kufanya uchunguzi wa kina kuhusu suala hilo huku naye akirejea wito kwa watumishi wa Mamlaka hiyo mkoani humo, kufanyakazi zao bila kuwanyanyasa wafanyabiashara pamoja na kutohusisha na vitendo visivyofaa ikiwemo kuomba rushwa.

Share.

About Author

Leave A Reply